The House of Favourite Newspapers

Naibu Spika Awatimua Bungeni Mnyika na Bulaya

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameagiza Mbunge wa Kibamba Mhe. John Mnyika na Ester Bulaya kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge kwa kile alichodai kutoheshimu kiti cha Spika.

Tulia ametoa maamuzi hayo jioni ya leo Mei 9, 2018 wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19, baada ya Mnyika kusimama akitumia kanuni ya 69(1), akitaka kuahirishwa kuhitimishwa kwa hoja ya wizara ya Maji na Umwagiliaji ili apewe nafasi ya kutoa hoja yake ya kwanini bajeti ya wizara hiyo isipitishwe na Bunge.

Kufuatia kauli hiyo, Tulia alisimama akitumia kanuni ya 69 (2), na kusema kama Spika atakuwa na maoni kwamba kuwasilishwa kwa hoja hiyo ni kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za Bunge, atakataa kuitoa ili ijadiliwe. Kutokana na mabishano hayo ya kinanuni, Tulia Ackson aliamuru Mnyika atolewe nje kwa kutoheshimu kiti cha Spika.

Mbali na Mnyika Naibu Spika Dk. Tulia Ackson amemtoa pia ndani ya Ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) kwa kutoheshimu kiti cha Spika.

Comments are closed.