The House of Favourite Newspapers

MTOTO WA MUNA AWATOA MACHOZI MASTAA !

DAR ES SALAAM: Machozi! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mastaa mbalimbali wa filamu na wadau akiwemo mtangazaji Zamaradi Mketema kujikuta wakitoa machozi ya kumsikitikia mtoto wa msanii wa filamu, Rose Alfonce ‘Muna’ anayejulikana kwa jina la Patrick ambaye yupo mahututi nchini Nairobi alipolazwa kutokana na kusumbuliwa na uvimbe kichwani.

 

Mastaa hao walionekana kuguswa na hali mbaya aliyonayo mtoto huyo na kuamua kumuweka kwenye maombi huku wakichangisha fedha kwa ajili ya matibabu kwani kwa siku sita tu za awali alizokaa hospitalini zinatakiwa shilingi milioni 22.

 

ZAMARADI AJITOA KUHAMASISHA

Zamaradi aliamua kuanzisha zoezi la mchango kwa kila Mtanzania atakayeguswa amchangie kwa chochote alichonacho na kudai kuwa alifanya hivyo kwa sababu anajua wazi kuwa anahitaji kusaidiwa kutokana na jinsi alivyohangaika na mwanaye na fedha nyingi zimetumika kwenye matibabu hayo mpaka sasa.

 

“Wapenzi mwenzetu yuko kwenye mtihani mzito, anauguza mtoto wake na yuko Hospitali Nairobi huku mtoto akiwa ICU, tunaelewa kuuguza ni nini hata kama una kitu  bado hakitatosha.

“Dawa anazotumia mtoto kwa siku hizi sita zilizopita anadaiwa milioni 22 na bado zinaongezeka, nimeongea naye kuhusiana na pale tunapoweza amekubali tumsaidie jamani,” alisema Zamaradi.

WEMA AMALIZA BIFU LAKE NA MUNA

Kutokana na ugonjwa wa mtoto huyo kushtua wengi pamoja na mastaa mbalimbali kumposti kwenye kurasa zao wakimuombea Mungu amponye, Wema naye aliamua kumaliza bifu lake na Muna na kumuombea maombi ya kumponya pia akamchangia pesa ikiwa ni ushawishi wa wengine nao kumchangia.

 

“Tunamuombea kipenzi Muna… Pat bado ana safari ndefu sana… ana ndoto nyingi sana anazotakiwa kutimiza…na ana mengi anayotakiwa hakika Mungu atamsaidia,” aliandika Wema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

 

Msanii mwingine aliyeonekana kumuombea Pat kwa masikitiko makubwa alikuwa ni Halima Yahya ‘Davina’ ambaye alidai kuwa ameumizwa kama mzazi na anamuombea mtoto huyo apone haraka ili kurejesha furaha ya mama yake.

 

“Jamani namuombea mtoto wa Muna apone haraka kwani atarejesha furaha ya mama yake, mimi ninasikitishwa na afya ya mwanaye kwani mimi pia ni mzazi jamani lakini naamini Mungu atatenda miujiza yake,” alisema Davina.

JOHARI NAYE AMLILIA

Mwingine aliyeonesha kuguswa ni pamoja na Blandina Chagula ‘Johari’ ambaye aliliambia Amani kuwa, kama wasanii wanajitahidi kujipiga piga na Watanzania kwa jumla ili kumsaidia pia kikubwa kumuweka kwenye maombi anaamini hakuna kinachoshindikana kwa Mungu.

 

“Unajua kwa Mungu hakuna kinachoshindikana, naamini Mungu atamponya tu kwani tunamuombea apone haraka ili amrudishie faraja mama yake, huwezi amini nimejikuta naangua machozi nikitafakari jinsi mtoto huyu anavyoumwa,” alisema Johari.

 

Wasanii walioonesha kumuombea ni wengi ukitaja idadi yao inaweza kujaa hapa kwani mbali na Patrick kuwa mtoto wa msanii mwenzao Muna lakini ni mtoto ambaye wamekuwa naye hata kwenye baadhi ya filamu pia amekuwa akijumuika nao kwenye matangazo kama msanii mtoto.

 

MUNA AWAOMBA WATANZANIA WAMSAIDIE

Gazeti la Amani baada ya kuongea na wasanii mbalimbali walionesha kuhuzunishwa na hali ya mtoto huyo lilizungumza na Muna kwa njia ya simu ambapo alieleza kwa kifupi kuwa mwanaye anasumbuliwa na uvimbe kichwani na hali yake ni mbaya hivyo anaomba kwa anayeweza kumsaidia amtumie chochote alichonacho kupitia akaunti yake ya benki ya CRDB: 01j2096190100 jina ROSE ALPHONCE NUNGU Au unaweza kumchangia kupitia namba ya kawaida ya simu; 0718814581 jina Rose Nungu.

 

NENO LA MHARIRI

Gazeti hili linaungana na watu wote walioguswa na kumpa pole Muna lakini pia linamuombea mtoto wake apone haraka.

Comments are closed.