The House of Favourite Newspapers

MTU WA AJABU DUNIANI! ANAKULA UGALI, MAYAI NA MAGANDA YAKE

KWA watu wengi, mayai yaliyochemshwa ni chakula kitamu na yanaweza kuliwa wakati wowote, asubuhi, mchana ama usiku.   Isaac Nyamwamu, mkazi wa eneo la Roysambu jijini Nairobi, Kenya, amegundua njia bora zaidi ya kula utamu wote wa mayai; anayala yote, pamoja na maganda yake.

Waandishi wa taasisi ya TUKO wanaandika kuhusiana na jamaa huyo.

Tulipomtembelea  nyumbani kwake majuzi, Nyamwamu amedai hadi sasa ni mwaka wa nane tangu aanze kula mayai na maganda yake, jambo alilosema hata yeye lilimshangaza alipoanza kufanya hivyo.

“Nilianza  kula mayai na maganda yake mwaka 2010.  Kaka na marafiki zangu walishangazwa na jambo hilo, lakini sikuacha kuyala maganda kwani ni matamu,” anasema.

Kila siku mkewe humtayarishia mayai saba ambayo huyala kukidhi njaa yake.

“Kuna wakati nilikwenda kumwona daktari kutaka kujua iwapo maganda ya mayai yana athari za kiafya kwangu, lakini alinihakikishia kwamba afya yangu ni nzuri tu,” alisema na kuongeza utani kwamba mlo huo humwongezea nguvu na ujuzi akiwa faragha na mama-watoto wake.

Tukiwa tunaongea naye mkewe alileta chakula ambacho ni ugali, kachumbari na mayai.  Tulikaribishwa na kuanza kula. Tulikula ugali, mayai na kachumbari tu, tukayakwepa maganda.  Lakini Nyamwamu, kama kawaida yake, alikula ugali, mayai na maganda yake huku akitoweza kwa kachumbari.

“Nachukulia jambo hili kama kipaji na nafikiri kuna siku nitaingia katika kitabu cha rekodi za dunia — Guinness Book of Record,” anasema akitarajia kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ili amwonyeshe kipaji hicho.

“Hamu yangu ya kupenda maganda ya mayai inaongezeka kila mara.  Karibuni nitaanza kula mayai kumi kwa siku,” anasema.

Comments are closed.