The House of Favourite Newspapers

Messi Aitupa Nje Man U, Ronaldo Out Uefa

BAADA ya kushindwa kufunga bao kwenye Dimba la Old Traff ord wiki moja iliyopita, jana Lionel Messi alifunga mabao mawili na kuitupa nje Manchester United, huku Cristiano Ronaldo na Juventus yake wakitupwa nje na Ajax.

 

Messi alishindwa kufunga bao kwenye mchezo ambao Barcelona walishinda bao 1-0 nchini England, lakini jana akiwa machinjioni Camp Nou, alikuwa shujaa wa timu yake alipofunga mabao mawili na Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Hii ina maana kuwa Barca sasa wametinga nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya na Manchester United ambao walianza mchezo huo kwa kujiamini wakirejea nyumbani kuwania nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya England.

Messi alianza kuonyesha ushujaa wake katika dakika ya 16 baada ya kuwachanja mabeki wa Man United akiwemo Phill Jones ambaye alisema awali kuwa anaweza kumkaba, na kufunga bao safi kwa shuti kali.

Muda mfupi kabla ya bao hilo, mwamuzi aliamuru Barcelona wapige penalti lakini baada ya kwenda kwenye kamera (VAR), kujiridhisha alibadilisha mawazo na kusema siyo penalti. Hata hivyo, dakika ya 20 ya mchezo, kipa wa United David De Gea, alifanya uzembe baada ya kushindwa kuokoa shuti laini lililopigwa na Messi ambaye aliifungia timu yake bao la pili.

Kuanzia hapo, Barcelona walitawala mchezo huo huku wakikosa nafasi kadhaa za wazi ikiwemo shuti la Luis Suarez ambalo liliokolewa na DeGea. Dakika ya 61, Phillipe Coutinho, aliachia mkwaju kutoka nje ya eneo la hatari na kuifungia timu yake bao la tatu huku likionekana kuwa bora kuliko mabao yote yaliyofungwa jana. Hadi dakika ya 80 inafi ka, Barcelona walikuwa wamepiga pasi 686 huku Man United wakiwa wamepiga 381.

JUVENTUS VS AJAX Juventus wakiwa nyumbani kwao, walitangulia kufunga bao safi kupitia kwa Cristiano
Ronaldo katika dakika ya 28 ya mchezo huo. Bao hilo liliwapa matumaini Juventus kuwa wanaweza kufuzu kirahisi kwenda nusu fainali, baada ya kupata sare ya 1-1 nchini Uholanzi wiki moja iliyopita, lakini mambo hayakuwa hivyo kwani dakika ya 34, Donny van de Beek aliifungia Ajax bao safi la kusawazisha.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya bao 1-1, lakini kipindi cha pili Ajax walionekana kuwa bora zaidi na katika dakika ya 67, Mathijs de Light, aliifungia Ajax bao la pili na kuipeleka nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.

 

Sasa Ronaldo ameshindwa kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa huu akiwa na timu tatu tofauti baada ya kutwaa akiwa na Man United na Real Madrid, labda kama atasubri msimu ujao. Hatua ya nusu fainali sasa Barcelona watavaana na mshindi kati ya Liverpool au Porto, huku Ajax wakicheza dhidi ya Manchester City au Tottenham.

Comments are closed.