The House of Favourite Newspapers

Mwalimu wa Nursery Matatani Ubakaji!


 

HII NI AIBU! Mwalimu siku zote amekuwa ni kimbilio kwa wazazi ambao huamini ni mlezi wa pili, lakini linapokuja suala la mwalimu huyo kutuhumiwa kwa ubakaji ndipo inaogopesha.

 

Katika tukio hili ambalo halijathibitishwa kuwa lina ukweli, Mwalimu Raphael (45) wa shule moja ya awali (Nursery) iliyopo Mbalizi Wilaya ya Mbeya, mkazi wa Jakaranda ameingia matatani kwa ubakaji wa mwanafunzi wake. Raphael anashitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, kwa ubakaji wa mwanafunzi wake aliyekuwa anasoma chekechea katika shule hiyo.

 

Tukio hilo linadaiwa kutokea mwaka jana kwa nyakati tofauti ambapo mtoto huyo (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka minne alisimulia mkasa mzima. Shauri hilo lipo mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Zawadi Leizer huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Davice Msanga.

 

Upande wa utetezi unawakilishwa na wakili wa kujitegemea, Victor Mkumbe. Msanga alisema kosa hilo ni kinyume cha sheria kifungu cha 130 (1), (2), (e) na 131 (3) sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

 

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kwa nyakati tofauti, mshtakiwa alikuwa akimchukua mtoto huyo kutoka bwenini nyakati za usiku na kumpeleka katika darasa kisha kumbaka. Kesi hiyo iliyosomwa Aprili 9, mwaka huu ilipangwa kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali, lakini iliahirishwa kusomwa kutokana na ombi la mshtakiwa aliyesema kuwa anaomba kesi iahirishwe kwa kuwa wakili wake huyo alikuwa na udhuru.

 

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 25, mwaka huu. Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana.
Gazeti hili linafuatilia kwa karibu kesi na litakuwa linaandika kila kitakachojiri mahakamani.

Comments are closed.