The House of Favourite Newspapers

MTOTO: BABA AMENIBAKA MPAKA BASI

INASIKITISHA! Mwanaume mmoja anayejulikana kwa jina la David, mkazi wa Msongola jijini Dar amefanya kitendo cha kinyama baada ya kudaiwa kumuingilia kimwili ‘kumbaka’ mtoto wake wa kufikia (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili).

 

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 16 ambaye baba huyo alimlea tangu akiwa na umri wa miaka 6, alieleza kuwa amekuwa akibakwa na baba yake huyo mara kadhaa.

Akiendelea kusimulia kwa huzuni mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule moja iliyopo Dar, alisema kuwa baba yake huyo ameanza kumbaka tangu akiwa darasa la tatu na mara nyingi kitendo hicho kinafanyika wakati mama yake akiwa kwenye mihangaiko yake.

 

“Baba amekuwa akinibaka mpaka basi na anafanya hivyo wakati mama akiwa hayupo, maana nilikuwa ninaishi naye mimi na mama tu hivyo mama akitoka kwenda kwenye biashara zake huko Msongola-Magengeni, baba amekuwa akinifanyia mchezo huu mbaya,” alisema mtoto huyo.

 

Mtoto huyo alibainisha kuwa mara nyingi baba yake amekuwa akimtisha kwa kisu au kumpiga wakati anataka kumuingilia, jambo ambalo lilimfanya aogope na hata ashindwe kusoma vizuri shuleni. “Baba amekuwa akinitishia nikikataa kufanya naye kitendo hicho na alikuwa akiniambia nikisema kwa mtu yeyote atanichoma kisu,” alisema mtoto huyo.

 

Hata hivyo, alisema aliwahi kumwambia bibi yake mzaa-mama ambaye amefariki dunia wiki mbili zilizopita, lakini bibi yake huyo alimwambia anyamaze kwa sababu akisema anaweza kufungwa halafu wakakosa mtu wa kuwahudumia chakula hapo nyumbani.

 

MAMA WA MTOTO ATOA MACHOZI

Mama wa mtoto huyo, Arafa Mohamed, alisema amesikitishwa na kitendo alichofanya mumewe huyo, kwani alikuwa akimuamini mno na alikuwa akimlea mtoto wao huyo kama mwanaye aliyemzaa na yeye hakuwa anajua kama kuna kitendo kama hicho kinaendelea kwa sababu mara nyingi anakuwa yuko kwenye biashara zake.

 

“Baada ya kujua kitendo alichofanya mume wangu nimeumia sana na kama mama nashindwa hata nifanye nini maana baada ya siri hiyo kugundulika siku ya msiba wa mama yangu mzazi, nilitamani hata kunywa sumu maana ni kitendo cha fedheha sana, lakini kwa sababu tayari mume wangu huyo yuko mikononi mwa Polisi namshukuru Mungu sana na sheria ifuate mkondo wake,” alisema mama huyo.

 

Aliendelea kueleza kuwa angejua suala hilo kwa muda mrefu, angeshaachana na mume wake huyo kwani wameishi kwa miaka tisa hakujua chochote. Pamoja na ujinga huo, mama huyo alieleza kuwa anamshukuru Mungu baada ya mtoto huyo kumpima na kukuta hana tatizo lingine, ikiwemo maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

 

BABA MDOGO NAYE AELEZA MACHUNGU YAKE

Baba mdogo wa mtoto huyo, Ramadhan Amini ambaye ni shemeji wa mama yake alisema kuwa walianza kugundua uchafu huo unaofanywa na David, siku ya msiba wa mama mkwe wake ambapo baba huyo hakulala msibani na pia alimchukua mtoto huyo na kwenda naye kulala nyumbani na kumfanyia vitendo hivyo.

 

“Unajua mwanzoni tulikuwa tukisikia kwa kificho sana kwamba huyo baba kuna mchezo anamfanyia mtoto huyo, lakini ukweli ulijiweka wazi siku ya msiba wa bibi yake tukashangaa tu kamchukua mtoto na kuondoka naye kulala nyumbani, jambo ambalo siyo la kawaida, ndiyo tukaitisha kikao mtoto akaeleza kila kitu kwa mara kwanza ambapo na yeye mhusika alipoulizwa kwa sababu alikuwepo akajibu kama alivyohadithia mtoto,” alisema.

 

Baada ya kikao hicho cha familia, waliamua mtoto atoke pale nyumbani na kwenda kukaa kwake ambako ilikuwa kila siku baba huyo alikuwa akija mpaka na visu kumtishia kuwa anamtaka mtoto huyo arudi nyumbani, jambo ambalo lilimkera na kumlazimu apeleke jambo hilo Serikali ya mtaa.

 

“Kiukweli nilikuwa sina raha hata kidogo na familia yangu, yule baba alikuwa akifanya fujo sana akimtaka mtoto arudi nyumbani. Ilibidi sasa nichukue hatua zaidi kwenda kuripoti Serikali ya mtaa. “Kule wakatuma mtu aende kumkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi cha Msongola na baadaye kupelekwa Kituo cha Polisi cha Chanika. Huko Chanika tulipewa hati ya taarifa namba CNK/RB/4846/2018,” alisema baba mdogo huyo.

 

Gazeti hili lilienda mpaka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msongola aliyejitambulisha kwa jina moja la Misheshe ambaye alithibitisha na kufafanua kuwa tayari suala hilo liko Polisi.

STORI: Imelda Mtema , DAR

Comments are closed.