The House of Favourite Newspapers

THIS IS TOO MUCH… BUKU YAMTOA ROHO MUME WA MTU!

Benard Kanje (katikati) enzi za uhai wake akiwa na dada zake.

 

THIS is too much! Matukio ya kinyama hasa mauaji yanazidi kushika kasi kwenye jamii ambapo tukio bichi ni la mume wa mtu aliyejulikana kwa jina Benard Kanje, mkazi wa Tegeta jijini Dar ambaye ametolewa roho kinyama, kisa kikielezwa kuwa shilingi elfu moja ‘buku’, Ijumaa Wikienda linaripoti.

 

Kanje anadaiwa kuuawa na kijana mwenziye aliyetajwa kwa jina moja la la Erick ambaye ilisemekana kwamba alimpiga mwenzake kwa mbao kichwani wakati wakiwa kwenye ugomvi wa kubishania hela ambayo ilikuwa ni malipo kwa ajili ya pikipiki aliyoiendesha almaarufu ‘deiwaka’.

 

Tukio hilo lilijiri hivi karibuni maeneo ya Mbezi-Ndumbwi jijini Dar kwenye kijiwe cha bodaboda cha jamaa hao na kusababisha taharuki kwani wengi waliamini kuwa wawili hao wanafanya utani.

 

 

TUJIUNGE NA SHUHUDA

Akilisimulia Ijumaa Wikienda kisanga kizima kilivyojiri, shuhuda wa tukio hilo ambaye ni dereva bodaboda mwenzao aliyeomba hifadhi ya jina kwa sababu binafsi alieleza kuwa, ilikuwa majira ya mchana ambapo Kanje alimuazima Erick pikipiki kisha akampa shilingi 1,000 (buku) ambapo alisema anakwenda Africana-Mbezi kisha angerejea muda huohuo.

 

Shuhuda huyo alisema kuwa, tofauti na makubaliano, Kanje alirejea na pikipiki hiyo majira ya saa 1:00 usiku, jambo ambalo lilimkasirisha mno Erick.

Alisema kuwa, alipofika kijiweni hapo, Erick alimwambia kuwa, inabidi atoe kiasi cha shilingi elfu kumi (10,000), badala ya 1,000, jambo ambalo lilipingwa vikali na Kanje ambapo walianza kuzozana hadi kufikia hatua ya kushikana na kupigana.

“Ulikuwa ugomvi wa muda mrefu sana. Mgogoro mkubwa ulikuwa umesababishwa na buku aliyoitoa Kanje ambayo Erick alikuwa akidai kuwa huko ni kudharauliana.” Alisema shuhuda huyo.

Kijana huyo aliendelea kusimulia kuwa, baada ya muda, Kanje aliondoka kisha akarejea na kiwembe ambapo moja kwa moja alikwenda kwenye pikipiki ya Erick na kuanza kuchana kiti.

Alisema kuwa, jambo hilo lilimtia Erick hasira ambapo alipokuwa akijaribu kwenda kuichukua pikipiki yake, Kanje alianza kumkimbiza na kiwembe ndipo naye alipoamua kuchukua kipande cha mbao na kuanza kumpiga nacho kichwani kabla ya kuanguka chini.

 

Alisema: “Yaani ilikuwa kama utani vile, lakini kilichofuata ni unyama mtupu maana baada ya purukushani ile, Erick alichukua mbao, akaanza kumpiga nayo kichwani na sehemu nyingine za mwili baada ya kuona anataka kuchanjwa na kiwembe.

“Baada ya kumpiga na mbao, Kanje alidondoka na kuanza kugaragara huku damu nyingi zikimtoka.”

Alisema kuwa, baada ya Kanje kuanguka, Erick aliongoza mwenyewe kwenda Kituo cha Polisi cha Kawe kisha kutoa taarifa ambapo baada ya muda, alifika mke wa marehemu na mgonjwa huyo kabla ya kufariki dunia.

MKE NAYE ASIMULIA

Kwa upande wake, mke wa Kanje, Pili Hamisi alisema kuwa, anaumizwa na kifo cha mumewe kwani yeye alifuatwa tu na kuambia kuwa mumewe anakufa na alipofika eneo la tukio, alimkumta mumewe huyo akigaragara huku damu nyingi zikimtoka.

Aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa, alifanya utaratibu wa kutafuta gari na alipofika polisi, alimkuta mtuhumiwa ameshafika hivyo aliwaambia polisi kuwa aliyemdhuru mumewe ndiyo huyo.

“Tulipofika Kawe kuchukua PF-3 (fomu ya matibabu), tulimkuta mtuhumiwa ameshafika hivyo niliwaambia polisi kuwa ndiye huyo aliyemdhuru mume wangu. Mimi nikaondoka hadi Hospitali ya Mwananyamala. Baadaye tulihamishiwa Muhimbili ambapo baada ya kumfanyia operesheni ya kichwa, mume wangu alifariki dunia,” alisema Pili ambaye hakubahatika kuzaa na Kanje.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema alipata taarifa ya majeruhi ya Kanje, lakini hakuwa na taarifa kama alifariki dunia.

“Nilipata taarifa kama majeruhi, lakini sikujua kama amefariki dunia,” alisema Kamanda Miliro na kuahidi kulifuatilia jambo hilo kwa undani.

Stori: Imelda Mtema, Dar

Comments are closed.