The House of Favourite Newspapers

MSHTUKO! MUME, MKEWE WAJIUA WASIUONE MWAKA MPYA

WAKATI watu wengi wakiwa kwenye dua kuomba Mungu awafikishe Mwaka Mpya wa 2019, kuna wengine walijiapiza kutouona kwa kuamua kuuana, kisa kikiwa ni wivu wa mapenzi, Uwazi lina kisa kizima.

“Nakuambia bora huo mwaka mpya tusiuone,” mume alimwambia mkewe ambaye naye alidaiwa kumjibu: “Hakuna shida.”

 

Mkazi wa Kijiji cha Kifuru Kata ya Kinyerezi, Ilala jijini Dar, Tobimeni Mahembe maarufu kwa jina la Mnyalu na mpenzi wake aliyefahamika kwa jina moja la Elizabeth au Eliza wamefia ndani ya nyumba yao baada ya kuteketea kwa moto ambao unatajwa kuwa ni wa kujilipua.

Mmoja kati ya majirani (jina linahifadhiwa) aliliambia Uwazi kuwa, kabla ya tukio hilo ambalo lilijiri Desemba 26, mwaka uliopita, kulitanguliwa na purukushani za ugomvi baina ya wapenzi hao.

“Nilisikia mwanaume akimwambia mwenzake kwamba kwa kuwa anajifanya mjanja, wote hawatauona mwaka mpya, inaonekana walikuwa wakigombana kwa sababu ya wivu wa kimapenzi.

 

“Kingine inaonekana walipigana sana kabla ya nyumba kuchomwa na kusema kweli haijulikani nani aliichoma maana maiti zote zimekutwa kitandani,” alisema jirani huyo.

Akizungumza na Uwazi, mtoto wa kaka wa Tobimeni, Gatrude Maembe alisema kuwa, alipigiwa simu na baba yake ambaye ni kaka wa marehemu akimwambia kuwa aende kwa baba yake mdogo kwa kuwa nyumba yake ilikuwa imewaka moto na amefariki dunia pamoja na mkewe.

“Ikabidi nije, nikakuta hali ndiyo kama hiyo, baba mdogo pamoja na mke wake wamefia ndani na vitu vyote vimeteketea.

“Lakini sisi kama familia tulikuwa hatujui kama baba mdogo alikuwa akiishi na mke ni kwamba taarifa hizi tumezipata hapa kwa majirani, kuwa kuna binti alikuwa anaishi naye na pia nyumbani kwao hakuna anayepajua na jina lake tulifanikiwa kulijua ni moja tu la Eliza.

“Kwa hiyo hadi sasa ndugu wa Eliza hatujui wako wapi na hatujui tutafanyaje kwa sababu hata taarifa hazijawafikia,” alisema.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kifuru, Joseph Kanuti alisema kuwa, alipigiwa simu na Mwanyekiti wa Mtaa wa Kifuru, Michael Msome akimueleza kuwa kuna nyumba imeungua na watu wamefariki dunia.

 

“Nilipigiwa simu na mwenyekiti akiniambia kuwa kuna nyumba inaungua na watu wamefia ndani, ikabidi twende eneo la tukio nikiwa na wenzangu.

“Tulifika pale muda wa saa 7:43 usiku nikiwa na mwenyekiti pamoja na majirani, ikabidi tuuzime moto kwa kutumia mchanga, tulifanikiwa kisha tukabomoa mlango tukaingia ndani.

“Tulipofika kule tukamkuta mwanaume akiwa amelala kitandani ameungua moto mwili mzima na mwili wa mwanamke ukiwa unaning’inia kwenye kitanda, nao ukiwa umeunga maeneo ya kuanzia miguuni hadi kiunoni.

 

“Ikabidi tupige simu polisi na kuendelea kuuliza majirani huenda kuna kitu walikisikia kutoka kwa hawa marehemu kwa kuwa walikuwa wakiishi wawili tu na huyo mwanamke ana miezi mitano tu tangu afike pale na kwamba inasemekana kwao ni Kigamboni jijini Dar.

“Majirani wakatuambia kuwa walisikia ugomvi kati ya wawili hao jana yake na mwanamke aliondoka, lakini ilipofika muda wa saa kumi na moja jioni alirudi akiwa na mumewe ikionesha kwamba huenda aliondoka na kwamba mumewe alimfuata kwao na kuyamaliza.

 

“Tulipata shida sana kupata namba za ndugu kwa kuwa vitu viliungua, tukabahatisha kupata kidaftari kidogo ambacho tulipekua tukakuta namba ya simu, lakini tulipoipiga ile namba kuna mtu aliipokea, tulipomwambia kuwa anamfahamu yule marehemu alijibu kuwa hamfahamu kisha akakata simu.

“Ikabidi tujaribu namba nyingine huyo yeye alituambia kuwa ni ndugu yake, lakini akatutumia namba zingine tumtafute mtu mwingine aliyedaiwa kuwa ni kaka wa marehemu, tukampigia, kweli tulifanikiwa hatimaye walifika muda wa saa 10:45 alfajiri.

 

“Na baadaye polisi waliweza kufika na kuingia kuanza kukagua, walipomtazama mwanamke wakatuambia kuwa inaonesha alipigwa na kitu maeneo ya kisogono na damu zilikuwa zimetapakaa pale chini kwa hiyo inaonesha kuna mmoja alifanya tukio kisha kulipua nyumba.

“Polisi walipozunguka nje ya nyumba walizikuta simu za marehemu zikiwa zimefichwa kwenye mabomba ambayo yako nje ya nyumba, inawezekana kulikuwa na ugomvi mmoja wao akachukua zile simu na kuzificha huko,” alisema Joseph.

 

Naye kaka wa mume aliyejitambulisha kwa jina la Stanley Charles Mahembe alisema, alijulishwa tukio hilo kwa njia ya simu na akaja nyumbani wa mdogo wake na kukuta tukio hilo la kusikitisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishina Msaidizi ACP Salum Hamduni alithibisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

“Kama kuna mwananchi yeyote anayefahamu chochote kinachohusiana na kifo chao tunaomba atusaidie katika upelelezi wetu,” alisema kamanda huyo.

STORI: NEEMA ADRIAN NA RICHARD BUKOS, DAR

 

 

Comments are closed.