The House of Favourite Newspapers

Muuguzi Aliyempiga Mjamzito Afutwa Kwenye Baraza la Wauguzi na Wakunga

0

 

BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania, limemwondoa kwenye orodha ya wauguzi na wakunga Tanzania, Valentine Kinyanga wa kituo cha afya Mazwi, Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, baada ya kumkuta na hatia ya kumpiga vibao Zulfa Said aliyefika kujifungua kituoni.

 

 

 

Tukio hilo, lilitokea tarehe 5 Januari 2021, saa nne usiku, ilidaiwa Muuguzi, Valentine Kinyanga alimpiga vibao Zulfa Said ambaye alifika kituoni hapo kujifungua.

 

 

Akisoma hukumu hiyo jana Ijumaa tarehe 22 Januari 2021, mbele ya wakili wa Serikali, Fortunatus Mwandu, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Abner Mathube alisema, baraza limemtia hatiani mlalalamikiwa (Valentine) chini ya kifungu 26(a)(c) ya sheria ya uuguzi na ukunga kwa kosa la kwanza na la pili.

 

 

Mathube alisema, baraza lilichambua maelezo ya mlalamikiwa, mlalamikaji pamoja na mashahidi kuhusu kosa la kwanza la kumpiga mgonjwa kinyume na kifungu 25(3)(c)cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania.

 

 

Katika kosa la kwanza, lililotolewa ushahidi, ulithibitisha ni kweli mlalamikiwa alimpiga mlalamikaji na mtuhumiwa alikiri kumpiga mlalamikaji.

 

 

Mathube alisema, kosa la pili, lilikuwa ni kushindwa kusimamia maadili na weledi wa kitaaluma kinyume na kifungu 25(3)(k), lilithibitika kwa mtuhumiwa kushindwa kufuata utaratibu wa utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga kwa mlalamikaji.

 

 

Kushindwa kuchukua na kuhifadhi taarifa za vipimo vya mgonjwa, kushindwa kufuatilia mwenendo wa uchungu wa mgonjwa wakati wa kumpokea katika kituo cha kutolea huduma na kuruhusu mtu ambaye sio mtaaluma kumpima mlalamikaji (mgonjwa).

 

 

“Kwa kuzingatia utetezi wa mlalamikiwa na ushahidi uliotolewa na mlalamikaji na mashahidi, umethibitisha mashitaka yote kama alivyo shtakiwa na mlalamikaji na kwa kuangalia uzito wa makosa yaliyobainishwa dhidi ya mlalamikaji.

 

 

“Ya kwamba, angeweza kusababisha madhara makubwa kwa kumchapa vibao mama ambaye alikua tayari amejifungua pasipo msaada wake, muuguzi huyo alipaswa kumuhudumia kwa weledi na upendo mkubwa,” alisema Mathube.

 

 

Alisema, kutokana na hayo, baraza limempa adhabu ya kumuondoa kwenye orodha (Rolls) ya wauguzi na wakunga Tanzania chini ya kifungu 28(3)(a) cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania ya mwaka 2010 na kutakiwa kurejesha vyeti na leseni kwa muuguzi mkuu wa mkoa wa Rukwa ambaye atawasilisha kwa Baraza.

 

 

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema, haki ya rufaa imeelezwa chini ya kifungu 31(1) cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania ambapo anaweza kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ndani ya miezi mitatu tangu tarehe ya hukumu.

 

 

Mara baada ya hukumu hiyo kutolewa, Rais wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluya, aliwataka wauguzi kufanya kazi kwa weledi licha ya changamoto ya watumishi hasa katika kada ya uuguzi.

 

 

Baluya aliwataka wauguzi wote nchini, kuishi kwa kufuata miongozo ya taaluma yao kwani kukiuka maadili ya taaluma yao inawaondolea sifa na kuonekana muuguzi sio rafiki wa mteja.

 

 

Kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi, Baluya alisema suala hili lipo mamlaka nyingine hivyo wauguzi wanapaswa kulinda hadhi ya taaluma yao kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mahali walipo.

 

 

Leave A Reply