The House of Favourite Newspapers

Mtibwa: Tumejipanga Kutwaa Kombe

0
Kikosi cha timu ya Yanga.

 

KUFUATIA mfululizo wa kukaa kileleni mwa Ligi Kuu Bara kila msimu unapoanza, Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amezungumzia siri ya mafanikio na mbinu hizo huku akiweka bayana mipango yake ya kutwaa kombe hilo.

 

Mtibwa ambayo hadi sasa ina jumla ya pointi 11 na mabao matano baada ya kung’olewa kileleni na Simba kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, imekuwa ni klabu pekee kuwa na mwendelezo wa kuanza ligi ikiongoza usukani zaidi ya misimu mitatu sasa pamoja na kuwa chini ya makocha mbalimbali.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Katwila amesema kuwa ili waweze kuwa mabingwa wanatakiwa kuhakikisha wanashinda michezo yote ya nyumbani na ugenini na inapotokea wameshindwa kabisa kupata matokeo ya ushindi basi njia pekee ni kuhakikisha wanapata angalau sare.

“Kumekuwa na maswali mengi sana juu ya timu yetu kuongoza ligi mwanzo wa msimu na baadaye kuonekana ikishuka jambo ambalo baadhi ya watu wamekuwa wakidhani tunapanga kufanya hivyo ili kujinusuru na kushuka daraja kitu ambacho si kweli.

 

“Wanachotakiwa kuelewa ni kwamba, siku zote mbinu zetu zimekuwa ni kushinda kila mchezo na ikiwezekana kutwaa kombe la ligi, ila mara kadhaa tumekuwa tukigonga mwamba kufuatia kikosi chetu kuporwa wachezaji na mara nyingine kujikuta wapinzani nao wakitukamia kwa kujipanga vizuri.

 

“Njia nyingine ambayo mimi naamini kwa mwaka huu itaweza kutupa ubingwa ni uwepo wa wachezaji wangu wakongwe ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa ni sehemu ya makocha pale mechi inapochezwa kwa kunisaidia kuwaongoza vijana ambao hawana uzoefu mkubwa.

 

“Unajua wazi kuwa Mtibwa imekuwa na kawaida ya kupandisha vijana wadogo kila mwaka na kwamba wamekuwa wakifanya vyema tofauti na timu nyingine, hivyo kuwafanya waweze kupambana ni lazima uwe na watu wazoefu wa ligi kama ilivyo kwa Shabani Nditi na Henry Joseph ambao wamecheza ligi kwa muda mrefu.

 

“Kutokuwa na kikosi cha watu wazoefu kama hawa ndiyo chachu ya kutoweza kufanya vyema hasa unapokuwa na kikosi cha vijana wengi kwani utacheza bila washauri ndani ya uwanja jambo ambalo limekuwa likiwashinda wengi kukuza vipaji vichanga kama ilivyo kwa klabu za Simba na Yanga.

 

“Mimi nimekuwa muumini wa hili tangu niwe kocha msaidizi na sasa naongoza timu kama kocha mkuu, kuna faida kubwa sana unapokuwa na wazoefu ndani ya klabu na hili ni jambo la kujivunia kwani sisi tumekuwa na kawaida ya kuwapa nafasi jambo ambalo linawafanya hata wao kutusaidia kazi makocha kwa moyo wote na ndiyo maana mtu anapotokea Mtibwa hata akienda wapi siku anapoachwa anaona ni vyema kurejea nyumbani kutokana na umoja uliopo.

 

“Najua ligi ya mwaka huu ni ngumu kutokana na klabu nyingi kuwa na uwezo wa kujiendesha kwa kuwa zimepata udhamini, ila hata TFF inaonekana kujipanga vyema juu ya kuwahisha fedha za uendeshaji, lakini hili halitatufanya tushindwe kupigania ubingwa kwani nia yetu ni kuona tunatwaa kombe kabisa hata ikishindikana basi tumalize kwenye nafasi inayoweza kutufanya tucheze michuano ya kimataifa.

 

“Kweli Simba wamekwea kileleni kwa tofauti ya mabao jambo ambalo sisi halitaweza kutukatisha tamaa kwani nia yetu ni kusaka pointi tatu kila mchezo na hiyo ndiyo siri ya mafanikio ambayo mimi na wenzangu tumekuwa tukijipangia kufanya hivyo, maana hakuna timu yenye uhakika wa kushinda michezo yote au kutufunga.

 

“Hadi sasa utaona tumeendelea kusimamia hili kwa kutokubali kabisa kupoteza mchezo wowote uliopo mbele yetu lengo likibaki kutwaa ubingwa kama Mungu atatujalia hivyo, maana saa nyingine matokeo mazuri huambatana na bahati kutoka kwake, jambo la kujituma ni la pili maana unaweza kupambana ila kama Mungu hajakujalia basi utaishia kupoteza.

 

“Nitumie fursa hii kuwaambia wapenzi na mashabiki wetu kuwa hatuna nia ya kuongoza mwanzo wa msimu tu kisha tupotee nia yetu ni kuwa mabingwa wa ligi, hivyo waendelee kutuamini na kutupa moyo kwani mipango yetu kama benchi la ufundi na wachezaji wote ni kuona mwisho wa ligi tunaibuka mabingwa kwani ndiyo lengo kubwa na nia ya kila mmoja wetu,” anasema Katwila.

Leave A Reply