The House of Favourite Newspapers

Museveni, Kenyatta Wamuunga Mkono Rais Magufuli

rais-magufuli

Rais Magufuli akipokea msaada wa fedha taslimu zilizotolewa na Rais Museveni

RAIS John Magufuli amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera na mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Kigoma kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo ya maafa na michango kwa ajili ya waathirika wa maafa hayo, Rais Magufuli aliwashukuru wote waliojitoa kusaidia waathirika akiwataja marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuwa wamempigia simu za kumpa pole na tayari wametoa misaada yao.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema pamoja na kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli alipokea mchango wa fedha taslimu Dola za Kimarekani 200,000 sawa na takribani Sh milioni 437 kutoka kwa Rais Museveni. Pia Rais Magufuli alipokea taarifa ya mchango wa mabati, blangeti na magodoro vyenye thamani ya Sh milioni 115 kutoka kwa Rais Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

yoweri-museveni-007Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.

Pia alizishukuru nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa umma na watu binafsi waliochangia na kusema michango hiyo ina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na athari za maafa haya.

president-uhuru-kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Alitoa wito kwa Watanzania na wote walioguswa na maafa hayo kuendelea kutoa misaada kwa waathirika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, huku akionya na kuvitaka vyombo vya dola kuwafuatilia watu wanaotaka kutumia maafa haya kukusanya michango kwa lengo la kujinufaisha.

Alibainisha kuwa serikali itahakikisha inarekebisha miundombinu iliyoharibika zikiwemo shule, vituo vya matibabu, barabara na huduma nyingine za kijamii na pia ametaka wananchi waliokumbwa na madhara ya tetemeko hususan nyumba zilizobomoka, wajipange kurekebisha nyumba zao kwa kuwa serikali pekee haitaweza kujenga nyumba zote zilizobomoka.

Aidha, Rais Magufuli aliwasihi Watanzania kuwapuuza watu wanaotaka kutumia maafa hayo kueneza uchonganishi na chuki dhidi ya serikali na aliweka wazi kuwa mpaka sasa hakuna teknolojia ya kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi na kwamba tetemeko hili halikuletwa na serikali.

Alisema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi na teknolojia yanakumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya wananchi na uharibifu mkubwa wa mali.

“Nilikuwa najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China kwenye mwaka 2014 watu 617 walipoteza maisha, Mwaka 2013 walipoteza watu 193, Mwaka 2010 walipoteza watu 2,998 Mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712. Ukijaribu kuangalia Japan, nchi ambayo imeendelea na ina utaalamu wa hali ya juu sana, kwenye mwaka 2016 tarehe 14 mwezi wa Aprili ilipoteza watu sita, baada ya siku mbili tetemeko likatokea tena na likaua watu 35.

Mwaka 2012 liliua watu watatu, mwaka 2011 likaua watu 15,904 mwaka 2008 likaua watu 12, mwaka 2007 likaua watu 11, mwaka 2004 likaua watu 40, mwaka 1923 liliua watu 142,800 na hiyo ni Japan,” alisisitiza Rais Magufuli.

Katika taarifa yake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17, majeruhi 440, nyumba 2,063 zimeanguka, nyumba 14,081 zipo katika hali hatarishi na nyumba 9,471 zimepata uharibifu mdogo, huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

Aliongeza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kupeleka chakula, huduma za matibabu na hifadhi za dharura kwa waathirika na pia inaratibu ukusanyaji wa michango kutoka sehemu mbalimbali ambapo mpaka sasa kiasi cha Sh bilioni 3.6 zimepatikana.

 

Comments are closed.