The House of Favourite Newspapers

NAKAAYA SUMARI ATOBOA SIRI YA KUPIGA CHINI MUZIKI

WIMBO wa Mr Politician ulimtambulisha vyema mwanamuziki Nakaaya Sumari ‘Nakaaya’ kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva.

Nakaaya ambaye ni dada wa aliyewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2005, Nancy Sumari aliutoa wimbo huu kipindi kifupi tu baada ya kutoka kwenye mashindano ya Tusker Project Fame, yaliyofanyika wakati huo jijini Dar.

Baada ya kutoa wimbo huu alikuwa gumzo kila kona kwenye media za ndani na nje ya Bongo. Ni wimbo huo uliofanya mpaka media kubwa duniani ya CNN kufunga safari kuja Bongo kupitia kipindi kiitwacho Inside Afrika kwa ajili ya kufanya mahojiano na mwanadada Nakaaya.

 

Kama haitoshi, mwaka huo wa 2009, Nakaaya pia aliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo ya MTV Africa Music kwenye kipengele cha Listeners Choice (Chaguo la Wasikilizaji), kipengele ambacho alishinda mwanamuziki kutoka Kenya, aitwaye Nameless kupitia wimbo uitwao Sunshine.

Huyo ndiye Nakaaya Sumari, mwanadada aliyekimbiza pia kwenye kolabo kali ikiwemo ile aliyofanya na Kala Jeremiah ya Wimbo wa Taifa!

Hata hivyo baada ya kusumbua sana Bongo, akiwa amefanikiwa pia kuvuna Tuzo ya Pearl of Africa Music Awards, kutengeneza albamu moja iitwayo Where I Live, Nakaaya alipotea ghafla kwenye muziki.

 

Jambo ambalo watu wengi hawalifahamu ni kwamba kilichompoteza ilikuwa ni ajali mbaya aliyoipata mwaka 2011, kiasi kwamba mgongo wake ukaharibika vibaya na kumaliza miezi mingi akiwa amelala kitandani bila kufanya lolote lile.

Baadaye alipona na kuendelea na mishemishe zake, ambapo baada ya ukimya wa muda mrefu Over Ze Wikiend, imemnasa na akakubali kufanya mahojiano mafupi, ungana naye hapa chini;

Over Ze Wikiend: Kimya sana kwenye muziki Nakaaya, nini kinaendelea?

Nakaaya: Kiukweli kwa sasa nimeacha muziki.

 

Over Ze Wikiend: Kwa nini umeamua kupiga chini muziki, mashabiki bado wanapenda kukusikia.

Nakaaya: Ni kweli, lakini kwa sasa nina mambo mengi ya kufanya. Nina kampuni yangu ambayo inahusika na mambo mengi ikiwemo chakula, ndiyo nadili nayo kwa sasa.

Over Ze Wikiend: Kuna kipindi ulihamia Nairobi, Kenya, kwa sasa umerudi kuishi tena Tanzania. Nakaaya: Maisha yangu ni Kenya zaidi. Arusha Tanzania ni nyumbani, kwa hiyo ni lazima nirudi nyumbani.

 

Over Ze Wikiend: Sababu hasa ni ipi ya kuhamishia makazi yako Nairobi?

Nakaaya: Unajua Arusha ni mji mdogo. Kiukweli nina mambo makubwa ya kufanya kwa hiyo naona ni sehemu ndogo ya kuishi, ndiyo maana nikalazimika kutafuta sehemu kubwa. Lakini pia kumbuka nimekulia Nairobi.

Over Ze Wikiend: Unasikiliza muziki bila shaka, nani anakuvutia zaidi?

Nakaaya: Ninasapoti wanamuziki wote. Kiukweli wanafanya vizuri na muziki unakua na unakwenda mbali.

 

Over Ze Wikiend: Kipi kinakukera kwenye muziki?

Nakaaya: Hakuna.

Over Ze Wikiend: Vipi kuhusu familia?

Nakaaya: Nina mtoto anaitwa Kay, basi!

BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.