The House of Favourite Newspapers

MWANDISHI AANIKA SIRI MAUAJI YA ALBINO KWENYE KITABU

0

 Jalada la kitabu cha ‘MIFUPA YA ALBINO’.

 

MWANDISHI wa habari mwandamizi nchini, Daniel Mbega, amekamilisha kuandika kitabu kinachofichua siri zilizo nyuma ya pazia kuhusiana na mauaji ya vikongwe na albino nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

 

Mwandishi huyo, ambaye alifanya utafiti kwa kipindi cha miezi nane mfululizo katika mikoa 10 ya Kanda ya Maziwa Makuu, amesema kitabu hiyo alichokipa jina la ‘MIFUPA YA ALBINO’ kinatarajiwa kuwaingia kiwandani wakati wowote na kwa sasa anatafuta msaada wa fedha za kuchapia.

Mwandishi Daniel Mbega, akiwa ameshikilia Karunguyeye waliokaushwa nyumbani kwa mganga wa jadi.

“Nimekamilisha, lakini nimekwama kidogo kuhusu fedha za uchapaji na kama kuna taasisi yoyote au mtu anayeweza kunisaidia nitashukuru sana,” amesema mwanahabari huyo.“Yeyote mwenye nia njema na jamii ya Watanzania na anaguswa kusaidia uchapaji wa kitabu hiki, ninaomba awasiliane nami kwa namba hii 0656-331974, kwani naamini kitabu hiki kitakuwa msaada pia wa kiroho baada ya kujua mambo yanayofanywa hata na baadhi ya viongozi wa dini wanaotumia ushirikina,” aliongeza.

 

Bw. Mbega amesema kwamba, katika utafiti wake huo alifanikiwa kukutana na waganga wa jadi, wachawi na matapeli katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa, ambako alikaa kwa miezi miwili akifanya uchunguzi.

Mwandishi Daniel Mbega, akiwa kwa mganga huko Kachwamba, wilayani Chato wakati akifanya uchunguzi wa mauaji ya albino.

Aidha, amesema kwamba, katika uchunguzi wake huo alishiriki pia kikamilifu katika misako mbalimbali ya wahalifu walioshiriki kwenye matukio hayo na kushuhudia namna vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotenda kazi.Kunusurika kifo kwa ajali ama kuzingirwa na baadhi ya wananchi ni moja ya hatari alizokumbana nazo wakati wa uchunguzi wake, huku akisafiri umbali wa zaidi ya kilometa 40,000 katika kipindi hicho.

Mtuhumiwa Sajenti Kalinga Malonji akiwa chini ya ulinzi baada ya kukishusha kiganja cha Baraka Cosmas kwenye mti nyumbani kwake kijijini Hanseketwa, Mbozi siku ya Jumapili, Aprili 26, 2015. Sajenti tayari amehukumiwa miaka nane jela na wenzake wamehukumiwa vifungo vya hadi miaka 20 jela.

“Wakati mwingine nilikosa usingizi hata kwa siku tano mfululizo, nililazimika kusafiri mchana na usiku katika mazingira mengi hatarishi nikikusanya habari,” alisema.Akaongeza: “Haikuwa kazi rahisi kuweza kufanya mahojiano na waganga wa jadi, achilia mbali wachawi ambao baadhi yao waliamua kujiweka wazi na kueleza mambo yanayotendeka katika ulimwengu wa giza na jinsi yanavyohusiana na mauaji ya wenye ualbino.”

 

Alisema katika uchunguzi huo alikumbana na mambo mengi ya ajabu ikiwa ni pamoja na kushika matunguli, pembe zinazofoka damu, damu na maiti, mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu na mambo mengine kadha wa kadha.Aidha, alisema kwamba, alizungumza pia na wanamichezo, baadhi ya viongozi wa dini ambao nao wanatumia nguvu za giza ambapo waganga walieleza jinsi nao wanavyoshiriki katika matukio hayo ya mauaji ya wenye ualbino.

 

“Ni mtandao mpana sana, siyo Tanzania tu, bali hata katika nchi jirani za Kenya, Malawi, Burundi, Msumbiji, Afrika Kusini na Swaziland… naamini kkitabu hiki kitaiamsha jamii na kubadilisha mitazamo ya watu mara watakapojifunza yale niliyoyakusanya kutoka kwa vinywa vya wahusika wenyewe,” amesema na kusisitiza kwamba amepanga kitabu hicho kiwwe mtaani mwishoni mwa mwezi Septemba ikiwa atapata msaada wa kufanikisha uchapaji.

 

Leave A Reply