The House of Favourite Newspapers

Mzee Kingunge Apokea kwa Masikitiko Taarifa za Kifo cha Mkewe

Mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwiru leo Jumamosi amepewa taarifa za kifo cha mke wake Pares Mwiru ambazo imeelezwa kuwa amezipokea kwa mshtuko mkubwa.
Kingunge aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wodi ya Mwaisela akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na mbwa nyumbani kwake Kijitonyama, alifanyiwa upasuaji Januari 4 mwaka huu.
Leo Januari 6, mtoto wa mwanasiasa huyo Kinje Mwiru amesema wamempa taarifa baba yao saa tano asubuhi leo.
 
“Tumemfahamisha leo saa tano, ilikuwa ni vigumu sana wakati tunamfikishia taarifa hizo na amezipokea kwa ugumu sana. Haikuwa rahisi kwa yeye kupokea taarifa wakati tunamweleza,” amesema.
Kinje amesema kwa sasa wamemuacha apumzike ili aweze kuwapatia mwongozo nini kifanyike baada ya kifo cha mke wake.
Pares alifariki Januari 4 saa nane mchana katika wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa, tangu alipofikishwa Muhimbili Oktoba 3, mwaka jana.
Ofisa Uhusiano wa MNH John Stephen amesema kwa sasa afya yake imeimarika.
 “Anaendelea vizuri na afya yake imetengamaa, bado yupo chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari, baada ya upasuaji aliofanyiwa,” amesema.

Comments are closed.