The House of Favourite Newspapers

MUME AMFANYIA MKEWE, BINTIYE KITU MBAYA

DAR ES SALAAM: WANANDOA kugombana ni jambo la kawaida, lakini inapofikia hatua ya kuharibu samani mbalimbali za familia na kufanya mambo ya kudhalilisha hugeuka aibu kwa jamii nzima.

 

Habari ya mwanamama Zuwena Mtaraziki (63) na bintiye Asha Mkumba, inaweza kutoa tafsiri hiyo kutokana na baba wa familia hiyo ya watoto wawili, aliyetajwa kwa jina la Hamisi Mkumba (65), mkazi wa Mbagala Makuka jijini Dar es Salaam, kuwafanyia kitu mbaya.

 

Akizungumza na Amani, juzi Jumanne, nyumbani kwake Mbagala, jijini Dar es Salaam, Zuwena alisema amekuwa akiishi kwa tabu na mumewe huyo, ambaye amekuwa na kawaida ya kuondoka nyumbani kisha kurudi baada ya muda mrefu. “Kwakweli naishi kwa mateso, mume wangu sijui amepatwa na nini. Ugomvi kidogo, anaondoka nyumbani, anakwenda kwa wanawake zake huko, anakaa kwa miezi, pesa zake zikiisha, anarudi nyumbani,” alisema mama huyo.

 

MAMA ANAENDELEA

“Ni muda tumegombana, hadi imefikia hatua tumegawana vyumba, lakini huwa ana kawaida ya kuondoka na kurudi baada ya miezi kadhaa. Mara ya kwanza, alirudi baada ya kuondoka muda mrefu, akataka tuendelee kukaa chumba kimoja. “Mimi nikamwambia kama anataka, tukapime kwanza, akakubali. Kweli baada ya kupima, tukaendelea. Lakini aliondoka tena, aliporudi safari hii akaniambia eti niondoke nyumbani. Niende wapi sasa miye?” anasema mama huyo.

 

 

AMFUKUZA MWANAYE NYUMBANI

“Mimi na mume wangu tulijaliwa watoto watano, bahati mbaya watatu wakawa bahati mbaya. Tukabaki na wawili, huyu (akamwonyesha mwandishi wetu mwanaye wa kike – yupo ukurasa wa kwanza) wa kike na mwingine wa kiume. “Baada ya kelele za mume wangu, mwanetu wa kiume alishindwa kuvumilia, akaamua kuondoka nyumbani. Kama siyo kelele zake, mtoto asingeondoka,” anasema.

 

AHARIBU SAMANI

Mama huyo anasema, katika kumshinikiza aondoke nyumbani hapo, mumewe huyo alifikia hatua ya kubomoa choo, milango mitano na madirisha na kwenda kuviuza. “Hivi ninavyokuambia hatuna mahali pa kujisaidia. Anafanya visa vya kila aina. Anatuaibisha hapa mtaani huyu mume wangu,” anasimulia kwa huzuni.

 

KESI YAFIKISHWA SERIKALI YA MTAA

Mama huyo anasema, siku ambayo mumewe alibomoa choo, ilibidi aende kwa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Makuka Kusini, ambapo alishtaki, mumewe akapelekewa barua ya wito. “Tulifika kwa mjumbe, akadai anataka kuniacha. Wakamwambia sawa, kama anataka kuniacha, basi tuuze nyumba ili kila mtu apate mgawo, akakataa. Akaambiwa anipe milioni 16, kila mtu aendelee na maisha yake, akasema hana.

 

“Basi akaambiwa aniache niishi. Kwanza ujue kila mtu anaishi kwenye chumba chake, hanipi matumizi yoyote. Najitegemea mwenyewe, labda na wanangu huwa wananisaidia. Simtegemei kwa chochote. Aniache niendelee na maisha yangu,” alisema.

 

AHARIBU BIASHARA

Anaeleza kuwa, nyumbani hapo huwa anafanya biashara ya kuuza maandazi, lakini mume wake amekuwa akiwafanyia fujo wateja wa kiume, hali iliyosababisha wateja wapungue.

 

“Mimi huwa nina biashara yangu ya kuuza maandazi hapa nyumbani, nilikuwa namaliza hadi kilo tisa kwa siku, lakini akaanza kuwatukana na kuwafukuza wateja wa kiume, kwa sasa wamepungua kwa sababu wanamuogopa. Hivi napika kilo mbili tu,” alisema mama huyo na kuongeza: “Kama hiyo haitoshi, amekuwa akijisaidia haja ndogo kwenye kopo, kisha anamwaga mkojo katika sehemu ninayofanyia biashara. Akifanya hivyo harufu huwa mbaya na wateja wanazidi kupungua. Kiukweli huyu baba ananitesa sana.”

 

MJUMBE ANENA

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Makuka Kusini, Ally Shabani Matuga, alikiri kupokea taarifa za tukio hilo na kwamba ofisi yake ililishughulikia kwa ngazi yake. “Tulipopata taarifa niliwaita pande zote mbili, mzee alieleza na mama alieleza na kulalamika kuhusu mienendo ya mumewe, lakini mwanaume alidai kwamba alimpa talaka mkewe ingawa hakumwandikia. Walikubaliana kuachana, lakini wauze nyumba na kugawana.

 

“Sisi tumewaambia, kwa sababu bado mteja hajapatikana, warudi nyumbani waendelee kuishi. Mteja akipatikana, wauze na kugawana, kila mtu aendelee na maisha yake lakini kwa sasa tumesisitiza mama arudi nyumbani kwake na asinyanyaswe, jambo ambalo tunalisimamia,” alisema Matuga.

Stori: Neema Adrian na Amani

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.