The House of Favourite Newspapers

‘National Public Speaking Competition’… Mkombozi Kwa Vijana Kutimiza Ndoto

0

TANZANIA na Dunia kwa ujumla inahitaji watu hususani vijana wenye uwezo wa kuzungumza kwa usahihi mbele ya hadhara. Kila nyanja katika jamii inahitaji watu wenye weledi na uwezo wa kuzungumza kama vile ilivyo padre, au mchungaji kanisani, Mashehe misikitini na hata viongozi wa kada mbalimbali kama siasa, pia hutakiwa kuwa na mbinu za kuzungumza kwa ufasaha.

 

Kwa kulitambua hilo, kampuni ya Global Publishers iliamua kuanzisha shindano la kitaifa linalolenga kusaka vipaji, lakini pia kuviendeleza vipaji hivyo vya vijana wenye uwezo wa kuzungumza katika hadhara.

Shindano lililopewa jina la National Public Speaking Competition, lilizinduliwa Novemba mwaka jana kwa kuanza na mchakato wa kugawa fomu kwa vijana nchi nzima ambapo walikuwa wanazijaza fomu hizo na kuzirejesha katika ofisi za kampuni hiyo.

Hata hivyo, baada ya zaidi ya fomu 400 kugawanywa, zaidi ya vijana 300 walijitokeza katika awamu ya kwanza ya shindano hilo ambayo ilianza Februari 10 mwaka huu kwa vijana hao kuanza kujielezea mbele za majaji kabla ya kuendelea na mchujo wa awamu ya pili.

 

Mmoja wa waratibu wa shindano hilo, Pacific Ibrahimu anasema hii ni kwa mara ya kwanza shindano hili kufanyika hapa Tanzania na Afrika Mashariki kiujumla.

 

“Tulitumia mfumo wa kutoa fomu ambapo washiriki walijaza fomu, na kwa kuwa ilikuwa ni kwa mara ya kwanza, tulitoa angalizo kwa washiriki wa mikoani kuja Dar es salaam

Hatua hii imeonesha ni aina gani ya washiriki tulionao maana wameonesha nia ya dhati kuthamini hiki kitu mpaka kuamua kutoka mikoani na kuja huku na kushiriki,” alisema.

 

Aidha, alisema majaji walioteuliwa katika usaili huo wamekidhi vigezo ambavyo sasa vitawasaidia kupata vijana 30 watakaoendelea katika mchujo wa awamu ya pili.

 

“Vijana hawa 30 watakaa kwa pamoja na watakuwa chini ya uangalizi wa majaji waliobobea katika uzungumzaji na kufundishwa njia mbalimbali za kutumia ili kujiimarisha zaidi,” anasema

Anasema miongoni mwa malengo ya shindano hili ni kuwajengea vijana uwezo wa kuzungumza mambo yenye mantiki kwa mpangilio wa mawazo ulio sahihi, kukuza uwezo wa kuihusisha hadhira mazungumzo, kulitawala jukwaa lakini pia kutumia vyema viungo mbalimbali vya mwili katika uzungumzaji ili kusaidia kufikisha ujumbe kwa urahisi.

 

WASHIRIKI WAISHUKURU GLOBAL PUBLISHERS

Washiriki hao pia wameonesha kukoshwa na shindano hilo na kuishukuru Global Publishers ambao ni waandaji wa shindano hilo kwa kuwasaidia kufikia malengo yao.

 

Mmoja wa washiriki wa shindano hilo, Charles Mwansasu anasema licha ya kuwa kuna zawadi nono katika shindano hilo, hata asiposhinda, elimu aliyoipata itamsaidia kukuza kipaji chake.

 

“Kwanza hapa kuna faida nyingi tunazipata kama washiriki, tunajifunza mengi tunayotakiwa kuyajua kuhusu tasnia hii ya uzungumzaji. Tunapata wasaa wa kusoma vitabu mbalimbali pindi tunapoandaa mada mbalimbali za kuziwasilisha, lakini pia imenipa nafasi ya kujuana na watu wengi na kutengeneza mtandao ambao ni faida kubwa kwangu,” anasema.

JAJI ALONGA

Naye Alice Nchwali ambaye ni miongoni mwa majaji wa shindano hilo, anasisitiza vigezo vya kumsaka mshindi ambavyo ni miongoni mwa vitu vinavyozingatiwa kwa umakini mkubwa, hivyo Watanzania wasubirie kuwapata vijana wenye weledi na ujuzi wa kuzungumza katika hadhara mbalimbali.

 

“Malengo yetu ni kuhakikisha tunazalisha vijana wengi wenye uwezo wa kusimama katika mkusanyiko mkubwa wa watu wakazungumza kwa kufuata vigezo vya uzungumzaji katika mihadhara.

 

“Wakifanikiwa kufikisha ujumbe uliokusudiwa, ni jambo ambalo tunajivunia mimi na timu nzima ya majaji kwa kuhakikisha tunazingatia vigezo vyote kwa umakini mkubwa ili tuweze kufikia malengo yetu na taifa kwa ujumla” anasema Nchwali

Leave A Reply