The House of Favourite Newspapers

Mwanzo wa mwisho wangu 06

0

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba au maarufu zaidi kama Ben, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo na kilichokuwa kikisubiriwa ilikuwa ni hukumu tu.

Wakati kila mtu akiamini kwamba Ben ameua, Jordan Rwechungura, wakili aliyekuwa akimtetea katika kesi hiyo ambaye ukiachilia mbali kazi yake pia alikuwa rafiki mkubwa wa Ben, waliyecheza pamoja tangu wakiwa watoto wadogo, anakuwa mgumu kuamini kwamba ni kweli rafiki yake huyo ameua.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anaingizwa mahakamani huku mamia ya watu, wakiwemo waandishi wengi wa habari wakifuatilia kwa umakini kesi hiyo iliyogusa hisia za watu wengi.

Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma. Licha ya maisha ya kifukara anayopitia, anaonesha uwezo mkubwa darasani unaomshangaza kila mmoja.
Je, nini kitafuatia? Ben atapewa hukumu gani? SONGA NAYO…

Miezi mitatu baadaye, Ben na wanafunzi wenzake wa kidato cha nne, walifanya mtihani wa mwisho wa kuhitimu kidato cha nne ambapo kila mmoja alikuwa na matumaini makubwa kwamba kwa mara nyingine, Ben atafanya maajabu.
Baada ya kufanya mitihani, Ben alirudi nyumbani ambapo safari hii alijiingiza rasmi kwenye shughuli ya kubeba mizigo. Akawa anashinda kutwa nzima akifanya vibarua vya kubeba mizigo mpaka jioni.
Japokuwa alikuwa anapata fedha za kuifanya familia yake ipate mahitaji muhimu, ikiwa ni pamoja na mama yake kupata dawa, kijana huyo mdogo alikuwa akichoka sana kutokana na ugumu wa kazi.
Siku zilizidi kusonga mbele na hatimaye matokeo ya kidato cha nne yakatoka, katika kile kilichotegemewa na wengi, hasa waalimu na wanafunzi wa shule aliyotokea, jina la Benjamin Semzaba lilikuwa miongoni mwa majina kumi ya wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha juu zaidi nchi nzima.

“Ben again! Ooh my God! He made it, I saw it coming!” (Ben tena! Ooh Mungu wangu! Amefanya vizuri, nilishaona dalili kuanzia mwanzo) mkuu wa shule aliyokuwa anasoma, Tung’ombe aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupata matokeo hayo, alisema huku machozi ya furaha yakimtoka wakati akifuatilia matokeo hayo mtandaoni.
Tangu aanze kazi ya kufundisha miaka mingi iliyopita, haikuwahi kutokea shule yake ikatoa japo mwanafunzi bora kwa ngazi ya mkoa lakini safari hii, Ben alikuwa ameingia mpaka kwenye kumi bora za nchi nzima, jambo lililomfanya mwalimu huyo ajihisi anapaa angani kwa furaha.

Harakaharaka aliwapigia simu walimu wenzake ambao nao waliwatangazia wanafunzi, furaha ikatanda kila mahali huku taarifa hizo zikiendelea kusambaa kwa kasi kubwa kwenye mji mzima wa Tunduma na Mkoa wa Mbeya.
Ben akiwa hana hili wale lile, akiendelea kubeba viroba vya unga, ndoo za mafuta na katoni za sukari, alishangaa kusikia wanafunzi watatu aliokuwa anasoma nao, wakimuita jina lake huku kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.

Awali alitaka kuwakwepa kwani hakuwa anapenda watu wanaomjua wamkute akiwa kazini lakini kwa sababu walishamsogelea sana, alishindwa kufanya chochote, ikabidi atue mzigo aliokuwa ameubeba na kuwasikiliza.
“Hongera sana mwana! Daah! We mkali kichizi yani!” Isyaka Mwaibale, rafiki mkubwa wa Ben waliyemaliza wote kidato cha nne, alimwambia Ben, mwenyewe akawa anashangaashangaa kwani hakujua anapewa hongera za nini.

“Matokeo yametoka, umepasua divisheni wani ya pointi saba, kubwa zaidi umo kwenye top ten ya wanafunzi bora wa nchi nzima,” alisema Isyaka, kauli iliyomfanya Ben ajihisi kama yupo kwenye ndoto.
Hakutaka kuamini alichokuwa anakisikia, alijua atafaulu lakini siyo kwa kiwango kikubwa kama alivyokuwa anaambiwa, akainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake, rafiki zake wakamkumbatia kwa furaha bila kujali alivyokuwa amechafuka.

Muda mfupi baadaye, wakiwa bado wanapongezana, mkuu wa shule alipaki pikipiki yake jirani kabisa na pale alipokutana na Ben miezi kadhaa iliyopita, akawa anaangaza macho huku na kule kwani aliamini lazima atamuona.
“Ben! Ben! Ben!” aliita mwalimu Tung’ombe mfululizo huku akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake, Ben na wenzake wakageuka na kushtuka kugundua kuwa alikuwa ni mwalimu wao.
“Come here son! You have made it to the top, come!” (Njoo hapa mwanangu! Umefanya kwa kiwango cha juu kabisa, njoo!) alisema mwalimu Tung’ombe kwa furaha huku akitanua mikono yake kama ishara ya kutaka kumkumbatia Ben. Hakujali jinsi alivyokuwa amechafuka, wakakumbatiana kwa nguvu huku watu wengi wakiwashangaa.
Kutokana na jinsi alivyoitangaza vyema shule yake, uongozi wa Shule ya Sekondari Tunduma uliamua kumuandalia sherehe ndogo ya kumpongeza. Ben na mama yake wakaalikwa kwenye sherehe hiyo ambapo muda wote mama yake Ben alikuwa akitokwa na machozi.

Wanafunzi na walimu wakala, wakanywa na kucheza muziki pamoja na Ben na mama yake, ilikuwa siku ya furaha sana kwa kijana huyo mdogo na mama yake pamoja na uongozi mzima wa shule hiyo. Ben akawa ameingia kwenye historia ya kipekee. Kwa kuwa kila mmoja alikuwa anajua ugumu wa hali ya kimaisha waliyokuwa nayo, ilipitishwa harambee ambapo wanafunzi na walimu walijitolea kila walichokuwa nacho.
Fedha nyingi zikapatikana kwa ajili ya maandalizi ya kwenda kujiunga na kidato cha tano na matumizi mengine ya nyumbani huku mwalimu Tung’ombe akiahidi kumgharamia kila kitu mpaka atakapohitimu kidato cha sita. Miezi miwili baadaye, majina ya wanafunzi na shule walizochaguliwa kujiunga na kidato cha tano yalitoka, Ben akachaguliwa kwenda kujiunga na Shule ya Sekondari ya Vipaji Maalum ya Mzumbe.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply