The House of Favourite Newspapers

MAZIKO YA VAILETH — DADA WA SHIGONGO — YALIVYOKUWA BUPANDWAMHELA

Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Global Group, Eric Shigongo akiongea jambo kijijini Bupandwamhela.

MWILI wa marehemu Vaileth James Bukumbi, dada wa Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Global Group, Eric Shigongo, hatimaye umelazwa katika nyumba yake ya milele leo Ijumaa, Juni 21, 2019, nyumbani kwao katika Kijiji cha Bupandwamhela, Buchosa – Sengerema mkoani Mwanza.

 

Akitoa neno la shukurani, Shigongo amewashukuru watu wote waliohudhuria tukio hilo na kushirikiana nao mbali na kwamba waliacha shughuli zao.

 

“Nimesimama hapa kando ya jeneza la dada yangu Vaileth, nilikuwa nakupenda sana dada yangu na nitaendelea kukupenda, nakumbuka wakati unachumbiwa ulichumbiwa na wanaume watatu lakini mimi nilikushauri uolewe na James ambaye alikuwa maskini kwani mlitafuta naye mali mkapata.  Ulikuwa mpambanaji sana, na kupoteza mtu kama wewe ni hasara kubwa sana,” alisema kwa simanzi kubwa .

Aligusia pia kwamba kulikuwa na baadhi ya matatizo mengine ambayo marehemu alikuwa hayafikishi kwake (Shigongo) bali alikuwa anayamaliza yeye mwenyewe.

Alisema matukio ya kifo hupita kama saa  ambapo wanadamu wanaamini ni mipango ya Mungu ambaye pia humwomba msaada siku zote.

Alitoa wito pia kwa matajiri kuwakumbuka watu wa hali ya chini kwani kufanya hivyo ni kuweka hazina kwa Mungu.

 

“Vaileth ameungana na baba yangu, mama yangu, kaka yangu Julius, na dada yangu Jesca ambapo wametengeneza familia nyingine huko mbinguni.  Tunaamini ipo siku tutakutana nao na kuungana nao tena,” amesema Shigongo akiwa mwenye sura na sauti ya masikitiko.

Comments are closed.