The House of Favourite Newspapers

Mtu wa Kwanza Kutibiwa HIV Afariki kwa Saratani

0

MTU  wa kwanza kutibiwa virusi vya ukimwi (HIV), Timothy Ray Brown, amefariki kutokana na saratani. Brown ambaye pia alijulikana kama mgonjwa wa Berlin alipandikizwa uboho (yaani “bone marrow”, chembe za damu zinazokaa ndani ya mfupa wa binadamu au mnyama yeyote) kutoka kwa mtu ambaye alikuwa na kinga dhidi ya HIV 2017.

 

Hii ilimaanisha kwamba alikuwa hahitaji tena dawa za kukabiliana na virusi vya ukimwi, hivyo alisalia bila maambukizi yoyote ya virusi hivyo vinavyosababisha ukimwi kwa maisha yake yote.

 

Shirika la kimataifa kuhusu wagonjwa wa ukimwi duniani limesema kwamba Brown aliupatia ulimwengu matumaini kwamba dawa ya kutibu ukimwi inaweza kupatikana.

 

Brown mwenye umri wa miaka 54, ambaye alizaliwa nchini Marekani na alipatikana na virusi vya HIV alipokuwa akiishi Berlin 1995.

 

Na baadaye mwaka 2007 alipata saratani ya damu inayojulikana kwa jina la Myeloid Leukemia. Tiba yake ilianza kuharibu uboho wake ambao ulikuwa ukizalisha seli hizo za saratani kabla ya kufanyia upandikizaji. Uboho huo ulitoka kwa mfadhili ambaye alikuwa na mabadiliko nadra katika sehemu ya DNA iitwayo jeni ya CCR5.

 

Kinga dhidi ya HIV

CCR5 ni seti yenye maagizo ya jeni ambayo huunda mlango ambao virusi vya ukimwi (VVU) huingia kuambukiza seli. Mabadiliko ya CCR5 kimsingi hufunga mlango na kuwapa watu kinga dhidi ya VVU.

“Niliacha kula dawa siku ambayo nilifanyiwa upandikizaji  na baada ya miezi mitatu sikuwa na virusi vya ukimwi mwilini mwangu,”  Brown aliambia BBC mwaka 2012.

 

Virusi havikugundulika mwilini mwake tena. Kwa kweli alikuwa “amepona”, zilionyesha duru za kitaalam.

 

Lakini saratani ya damu ambayo ilisababisha kupona VVU, ilirudi mapema mwaka huu na kuenea kwenye ubongo wake na uti wa mgongo.

“Ni kwa masikitiko makubwa kwamba ninatangaza kifo cha Timothy ambaye aliaga dunia … akiwa amezungukwa na mimi na marafiki, baada ya vita vya miezi mitano na saratani ya damu,” mwenzake Tim Hoeffgen aliandika kwenye Facebook.

 

Aliongeza: “Tim alitumikia maisha yake kusimulia hadithi yake juu ya tiba yake ya VVU na kuwa balozi wa matumaini.”

 

Je tunakaribia kupata tiba?

Tiba ya  Brown ilikuwa hatari sana kutumika mara kwa mara – inasalia kuwa tiba ya saratani. Njia hiyo pia ni ghali sana kwa watu milioni 38, wengi wao wanaoishi kusini mwa Jangwa la Sahara na  wanaofikiriwa kuishi na maambukizi ya VVU.

Hata hivyo, simulizi ya Brown iliwapatia msukumo wanasayansi na wagonjwa na ulimwengu kwamba tiba inaweza kupatikana. Jumuiya ya Ukimwi ya Kimataifa (IAS) ilisema ilikuwa ikiomboleza na “moyo mzito sana” kuhusu tukio hilo.

 

“Timothy na daktari wake, Gero Hutter, wanatudai shukrani kubwa kwa kufungua mlango kwa wanasayansi kuchunguza dhana kwamba tiba ya VVU inaweza kupatikana,” alisema Prof Adeeba Kamarulzaman, rais wa IAS.

Mgonjwa wa pili aliyepona VVU alitangazwa mapema mwaka huu. Adam Castillejo – anayejulikana kama mgonjwa wa London – alipatiwa matibabu sawa na yale ya  Brown na aliacha kutumia dawa zake za VVU.

Leave A Reply