The House of Favourite Newspapers

Naibu Waziri Ummy Ashiriki Hafla ya Chakula Siku ya Eid Al Fitr Chuo Cha Ufundi Yombo

0
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Watu wenye Ulemavu Yombo wakati wa hafla ya chakula cha mchana siku ya Eid el fitr, Mei 14, 2021 Jijini Dar Es Salaam.

Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu katika kusherekea sikukuu ya Idd El Fitir.

Akimwakilisha Waziri Mkuu katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema lengo la kuandaa chakula hicho ni kuendeleza umoja na kutoa faraja kwa kundi hilo la watu wenye ulemavu.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu akieleza jambo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Watu wenye Ulemavu Yombo.

Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Prof. Jamal Katundu, ametoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujenga utamaduni wa kuyajali na kuyasaidia makundi mbali mbali ya watu wenye mahitaji maalum kikiwemo chuo hicho cha watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa, amesema menejimenti pamoja na wanachuo wamefarijika sana na tukio hilo ambapo ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa tukio hilo.

Ummy Nderiananga (wa pili kutoka kulia) akimpatia chakula Kassim Ally katika hafla ya chakula cha mchana siku ya Eid El Fitr iliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wakipata chakula cha pamoja.

Aidha, baadhi ya wanachuo wameelezwa kufurahishwa na tukio hilo na wameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na viongozi mbali mbali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walijumuika nao katika chakula hicho.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo cha watu wenye ulemavu ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Kwasasa kina jumla ya wanafunzi 76 na kinatoa kozi mbali mbali zikiwemo; Ufundi Umeme, Uwashi, Ushonaji, Uchomeleaji Vyuma pamoja na Kilimo na Ufugaji.

Leave A Reply