The House of Favourite Newspapers

Mwanafunzi Auawa Kinyama, Anyofolewa Viungo vys Siri

0

WATU wasiojulikana wamemuua kikatili mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Tutuo, Sikonge mkoani Tabora, Maria Kazungu (13) na kisha kunyofoa viungo vyake vya siri wakati akienda kisimani kuchota maji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi (ACP) Richard Abwao, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kuahidi kukutana na waandishi wa habari ili kulizungumzia suala hilo.

 

Baba mzazi wa mtoto huyo, Ngassa Kazungu, alisema jana kuwa Maria alitumwa Ijumaa na mama yake kwenda kuchota maji kisimani baada ya kutoka shuleni majira ya saa 11:00 jioni.

 

Kazungu aliweka wazi kuwa kwa mara ya kwanza mwanawe huyo alifuata maji na kurejea nyumbani salama lakini aliporudia kwa mara ya pili hakuonekana hadi siku ya pili mwili wake ulipookotwa kwenye kichaka ukiwa umenyofolewa viungo vyake katika sehemu ya siri huku masikio yakiwa yametobolewa na kitu chenye ncha kali.

 

‘’Nimepata pigo ambalo sitalisahau katika maisha yangu kwani mtoto wangu Maria ameuawa kikatili na mimi niliamua kumsomesha mwanangu ili siku za mbeleni aje kunisaidia lakini wameamua kukatisha maisha yake,” alisema Kazungu huku akilia kwa uchungu.

 

Hata hivyo, Kazungu alisema anamwachia Mungu pamoja na Jeshi la Polisi kwa kuwa mauaji kama hayo hayapaswi kufumbiwa macho na vyombo vinavyohusika ni lazima vifanye kazi ili kuwabaini wanaofanya unyama kama huo.

Mwenyekiti wa Serikali Kitongoji cha Ulula, Masele Charles, alikiri kuuawa kwa mwanafunzi huyo na kwamba amesikitishwa na pia hajaridhishwa na mauaji hayo.

 

Mwenyekiti huyo aliweka bayana kuwa hivi sasa anategemea kuanza ulinzi mkali wa jeshi la sungusungu na polisi jamii katika kitongoji chake ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Diwani wa Tutuo, Rashidi Magope, alionya kuwa waliofanya unyama huo pia walimtoboa mara tatu sikio la mkono wa kulia na kuongeza kwamba tukio hilo la kuuawa kwa mwanafunzi huyo ni la pili kwa kuwa hata mwaka jana aliuawa pia mwanafunzi wa shule ya sekondari.

 

Diwani huyo aliongeza kuwa mauaji hayo yanaleta taswira mbaya katika kata yake na kuwataka baadhi ya wananchi wanaojihusisha na vitendo kama hivyo kuacha mara moja. Aliliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wahalifu hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

 

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, John Palingo, alipoulizwa juu ya tukio hilo, licha ya kukiri kuwapo alisema yeye hakuwapo kwenye eneo la tukio kwa kuwa sasa yuko Dar es Salaam kwa matibabu.

Leave A Reply