The House of Favourite Newspapers

Mshindi Wa Baba Lao Kupewa Ndinga Lake Wiki Ijayo

0

DIDAS Marik, bingwa aliyelala masikini Jumanne na Jumatano akamka tajiri, kufuatia kushinda gari mpya kupitia bahati nasibu ya Baba Lao, anatarajia kukabidhiwa ndinga yake mapema wiki ijayo.

 

Marik, aliibuka mshindi wa jumla katika droo kubwa ya bahati nasibu hiyo iliyofanyika juzi Jumatano. Ambapo mbali na Marik kuna washindi wengine sita ambao walifanikiwa kushinda fedha taslimu shilingi 50,000.

 

Droo hiyo ilifanyika katika viwanja vya Mabibo Sokoni na kuhudhuriwa na mamia ya watu, ambapo shughuli ya uchanganyaji kuponi hizo ulifanyika hadharani na kusimamiwa na kikosi kazi cha Global Publishers sambamba na Mkaguzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Elibariki Sengasenga.

Mkuu wa Idara ya Usambazaji ya Global Publishers, Anthony Adam alisema kuwa wiki hii unafanyika utaratibu wa kubadilisha kadi ya gari na kusajili vibali hivyo kwa jina la Marik, kisha baada ya hapo utawekwa utaratibu wa namna gani Marik atakabidhiwa gari lake.

 

“Wiki ijayo tunatarajia kumkabidhi mshindi wetu gari yake, wiki hii tunafanya utaratibu wa kusajili gari kwa jina la Marik ili aweze kutambulika kuwa ndiye mmiliki halali, baada ya hapo tutaweka utaratibu mzuri wa namna ya kumkabidhi.

 

“Siku hiyo pia tutawakabidhi na wale washindi wetu wa mikoani pesa zao, wale wa Dar tutakuwa nao kwenye hafla ya kukabidhi gari la mshindi na wao kupewa fedha zao. Naamini tutalitoa mwanzoni mwa wiki ijayo kama utaratibu wa kusajili utakwenda kwa wakati,” alisema Anthony.

Kwa upande wa Marik ambaye kuponi yake iliyoshinda ni ya Gazeti la Championi Ijumaa la Juni 12, 2020, baada ya kupewa taarifa za kufanikiwa kushinda gari hilo alisema: “Kwanza nashukuru, siamini kama leo hii mimi ndiye mtu ambaye naenda kumiliki gari ambayo sikuwahi kuimiliki kabla.

 

“Mwanzo wakati bahati nasibu hii inaanza sikuwa naamini kama ni kweli, lakini hivi sasa nimeamini moja kwa moja kwamba Global Publishers ni waaminifu na wa kweli.

“Mimi ni msomaji mzuri wa magazeti ya Championi, nawaambia wenzangu wasome haya magazeti kwani yanaandika habari za kweli na uhakika kabisa na hakuna janjajanja.

 

”Mbali na Marik ambaye ni mkazi wa Dar, wapo washindi hao sita waliopatikana kupitia droo ndogo ambao ni Khalifa Mwipawa, Seleman Ally Ruzegea, Maulid Ally, Msafiri Mawila ambao wote ni wakazi wa Dar.Wengine ni Mpoki Mwakyusa mkazi wa Mbeya na Kihiyo Hamisi mkazi wa Tanga.

 

Kabla ya kufanyika kwa droo hiyo juzi Jumatano kikosi cha Idara ya Usambazaji kilizunguka katika mitaa mbalimbali ya Dar kuinadi droo hiyo kubwa.Mitaa ya Kimara, Ubungo na Mabibo, wakazi wa eneo hilo walipata nafasi ya kutangaziwa uwepo wa droo hiyo kubwa kutoka kwenye bahati nasibu ambayo ilidumu kwa zaidi ya miezi mitatu.

 

Bahati nasibu hiyo ilianzishwa na Global Publishers kwa lengo la kurudisha kidogo kinachopatikana kwa jamii na watu wote ambao wamekuwa wakiisapoti kampuni ya Global Publishers kwa zaidi ya miaka 20 sasa

Leave A Reply