The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 10

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Nikiwa bado chumbani ghafla mlango ulisukumwa, akaingia mtu, nikashtuka na kumwangalia. SASA ENDELEA NAYO SASA…

Nadhani nilisikia vibaya, kwani nilipoangalia, mlango ulikuwa vilevile na wala hakukuwa na mtu. Sanasana nikasikia mlango wa nyumba ya pili ukifungwa. Nikaamini mlango niliousikia ni huo na si wa chumbani kwangu. Lakini cha ajabu mwili ulikuwa ukitetemeka na wasiwasi kujaa moyoni mwangu.

Nikahisi nywele zikisisimka. Mapigo ya moyo yakaongeza mbio kwa kupiga kwa kasi ya wasiwasi na hofu. Nikiwa nafikicha macho ili kuona vizuri, nikasikia kama mlango wa kabati ukifunguliwa, kuangalia hivi, upo vilevile. Hakukuwa na mlango wazi.

Nilijikuta nikilitupa begi kitandani na kutoka haraka sebuleni. Nilimkuta Tiaki akiendelea na juisi yake huku macho yakiwa kwenye runinga.
“Vipi shem?” nilimuuliza.

“Nakwenda sawasawa tu. umefurahia zawadi?”
“Sawa shem, nashukuru sana, Mungu akubariki sana,” nilimwambia nikimpa mkono.
“Wala usijali mama Kisu.”

Nilikaa kwenye kochi dogo, lakini nikawa namwangalia kwa woga huku pia nikimtafsiri kwa njia moja au nyingine kuhusu yale yaliyonitokea chumbani.
“Siku hizi kuna joto sana,” alisema Tiaki.
“Sana,” nilimjibu kwa mkato.

“Yaani ningekuwa nyumbani lazima ningeoga hata mara tano,” alisema.
Nikawa najiuliza nini maana ya kauli yake hiyo. Kwamba, anataka kwenda kuoga sasa anaomba kiaina au! Nilimwangalia kwa muda kisha nikafungua kinywa changu.
“Kwa hiyo shem unataka kwenda kuoga au?”

“Ah! Hata nikisema nikaoge nitajifuta na nini sasa? nitabadilije nguo? Acha tu, nitakwenda kuoga nyumbani.”
“Hamna! Taulo hapa lipo shem.

Halafu nguo zako mbona sizioni kama zimechafuka.”
Alinyamaza kimya, mimi nikasimama na kwenda kumwandalia taulo ili akaoge huku moyoni nikisema mume wangu alikuwa hapendi kutumia taulo, yeye alipenda sana kutumia kanga yangu kujifuta baada ya kutoka kuoga.

Lakini moyo wangu ulikuwa unakwenda na kushtukashtuka mara kwa mara. Kuna wakati nashtuka kwamba Tiaki si mtu mzuri, kuna wakati nasema ni mtu wa kawaida tu kama watu wengine.

Nikiwa chumbani nilijiuliza, nimwingize aoge kwenye bafu la chumbani au bafu la jumuiya? Nilipata wakati mgumu sana kwa kweli.
Nilisema liwalo na liwe, kwa mtu aliyejitolea kuleta zawadi kiasi kile halafu nimpeleke bafu la jumuiya niliona kama si kumtendea haki jamani! Niliamua akaogee bafu la chumbani, sasa ningefanyaje!

Nilitoka, nikamwita.
“Shem twende ukajimwagie maji.”
“Ooh! Mama Kisu bwana. Hukukubali, ukaona lazima nioge, sawa,” alisema akisimama.
Mimi nilikuwa mbele yeye nyuma, nikamwingiza chumbani na kumwonesha bafuni ambako kulikuwa na kila kitu katika uhitaji wa kuoga kisha mimi nikatoka kurudi sebuleni. Ile nakaa tu, mawazo yaliyonijia ni kuhusu marehemu mume wangu. Hususan kuhusu kazini kwake.

“Hivi ni kwa nini watu wa kazini kwa mume wangu sikumwona hata mmoja wakati wa msiba? Ina maana hawakusikia? Na kama hawakusikia, mbona hakuna mtu hata mmoja aliyekuja kuuliza? Mpaka nimemaliza arobaini sijamwona mtu. Ajabu!” niliwaza.
Yaani ikawa ajabu zaidi kwani wakati nawaza hayo, simu yangu ikaita, namba siijui, nikapokea.

“Haloo.”
“Haloo, nani mwenzangu?” sauti iliniuliza.
“We unataka kuongea na nani?”

“Sikia, mimi naitwa Simon ni mfanyakazi wa hapa Kampuni ya Power Domestic Material au kwa kifupi PDM. Sasa nilikuwa nauliza, sijamwona bosi muda mrefu sana. Namba yake haipatikani! Hii yako nimeipata kwa sekretari wetu,” ilisema sauti hiyo ya kwenye simu.

Nilikuwa nimekaa kama nimelala lakini ikabidi nikae vizuri ili nimsikie vizuri.
“Unasema?” nilimuuliza. Akaniambia vilevile bila kukosea.

Nilikata simu, nikasema nimsubiri Tiaki ili nimsimulie yote kuhusu yule mtu aliyepiga simu. Machozi yalinilengalenga, nikaanza kuwaza mengine mengi. Kwamba, kuna uhusiano gani kati ya mimi kuwaza kuhusu mume wangu na mfanyakazi wa ile kampuni kunipigia, nilishangaa sana hapo.

Nilihisi Tiaki anachelewa maana nilitaka nimsimulie anipe mawazo, nikasema niende kulekule chumbani kwa vyovyote atakuwa amemaliza kuoga. Niliingia.
Nilishtuka sana kumkuta Tiaki ameacha kutumia taulo kujifuta, anatumia kanga yangu iliyokuwa nyuma ya mlango.

“Haa! Hutumii taulo shem?”
“Sipendi kabisa mama Kisu, sijui kwa nini?”
“Sasa wewe umesema huna mke, kanga unapata wapi huko nyumbani kwako?”
Je, nini kilitokea? Fuatilia wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply