TUMEWAHI kusikia kwamba hata wale wanaojiita wazee wa klabu huwa wana maslahi yao, pale yanapoguswa tu, basi kunakuwa na tatizo kubwa sana.
Mara nyingi, wazee wamekuwa wakijificha katika mwamvuli wa “tumetoka mbali na klabu” au ule mwamvuli wa “tuna uchungu na klabu”.
Lakini kunaweza kukawa na ukweli zaidi ya huo kwa kuwa wale wanaopiga kelele sana nao wanakuwa wanafaidika sana pale kunapokuwa na mambo yanayowahusu wazee.
Mfano wazee wanasikilizwa kwa sababu ya kuheshimiwa, na wakati mwingine wanaweza kuzungumza jambo likaonekana halina maana lakini kivuli cha uzee kikaendelea kuwalinda.
Wapo wazee wa klabu, wanaonyesha ni wazee hasa na wamekuwa hawaingilii mambo ya klabu kama Yanga na Simba na wakati mwingine wametoa ushauri wao chinichini bila ya kujulikana na ukawa ushauri ambao ni msaada mkubwa.
Wakati fulani kulikuwa na maneno, kwamba mzee Ibrahim Akilimali, aliamua kupishana na uongozi wa Yanga kwa kuwa mwenyekiti wa klabu, Yusuf Manji alionyesha msimamo wa juu kabisa.
Msimamo wa Manji ilikuwa ni kusisitiza, baraza la wazee halitambuliki kikatiba, hivyo kutaka wazee hao kubaki kama washauri lakini si chombo chenye nguvu ya kugombana au kupingana na uongozi.
Lakini kukawa na taarifa kwamba wazee huwa kwenye kamati ya ufundi, kamati ambayo huchota fedha kila mechi na baada ya kukatwa kwa fedha hizo, ndiyo tafrani likaanza kati ya wazee na uongozi. Hata hivyo, mzee Akilimali ambaye ni katibu wa baraza hilo la wazee, aliwahi kufafanua na kusema habari hizo hazikuwa na ukweli.
Yote yanawezekana, ukweli au uongo. Lakini wote mnakumbuka mzee Akilimali alivyokuwa akieleza kwamba Yanga ina fedha za kutosha kuisaidia k l a b u hiyo h a t a baada ya kuondoka kwa Manji.
Mzee Akilimali mara kwa mara alisisitiza suala la kuondoka kwa Manji, akisema kuna wawekezaji waliokuwa wanahitaji kuingia Yanga na kuwekeza. Tena akasema kulikuwa na fedha nyingi, takriban milioni 600 kwa ajili ya maendeleo ya Yanga, ingawa hakusema zinatokea wapi.
Yanga sasa iko katika wakati mgumu, inakosa uongozi wa mtu kama Manji aliyekuwa imara kwa maana ya uongozi, alikuwa na mipango thabiti kwa kuwa ni mfanyabiashara mkubwa na alijua nini cha kufanya.
L a k i n i Manji aliweza kuisaidia Yanga kwa kutoa kwa upendo au kukopa kwa kuwa ana uwezo. Yanga haikuwa na shida zinazotokea leo na maisha yalikuwa mazuri.
Yanga ilikuwa ni ya kimataifa, inayoweka kambi Uturuki na kadhalika. Iliyopanda ndege kila siku, sasa tangu kuondoka kwa Manji ambaye alionekana hafai na akina mzee Akilimali wakaonyesha hafai, Yanga imevuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho, imevuliwa ubingwa wa Tanzania Bara.
Bahati nzuri imepata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho hatua ya makundi, lakini wachezaji wamekuwa wakigoma, inasafiri kwa kuunga na hakika maisha ni magumu sote tunaona.
Swali linaanzia hapo, ukimya wa mzee Akilimali kuhusiana na mipango uko wapi? Kipindi kile alikuwa akisema na kueleza mambo lukuki, sasa yako wapi?
Yanga inateseka, nazikumbushia zile Sh milioni 600, sasa ndiyo wakati mzuri na zinahitajika. Wawekezaji aliosema wapo, huu ndiyo muda sahihi mzee Akilimali awalete.
Nimekuwa nikisisitiza, kwamba hizi klabu zinaumizwa na wale wenye matamanio na matakwa binafsi. Wale wanaojiona wamiliki lakini msaada wao ni maneno pekee.
Wakati mgumu kwa Yanga, hautadumu milele, iko siku atatokea mkombozi na si lazima awe Manji kwa kuwa Yanga haiwezi kuishi na Manji milele. Lakini vizuri wahusika na wenye nafasi za kuzungumza au kusema jambo kuhusiana na klabu muangalie maslahi zaidi yanayoihusu klabu na si yenu binafsi.
Kwenye shida mnakimbia, kukiwa na neema kila siku maneno na mnaungana kutaka kuwaonyesha watu wabaya mkisema wanafaidika na klabu na mkitaka kuionyesha jamii, klabu inanyonywa.
Sasa klabu hainyonywi? Angalia maisha haya ya shida, kipi bora? Mtu ajifaidishe na klabu ifaidike au kuwe hakuna anayejifaidisha na klabu inateseka, inaaibika na kuumiza mioyo ya mamilioni wanaoipenda.
Mzee Akilimali tunakukumbuka, hatujakusahau na tunazikumbuka na kuzikumbusha Sh milioni 600 zako. Sema mipango ya ukombozi ni ipi, usikae kimya Yanga inateseka!
WAKATI fulani kulikuwa na maneno, kwamba mzee Ibrahim Akilimali, aliamua kupishana na uongozi wa Yanga kwa kuwa mwenyekiti wa klabu, Yusuf Manji alionyesha msimamo wa juu
STORI: SALE HALLY
Comments are closed.