The House of Favourite Newspapers

MZEE YUSUF AANGUA KILIO HADHARANI – (PICHA NA VIDEO)

HUKU ni kujawa na imani iliyo thabiti! Hivi ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kiongozi wa zamani wa Kundi la Jahazi Modern Taarab aliyemrudia Mungu, Alhaj Mzee Yusuf kujikuta akiangua kilio mbele ya viongozi mbalimbali na waumini wa Kiislam kisa kikiwa ni maneno yaliyotolewa na ustaadhi mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Omary.

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita huko Mbagala Chalambe maeneo ya Chasimba jijini Dar ambako kulikuwa na hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Msikiti wa Madinah ambapo mbali na waalikwa wengine, Mzee Yusuf alikuwepo.

KISA KILIPOANZIA…

Awali, baada ya watu mbalimbali kuzungumza katika hafla hiyo, ulifika wakati wa Ustaadhi Omary ambaye alikuwa mshereheshaji (MC) kumkaribisha Mzee Yusuf naye atoe neno lakini ukaribishwaji wake ulijaa mbwembwe nyingi ikiwemo MC huyo kumsifia sana Mzee kwa kusema ni kipenzi cha wanawake wengi.

“Taaakbiiir…rrrhaaa… Haya sasa kina mama umefikia wakati wa kipenzi chenu Mzee Yusuf Mfalme kuzungumza machache, kaeni sawa kwa kumsikiliza.”

MZEE APEWA MAIKI, AANGUA KILIO

Baada ya MC huyo kumpamba sana Mzee Yusuf huku akionesha kuwa ni staa, anajulikana sana na anapendwa sana na wanawake, Alhaj huyo alipokamata ‘maiki’ baada ya kutoa salamu alianza kupingana na kile ambacho alikieleza ustaadhi huyo huku akilia kuonesha kuwa, alikereka na sifa za kidunia alizopewa.

 

“Waheshimiwa, mimi ni mtu mdogo sana, lakini kwa sababu shetani alifanya kazi kubwa sana mpaka leo nimekuwa mtu ambaye bado shetani anatumika kufanya kazi mbaya na mimi napigana kuondoka kwa shetani kuingia kwa Allah. Naogopa mapenzi haya yasije yakanipeleka pasipo, yakanitoa katika njia.

“Sikuja hapa mnione sura yangu, Allah Aqbar (Mungu Mkubwa), nimeogopa mpaka siwezi hata kuzungumza, si mapenzi ya Allah haya, si kweli…lakini niombeeni dua, haya mapenzi siyo kabisa (anaangua kilio kisha anajifuta machozi kwa mkono wake wa kushoto).

 

“Halafu unalosema usilichukulie kwa wepesi hivyo, sikuwa nikifanya kazi nzuri ya kumfurahisha Mungu, si kwamba walikuwa wakinipenda kwa sababu ya uzuri wangu, ni shetani tu. Sasa nawaombeni sana, msiwe na mapenzi yale ya zamani kwangu (walivyokuwa wakimpenda mashabiki wa taarab hasa wanawake), badilikeni (analia tena, kisha anajifuta machozi).

 

“Sijui ni wangapi wamekuja hapa kuniangalia sura yangu (kama ambavyo wengi walikuwa wanakwenda kwenye kumbi za starehe kumuona akiimba enzi zile), mtanisamehe mashehe, sikujia hilo, nimekuja hapa kwa Laaillaha illallah, Muhammad Rasulullah. “Sikuja kuonesha sura yangu na ndiyo maana nimekuwa nikiogopa sana na naogopa kila mahali. Lakini nawaombeni na ninyi mbadilike, mimi niwe sababu ya kuwabadili wengine,” alisema Mzee Yusuf huku machozi yakimtiririka.

 

AENDA KUKAA AKILIA

Hata baada ya Mzee Yusuf kurudisha kipaza sauti na kwenda kukaa, bado aliendelea kulia, mazingira yaliyoonesha kuwa, kilichosemwa juu yake kilimchoma na kwa kuwa ana mapenzi na Mungu wake, alijikuta kwenye simanzi hiyo.

 

USTAADHI  AMUOMBA RADHI

Baada ya hali ya hewa kuchafuka, Ustaadhi Omary alitumia busara alizojaaliwa na Mungu na kumuomba radhi Alhaj Mzee ambaye muda mwingi alionekana amejiinamia.

 

WAALIKWA KWENYE HAFLA HIYO

Mbali na viongozi mbalimbali wa Dini ya Kiislam, mgeni rasmi alikuwa Shehe Twalib Bin Hamad na mgeni mwalikwa alikuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Fortunatus Muslim.

 

Kamanda Muslim, Shehe Twalib na imamu wa msikiti huo, Omary Masenga waliwaongoza waumini na viongozi wengine katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti huo na baadaye Kamanda Muslim alitumia nafasi hiyo kutoa neno la amani. Aliwataka viongozi wa dini kutoa mahubiri ya kudumisha amani na utulivu pamoja na kufuata sheria za nchi ikiwemo sheria za usalama barabarani na kuwaelimisha waumini juu ya sheria za usalama barabarani ili kuepusha vifo na ulemavu.

STORI: Richard Bukos, Risasi Mchanganyiko

 

WALTER CHILAMBO – ONLY YOU (Official Video)

Comments are closed.