The House of Favourite Newspapers

Mwakifwamba Adaiwa Kutafuna Fedha za Shirikisho

0
Simon Mwakifwamba.

DAR ES SALAAM: Kimenuka! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya vyama saba kati ya kumi vina­vyounda Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’ kumwandikia barua na kumtaka kujiuzulu rais wao, Simon Mwakifwamba kwa madai ya matumizi mabaya ya nafasi yake, ikiwemo kutumbua fedha, vinginevyo watajiondoa.

Chanzo kilicho ndani ya vyama hivyo kimedai kuwa viongozi wa vyama hivyo walikaa kikao hivi karibuni na kumwandikia barua Mwakifwamba kumtaka ajiuzulu nafasi yake.

 

“Yaani mambo siyo mazuri kabisa ndani ya shirikisho, kuna wengine wanataka waende kwa waziri kumweleza jinsi Mwakifwamba anavyojinufaisha binafsi, kwa kuwa amekuwa akiomba fedha sehemu mbalimbali akidai ni kwa ajili ya shirikisho lakini anafanyia mambo yake binafsi.

“Pia gari la Shirikisho analitumia kwa shughuli zake, Tamasha la Arusha lililofanyika mwaka jana alilifanya ni lake wakati ni la shirikisho na mengine mengi,” kilisema chanzo hicho.

 

Risasi Mchanganyiko lilimpata mmoja wa viongozi wa vyama vilivyoandika barua hiyo, ambaye ni wa chama cha waigizaji Tanzania, Elia Mjata ambaye alithibitisha kwamba ni kweli wameandika barua hiyo inayomtaka Mwakifwamba ajiuzulu na asipojiuzulu baada ya wiki mbili vyama hivyo vitajitoa kwenye shirikisho.

“Ni kweli tumemwandikia barua kwa sababu tangu aingie madarakani hajawahi kutusomea taarifa ya mapato na matumizi ya shirikisho, pia tamasha la mwaka jana ambalo lilizinduliwa na Waziri Nape (Nnauye) la International Film Festival alisema ni la kwake wakati ni la shirikisho.

 

“Juzi tulipoitwa na Waziri Mwakyembe alitutaka tuanzishe mfuko kama wasanii wa Bongo Fleva, alikuja na dokumenti za mfuko ambao ameuanzisha na wanachama wake ni watu tofauti kabisa, hakuna msanii wa filamu hata mmoja hivyo tuna wasiwasi naye maana hatujui huo mfuko umeanzishwaje maana siyo shirikishi.

“Wenyeviti waliokaa na kuandika barua na kuzisaini ni wa Chama cha Waigizaji Tanzania, Chama cha Waongozaji, Chama cha Maprodyuza, Chama cha Waandika Miswada, Chama cha Waandishi, Chama cha Wasambazaji, Chama cha Wahariri,” alisema Mjata.

 

Alipotafutwa, Mwakifwamba alifunguka;

“Kwanza wanataka nijiuzulu kwa ushahidi gani, nimekula hela za nani? Wanachotakiwa ni wawe na ushahidi wa hayo wanayosema, kwanza kabisa huyo Elia anatakiwa kusema milioni tano walizochukua benki za chama cha waigizaji wamepeleka wapi.

“Wameona kwamba wameshapelekwa Takukuru kwa ajili ya kuchunguzwa, wameona ngoja wazushe hilo ili kulifunika hili, nitalisimamia hili mpaka ijulikane hizo fedha za chama walikula au walizipeleka wapi na wanatakiwa kuzirudisha.”

GLADNESS MALLYA, RISASI MCHANGANYIKO

VIDEO: Serikali Yaagiza Magazeti Yote Tanzania Kusajiliwa Upya

Leave A Reply