The House of Favourite Newspapers

Mukoko Tonombe Auhofia Mziki wa Yanga Kombe la Shirikisho Afrika

0
Kiungo wa TP Mazembe, Mukoko Tonombe.

KIUNGO wa TP Mazembe, Mukoko Tonombe amesema kuwa ubora wa Yanga waliouonyesha katika michuano ya kimataifa kwa msimu huu inaonyesha ni kwa kiasi gani timu hiyo imeimarika huku akiweka wazi kuwa mchezo dhidi yao utakuwa mgumu.

Mukoko kabla ya kujiunga na TP Mazembe alikuwa akikipiga Yanga kabla ya kurejea tena kwa miamba hiyo ya soka Afrika kutokea DR Congo.

Klabu hizo zimepangwa kundi moja katika Kombe la Shirikisho Afrika, pia kuna klabu za US Monastir kutoka Tunisia na Real Bamako ya Mali.

Akizungumza na Championi Jumatano, kiungo huyo alisema kuwa, anaamini utakuwa wakati mgumu kwake kukutana na Yanga katika michuano ya kimataifa mara baada ya kuondoka ndani ya timu hiyo.

“Yanga ni timu nzuri na utaona ni kwa kiasi gani wamefanya vyema kwa kuitoa timu kubwa na ngumu tena ugenini kisha wakafanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya shirikisho, hivyo utaona ni kwa kiasi gani mchezo wetu dhidi yao utakavyokuwa mgumu. Yanga wanatimu nzuri kwa sasa.

“Binafsi nitafurahi kurejea tena Tanzania kucheza na timu yangu ya zamani, wachezaji wengi ndani ya Yanga ni marafiki zangu na tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara.

“Lakini ukiachana na yote hayo bado naona tunakwenda kukutana na timu ngumu na nzuri lazima tujipange ili kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri zaidi,” alisema mchezaji huyo.

Leave A Reply