The House of Favourite Newspapers

Msigwa Kuhusu Tozo: Huwezi Kwenda Mbinguni Bila Kufa – Video

0

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amefananua matumizi ya tozo maalum ya miamala ya simu kwa kutaja maeneo matatu muhimu ambayo zinakwenda kufanya kazi kuchochea maendeleo.

 

Akizungumza katika kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255 Global Radio mapema leo, Msigwa alisema, tozo hiyo ni maalum na itakwenda kuboresha katika sekta ya Afya, Maji na ujenzi wa barabara.

 

“Wadau wa masuala yanayowahusu Watanzania ni Watanzania wenyewe, mfano suala la tozo, wadau ni wale wanaohusika na miamala. Maoni ya wadau ya kupanua wigo wa kodi yametolewa katika maeneo mengi, jambo hili lililpelekwa Bungeni sababu ndio wawakilishi wa wananchi.

Meneja TEHAMA wa Global Publishers, Edwin Lindege akimpa maelezo Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.

“Baada ya kupelekwa Bungeni, Bunge likapitisha, Waziri akatunga kanuni na jambo likaanza kutekelezwa, lakini baada ya kuibuka malalamiko ya wananchi, Mhe Rais akaagiza hivyo wataalam wakajichimbia na jana wametoa ripoti ya kwanza kwa Waziri Mkuu.

 

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na vituo vya afya mpaka vijijini, kuhakikisha maji yanapatikana lakini zaidi tujenge barabara za kuunganisha vijiji.

 

“Huwezi kwenda mbinguni bila kufa, huwezi kutarajia kujengewa barabara bila kutoa pesa, huo ndio ukweli, lazima utoe pesa ili ujengewe barabara, kinyume chake usiwe na barabara, usiwe na matibabu. Watu wanazungumzia kutoza tozo hawazungumzii kukosa huduma.

Msigwa akisalimiana na Kiongozi Msaidizi wa Idara ya Global TV, Kelvin Nyorobi.

“Serikali inapata pesa kwenye madini na maeneo mengine kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Haya mambo ukiyatekeleza kwa mpango wa kawaida unaweza kumaliza hata miaka 20, mama zetu wanakufa kwa kukosa huduma. Hatuwezi kusubiri mpango wa kukusanya ndipo zikagawanywe.

 

Haya malalamiko ya tozo asilimia kubwa yapo mjini tu, vijijini ambako kuna shida ya barabara, maji na ndiko pesa hii itakwenda kutumika wamefurahi sana. Ukiwa hapa Dar huwezi kujua, lakini kule vijijini kwenye dimwbi moja ng’ombe anakunywa hapo na binadamu anakunywa.,’ alisema Msigwa.

 

“Hii ni tozo maalum, tutakwenda nayo mpaka pale tutakaoona tumekamilisha haya mambo tuliyoyakusudia kuyafanya ndipo tutaangalia vinginevyo kama ni kupunguza au kuondoa.

“Vipaumbele vya fedha hizi za tozo ni huduma za afya, tunataka tumazlie kabisa hili tatizo la vituo vya afya na vilivyopo tuvipelekee dawa na vifaa tiba, X-Rays, CT-scan, MRI na vingine vingi, nchi yetu tunakwenda kuwa na utalii wa matibabu (medicine tourism).’ alisema Msigwa.

 

Tunataka kupeleka pesa za tozo kwenye maji, nchi hii ina tatizo kubwa sana la maji, pia tunapeleka kwenye barabara vijijini, tumalize matatizo ya barabara, na kwenye mpango huu lengo letu ni kukusanya Tsh tril 1.254.

 

Msigwa alizungumzia pia kuhusu uchumi wa nchi ambapo alisema, huko nyuma nchi ilikuwa ikikua kwa asilimia 7. 2 lakini kwa sasa unakua kwa asilimia 4.8 ambapo alisema si mbaya sana kwa kulinganisha na nchi za wenzetu hususan za jirani.

 

“Kutokana na na janga la Corona, wapo wenzetu wa nchi za jirani uchumi wao unakua kwa asilimia hasi hivyo Tanzania bado iko vizuri,” alisema.

Stori: Erick Evarist

Leave A Reply