The House of Favourite Newspapers

Mwanafunzi Amkuna JPM, Achangisha Sh. 24m Papo Hapo – Video

Rais Magufuli, leo ameendesha harambee ndogo katika eneo la Nyamongo ya kuchangia fedha kwa ajili ya kutatua kero katika shule ya Ingwe, Tarime mkoani Mara huku akiwataka wanaume katika eneo hilo kuacha mawazo potofu ya kuwalaghai wanafunzi.

 

Akiongea na wananchi katika eneo hilo la Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara, Rais alimruhusu binti aitwaye Monica Bernad mwanafunzi wa kidato cha tano, katika shule ya Ingwe kueleza kero zilizopo katika shule hiyo.

 

“Shule yetu imeanza mwezi wa saba tarehe 30 kama High School lakini shule yetu ina upungufu wa walimu na vitabu kwa o-level na advanced level, tuna bweni moja ambalo ‘tunashea’ wanafunzi wa o-level na advanced wa kike, katika bweni hilo tuna vitanda vichache ambapo inasababisha kitanda cha futi mbili na nusu tunalala wanafunzi watatu.

 

“Tunakosa vitabu rejea kwa kidato cha tano na cha sita na inatufanya kutumia kitabu kimoja kwa kuchangia na vitabu hivi shuleni havipo. Mheshimiwa Rais tunatoka katika familia maskini tunaomba ututatulie tatizo hili,” amesema Monica.

 

Baada ya kusikiliza kero hizo, Rais Magufuli alisema;

 

”Kwanza Monica nikushukuru sana lakini si ajabu vijana wa kiume wa Nyamongo wameshaanza kumwangalia angalia na pengine kufikiria kumtorosha, washindwe kabisa wasimsogelee Monica ambaye ameongea kwa niaba ya wanafunzi na vijana wengi”, alisema Magufuli.

 

Aidha katika kutatua kero za shule hiyo Rais aliendesha harambee ndogo katika mkutano huo wa hadhara ambapo viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani, Wabunge na Mawaziri walichangia na kuwezesha kupatikana kwa takribani shilingi milioni 24.

 

Mwisho Rais Magufuli yeye alichangia kiasi cha shilingi milioni 5, hivyo kufikisha zaidi ya milioni 29 ambazo amewaagiza Mkuu wa mkoa na RPC kuhakikisha zinakusanywa na kwenda kutumika kama ilivyokusudiwa ili wanafunzi katika shule ya Ingwe wasome bila shida.

Comments are closed.