The House of Favourite Newspapers

Mzee Akilimali: Simba walienda kutalii Misri

Ibrahim Mussa na Said Ally KATIBU wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali, amesema kuwa hakushtushwa na kipigo cha Simba walichokipata nchini Misri, kwa kuwa hawakwenda nchini humo kwa ajili ya soka, zaidi ya kufanya utalii.

 

Simba juzi imepokea kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Kwenye Uwanja wa Borg El Arab nchini Misri. Hii ni mechi ya pili mfululizo kwa Simba kupoteza kwa kipigo kikubwa cha mabao, baada ya mechi ya kwanza ya ugenini kufungwa na AS Vita 5-0 nchini DR Congo kabla ya kipigo cha juzi.

 

Mzee Akilimali ameliambia Championi Jumatatu kuwa alijua lazima Simba itapoteza kwa kuwa wenyewe wamekuwa wakisema wana kikosi kipana lakini kimeshindwa kuwa msaada wa kupata matokeo.

 

“Nilisema wasipokuwa makini yatajirudia ya kule DR Congo halafu wao wanasema si wana kikosi kipana, mbona kimeshindwa kuwasaidia kupata matokeo, zaidi ya kukimbiakimbia tu uwanjani na mwisho wa siku wamepata aibu.

 

“Naona kule walienda kufanya utalii, siyo kucheza mpira, haiwezekani wafungwe mabao mengi kiasi kile wakati wao kikosi chao ni kipana, niliwaambia siku moja kuwa wasimtukane mamba kabla ya kuvuka mto, sasa wenyewe mmeona kilichotokea,” alisema Mzee Akilimali.

Comments are closed.