‘Mzimu’ wa Ajali ya Lucky Vincent Bado Unatesa

ZAIDI ya ajali tatu mbaya zimeripotiwa kutokea tena katika barabara ileile ilipotokea ajali ya wanafunzi ya Shule ya Msingi, Lucky Vincent huku ajali hizo zote zikisababisha vifo vya watu na kuacha majeruhi.

 

Taarifa kutoka wilayani Karatu zinaeleza kuwa tangu kutokea kwa ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent Mei 6, 2017, watu wanaokadiriwa wanane wameshapoteza maisha katika ajali zilizotokea katika barabara hiyo inayoanzia Mjini Arusha na kupita Makuyuni mpaka Karatu na hifadhi ya Ngorongoro.

 

Ajali hizi hazijaripotiwa sana tofauti na ajali ya basi la wanafunzi wa shule ya Msingi Lucky Vincent ya mjini Arusha iliyosababisha vifo vya watu 35, wanafunzi 32, walimu wawili na dereva, katika kijiji cha Rhotia baada ya basi lililobeba wanafunzi hao kuacha njia na kutumbukia korongoni katika barabara inayosifika kwa milima mirefu na kona kali.

 

Emmanuel Aloyce, mkazi wa kijiji cha Rhotia ambaye amekuwa akiitumia barabara hiyo mara kwa mara anasema mpaka sasa mambo si shwari katika barabra hiyo, huku akigusia namna alivyoshuhudia ajali ya gari aina ya Fuso lililobeba ng’ombe, Machi mwaka huu,  ambapo watu wanne walipoteza maisha baada ya dereva kushindwa kulimudu gari katika milima na kona kali.

 

Inawezekana ng’ombe walizidi uzito, lakini kumbuka dereva alitoka nao mbali lakini gari likaja kupindukia Kilimatembo kwa sababu ya milima, miteremko mikali na kona,” anadokeza.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karatu, Jubilate Mnyenye,  anabainisha kuwa barabara husika ni changamoto na uongozi wa halmashauri hiyo ulishatoa mapendekezo ya kuiboresha.

 

Kuna sehemu ni hatari sana, ni mteremko mkali na kuna kona inayokunja zaidi ya nyuzi 60. Anayeteremka hamuoni anayepanda na anayepanda hamuoni anayeteremka kwa hiyo ikiwa gari itafeli kutoka juu hakuna namna ya kulikwepa kwa sababu barabara ni nyembamba. Na hili limeshatokea kwa magari kama matatu mpaka manne hivi yaliyoanguka,” anasema Jubilate.

 

Dereva au mwananchi yeyote ukimuuliza kuhusu eneo la Kilimatembo atakuambia. Mwanzoni mwa mwaka huu kuna gari lilibeba ng’ombe na likashindwa kupanda mlima likarudi nyuma na kupinduka, wakafa watu wanne, bahati nzuri nyuma halikua likifuatiwa na gari lingine, lakini madhara yangeweza kuwa makubwa zaidi,” anaeleza.

 

Itakumbukwa kuwa mkakati wa Umoja wa Mataifa kupunguza ajali za barabarani kwa kipindi cha muongo mmoja kutoka 2011 mpaka 2020, ambao Tanzania imeridhia, umetaja uboreshaji wa miundombinu kama nguzo ya pili kati ya tano za kupunguza ajali. Mpango huo pia unataja usalama na vyombo vya moto kama nguzo ya tatu ya kufikia malengo ya kupunguza ajali.

 

Mpango huu unaenda sambamba na malengo ya maendeleo endelevu ya dunia, ambapo lengo Na. 3.6 linaeleza kuhusu kupunguza nusu ya ajali za bararani ili kuokoa vifo vya mamilioni ya watu duniani wanaofariki kwa ajali kila mwaka. Umoja wa Mataifa unasisitiza uboreshaji wa miundombinu ya barabara kuzingatiwa ili kufikia malengo haya.

 

Mneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha Mhandisi John Kalupale anasema wapo tayari kupokea mawazo ya kuiboresha barabara hiyo ili kupunguza ajali za barabarani na kuokoa maisha ya watu, lakini akatilia shaka uwezekano wa kutekelezwa kwa mapendekezo ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karatu.

Kama sehemu ina milima na makorongo utafanya diversion sehemu gani? Kwasababu kila utakapoenda katika maeneo hayo patakuwa na miteremko mikali na milima. Nadhani tunachoweza kufanya ni upanuzi, kama tukipata fedha yale maeneo ambayo yana nafasi ya upanuzi ndiyo tuyapanue, ili pawe na nafasi hata ya kulipisha gari lililopata hitilafu,” anasisitiza.

 

Waambie wananchi suala hili tumelipokea na tutalifanyia kazi kwa kadri bajeti itakavyoruhusu. Tunaendelea kuiboresha barabara hiyo kila mara, wakati ule ajali ya Lucky Vincent ilipotokea alama za tahadhari zilikuwepo lakini wakasema zilikua chache, sasa tumewaongezea za kutosha ili dereva mgeni akipita asilete kisingizio chochote,” anasema mhandisi Kalupale.

 

Eveline Joseph, mkazi wa Karatu mjini ambaye amekuwa akitumia barabara hiyo mara kwa mara anasema ni vyema madereva wahakikishe magari hayana matatizo ya kiufundi kabla ya kukatiza barabara hiyo kwani lolote linaweza kutokea.

 

Madereva wawe na mazoea ya kufanyia service magari yao mara kwa mara, kwasababu gari likiwa na tatizo muda wowote linaweza kufeli breki katika milima na kona za Kilimatembo na Rhotia – Merera,” anaeleza.

 

Pamoja na gharama kubwa za kujenga miundombinu ya barabarani, lakini ajali za barabarani zinatajwa kuwa na gharama zaidi. Ripoti ya usalama barabarani ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ya mwaka 2018 inaeleza kuwa Tanzania hutumia asilimia 3 ya pato la Taifa kukabiliana na athari za ajali za barabarani, lakini pia hupoteza nguvu kazi kubwa kutokana na wengi wanaofariki kuwa ni vijana, hasa wanaume.

 

WHO inalitaja kundi kubwa zaidi ya vijana wanaofariki kwa ajali za barabarani kuwa ni lile la miaka 15 mpaka 29. Hili ni kundi la vijana walio kazini pamoja na walio taasisi mbalimbali za elimu, ikiwa ni maandalizi ya kuliingiza katika ujenzi wa Taifa, lakini ajali zinazima mipango yote na simanzi inatawala.

CREDIT: EATV


Loading...

Toa comment