The House of Favourite Newspapers

MZEE MAJUTO AACHA WOSIA MZITO!

WAKATI akiwa safarini kwenye matibabu nchini India, mkongwe wa vichekesho nchini kwa zaidi ya miaka 30, Athuman Amri ‘Mzee Majuto’, ameacha wosia mzito kwa Watanzania, hususan wasanii wenzake.

 

Mbali na wosia huo kwa wasanii wenzake, pia Mzee Majuto aliwashukuru watu wa kada mbalimbali waliojitokeza kufanikisha safari yake ya kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi.

 

STEVE NYERERE

Majuto alieleza hayo wikiendi iliyopita alipokuwa akizungumza na mwingizaji mwenzake wa vichekesho Bongo, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ muda mfupi kabla hajaondoka nchini. Steve ndiye alikuwa mtu wa karibu na Mzee Majuto wakati anapata matibabu yake hapa nchini na ametajwa na familia ya msanii huyo mkongwe kuwa mmoja wa watu waliofanikisha safari yake ya kwenda nchini India.

 

WOSIA

Steve aligusia wosia huo wa Mzee Majuto alipokuwa akizungumza na Ijumaa Wikienda kuhusu harakati za kufanikisha safari hiyo mwisho mwa wiki iliyopita.

Mahojiano ya Steve na Ijumaa Wikienda yalikuwa kama ifuatavyo;

Ijumaa Wikienda: Habari yako Steve, familia ya Mzee Majuto imekutaja kuwa mmoja wa watu inaowapa thamani sana kwa sababu ya kufanikisha safari ya baba yao kwenda nchini India kwa matatibu.

Nasi tunaungana na familia hiyo kukushukuru. Lakini kwani ilikuwaje Mzee Majuto akuchague wewe usimamie suala linalohusu familia yake?

Steve: Kwa kweli imetokea tu. Mzee Majuto alipokuwa anaumwa, alimwambia kijana wake, Hamza anitafute ili nimsaidie. Nikakubali na kufika kwake kuzungumza naye.

 

Ijumaa Wikienda: Pamoja na yote, tumesikia Mzee Majuto ameacha wosia kabla ya kuondoka nchini, hili likoje na unaweza kutuammbia unasemaje?

Steve: Aliponiita aliniambia kuwa ananipa mimi wosia huo kwani anaona sauti yangu inaweza kusikika kwa wasanii wengi. Hivyo akanitaka nipaze sauti ya kuwaunganisha wasanii wote katika masuala mbalimbali.

Mzee Majuto alisema anaiona tasnia ya filamu imeanza kupoteza mvuto. Lakini tatizo siyo tasnia, bali wasanii wenyewe ambao siku hizi wamekosa ubunifu.

Ijumaa Wikienda: Sasa amesema wewe uwaunganisheje?

Steve: Kuwa na mijadala ya pamoja na namna ya kuboresha sanaa ya filamu na kuwafanya wasanii waone kuwa wao ni ndugu. Waweze kusaidiana wanapopata matatizo badala ya kusubiri msaada kutoka kwa watu wengine.

Ijumaa Wikienda: Kwani tangu asafiri umeshawasiliana naye akiwa India?

Steve: Ndiyo, amefika salama na ameanza matatibu. Tuzidi kumwombea tu apone na arudi ili aendelee na majukumu yake.

 

FAMILIA SASA

Kwa upande wake, familia ya Mzee Majuto, mbali na Steve Nyerere ilieleza kwamba kama siyo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe mzee wao huyo angefia Bongo.

Katika mazungumzo na Ijumaa Wikienda, Ashraf ambaye alijitambulisha kwamba ni mtoto wa Mzee Majuto alisema kuwa, wao kama familia wanaishukuru Serikali kupitia waziri wake huyo, Mwakyembe kwani kama siyo yeye mzee wao angeendelea kuteseka na kujikuta akiishia kufa hapa nchini.

Alisema kuwa, Waziri Mwakyembe alikuwa bega kwa bega na familia yao huku akiwapa ushauri mara kwa mara hadi alipofanikisha safari ya mzee wao huyo ambaye alisafiri na watu watatu akiwemo mke wake alikuwa akichekelea safari hiyo ndani ya ndege, mwanaye na daktari mmoja.

“Mbali na wengine, lakini shukrani za kipekee ziende kwa Dk Mwakyembe kwa kufanikisha safari ya matibabu ya Majuto kwani alikuwa bega kwa bega na sisi na kama siyo yeye, mzee wetu angeendelea kuteseka pia tunaishukuru Serikali kwa jumla,” alisema Ashraf.

 

Hata hivyo, Ashraf alipinga vikali habari zilizoenea kwamba wasanii wa filamu ndiyo waliofanikisha safari ya matibabu ya Mzee Majuto na kusema kwamba siyo kweli, bali ni Serikali kupitia kwa Waziri Mwakyembe.

Kwa upande wake, Rehema ambaye ni dada wa Mzee Majuto aliliambia gazeti hili kuwa, kwanza anamshukuru Mwakyembe na Serikali kwa jumla, wadau na wasanii mbalimbali wa filamu ambao walikuwa bega kwa bega na familia kwa kipindi chote ambacho Mzee Majuto alikuwa amelazwa mpaka kusafirishwa kwake kwenda India.

Naye Afisa Habari, Uenezi, Mahusiano na Umma wa Chama cha Waigizaji Kinondoni, Massoud Kaftany alisisitiza kwamba, safari ya Mzee Majuto imegharamiwa na Serikali kwa kila kitu na siyo wasanii kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.

Mei 4, mwaka huu Mzee Majuto alisafirishwa kwenda nchini India kwa matibabu zaidi baada ya kusumbuliwa na Ugonjwa wa Tezi Dume na nyonga kwa muda mrefu huku akilazwa mara kwa mara katika Hospitali ya Tumaini, Dar.

 

Stori: Mwandishi Wetu, Dar

Comments are closed.