The House of Favourite Newspapers

Mtunisia Aleta Vifaa Vipya Yanga, Wachezaji Wapya Wajipange!

0
Daktari Mkuu wa Yanga, Mtunisia Youssef Ammar (kulia).

YANGA hawataki kufanya makosa katika usajili wa msimu ujao baada ya Daktari Mkuu wa timu hiyo, Mtunisia Youssef Ammar, kuweka wazi kuwa, vifaa maalum vitatumika kabla ya mchezaji yeyote kupewa mkataba huku akiahidi kulisimamia hilo kwa umakini mkubwa.

 

Tayari wapo baadhi ya wachezaji wanatajwa kuwaniwa na Yanga katika kuelekea msimu ujao ambao ni Victorien Adebayor anayekipiga US Gendarmerie ya Niger, Stephan Aziz Ki wa Asec Mimosas ya Ivory Coast.

 

Wengine ni Moses Phiri anayeichezea Zanaco ya nchini Zambia na Mkongomani Francy Kazadi Kasengu anayecheza EL Gaish ya Misri kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco sambamba na Mtanzania, Simon Msuva.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Ammar alisema kuwa, katika kuelekea usajili wa msimu ujao, kama benchi la ufundi hawataki kufanya makosa kama yaliyojitokeza katika msimu huu ya kuwasajili wachezaji baadhi bila ya kuwafanyia vipimo.

 

Ammar alisema kuwa katika msimu huu wamepanga kutumia vifaa maalum vitakavyotumika kuwapima wachezaji wao wapya kabla ya kuwasajili na hilo tayari amemwambia Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi na Kamati ya Mashindano ya Yanga.

 

Aliongeza kuwa katika msimu huu walifanya kosa hilo kwenye usajili wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Denis Nkane ambaye hakufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kupewa mkataba.

 

“Katika msimu huu tulifanya makosa kwa Nkane ambaye tulimsajili akiwa na majeraha ambayo alitoka nayo Biashara United aliyokuwa anaichezea huko kabla ya kusajiliwa Yanga.

 

“Kama unakumbuka wakati anajiunga tulikuwa tunakwenda katika Kombe la Mapinduzi ambako alicheza mchezo mmoja na kujitonyesha, akakaa nje kwa wiki kadhaa na kurejea uwanjani baada ya kumpatia matibabu.

 

“Hivyo tunakwenda katika usajili wa msimu ujao, hatutaki kuona hilo likitokea na hiyo imetokana na presha ya usajili wakati uongozi ukikapambana na muda wa kufungwa dirisha, lakini msimu huu hatutafanya usajili wa presha.

 

“Hiyo itatusaidia kupunguza idadi kubwa ya majeruhi katika timu, mfano msimu huu tulikuwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye majeraha kati ya hao wanne walifanyiwa upasuaji ambao ni Yacouba (Songne), Shomari (Kibwana), Moloko (Jesus) na Ninja (Abdallah Shaibu),” alisema Ammar.

Stori; Wilbert Molandi, Championi Jumatano

SIMBA Yatenga MIL 800 Kuwamaliza GENDERMARIE, Huku YANGA Wamvuta STAA wa STARS | KROSI DONGO

Leave A Reply