The House of Favourite Newspapers

NAVY KENZO; KUTOKA BANDA LA UANI HADI GHOROFA LA MIL. 400

Image result for NAVYKENZO
Aika Mariale na Nahreel.

KWA wafuatiliaji wa burudani ni wazi watakuwa wanalikumbuka Kundi la Pah One lililokuwa likiundwa na vichwa hatari kama vile Igwe, Ola, Aika Mariale pamoja na Nahreel.  

 

Ngoma ya Amatita ndiyo iliyowatoa na kubamba kila kona kutokana na staili yao ya uimbaji na kucheza, baadaye walikuja kutikisa tena na ngoma kadhaa kama vile I Wanna Get Paid pamoja na Ghetto.

Siku zote kizuri huwa hakidumu! Kundi hili lilikuja kusambaa ambapo Igwe na Ola walibaki kama Pah One huku Aika na Nahreel wakitengeneza kundi lao jipya waliloliita Navy Kenzo.

 

Japokuwa Pah One bado wanaendelea na harakati lakini Navy Kenzo limekuwa juu yao kwa muda mrefu wakitamba na vibao kibao kama vile Game, Bajaj, Feel Good na Chelewa. Kwa sasa kila kona gumzo ni ngoma yao mpya ya Katika waliomshirikisha Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ waliyoichia kwenye Mtandao wa Youtube yenye views zaidi ya milioni sita.

 

Uzuri wa Navy Kenzo licha ya kuwa ni wapenzi wenye mtoto mmoja, Nahreel ni bonge moja la prodyuza Bongo ambaye anahusika kwenye nyimbo zao ukiwemo wa Katika ambazo huzifanyia katika studio yao ya The Industry. Wawili hawa wamepitia ‘msoto’ wa kuishi pamoja katika mazingira magumu ambapo walikuwa wakiishi kwenye nyumba waliyoigawa studio ndani yake iliopo Mikocheni jijini Dar.

 

Kwa sasa wanamiliki mjengo wa ghorofa moja uliopo pembeni ya nyumba waliyokuwa wakiishi zamani wenye thamani ya shilingi milioni 400. Jiunge nao katika mahojiano maalumu kuhusu maisha yao na ya kimuziki;

WALIKUTANA WAPI MARA YA KWANZA?

“Kwa mara ya kwanza tulikutana nchini India, ambapo kila mmoja alikuwa nchini humo kwa ajili ya masomo lakini tulijikuta tu tunazoeana kwa sababu mimi nilikuwa napenda sana kuimba na Nahreel naye ikawa hivyo hivyo anapenda mambo ya kutengeneza muziki.”

 

WALIANZAJE KUISHI PAMOJA?

“Tulivyorudi Tanzania, kila mmoja aliamua kuwa kivyake ambapo mimi nilienda Arusha ambako ndiyo nyumbani na Nahreel akabaki Dar lakini bado tukaona kama tuko mbalimbali na tunahitaji kuwa karibu zaidi hivyo, Nahreel alikuja Arusha akawa anaendelea kufanya kazi ya uprodyuza mpaka tulivyoamua kuja Dar wote.”

 

ILIKUWAJE WAKAANZA MAISHA YAO?

“Maisha yalikuwa ni magumu mno asikwambie mtu yaani ukila mlo mmoja unashukuru sana Mungu na sio kwamba kwa wazazi wetu kulikuwa hakuna kitu lakini tu hawakupenda tujihusishe na mambo ya muziki hivyo waliamua kutuacha kwanza.”

 

Watumia sebule ndio studio“Kutokana na maisha kuwa magumu maana hata nyumba yenyewe tuliomba tulipe kodi kidokidogo lakini sebule ndio tukawa tunaitumia kama studio na kigodoro chetu mchana kinakuwa kochi usiku ndio kitanda na wala tulikuwa hatujali kabisa, tulijua tutafika tu huko mbele tunapotaka.”

 

WALIUMWA VIDONDA KWA KUKOSA KULA

“Kutokana na ugumu wa maisha tulikuwa tukishinda njaa, tukapata maradhi ya vidonda vya tumbo ambapo tuliamua kutafuta tiba.”

 

KWA NINI WAZAZI WAO HAWAKUWASAIDIA NA WANA HELA?

“Si kama wazazi hawakuwa na hela ya kutusaidia, walikasirishwa na uamuzi wetu wa kufanya muziki kwa wakati huo, tulitaka kuwaonesha wazazi kuwa muziki si kazi mbaya pamoja na kuwa walikasirishwa na sisi kuamua kuufanya wakati wametusomesha kwa kazi nyingine, ingawa hiyo sasa ni historia tuko vizuri na wazazi na wameikubali kazi.”

WALIPATA WAPI WAZO, FEDHA YA KUJENGA?

“Kiukweli ndoto yetu kubwa ilikuwa mimi niishi nyumba ninayoipenda na Nahreel pia lakini tukajiuliza tunaweza kufanikisha kweli? Tukajipa moyo, tukatoa Wimbo wa Kamatia uliotuletea mafanikio makubwa sana.

“Tulipokuwa tumepanga pembeni kulikuwa na kiwanja kama utani bwana mtu akatuunganisha tukaanza kulipa kidokidogo mpaka tukamaliza, ilikuwa ni milioni 50 hivi. ”

 

WAPOROMOSHA JUMBA LA MAANA

“Baada ya kununua kiwanja tu tukaita mtu ambaye alitukadiria gharama ambapo ilikuwa karibu milioni 700, lakini kwa sababu bado hatukumaliza vitu vingine ikagharimu kama 350 pamoja na ile ya kiwanja jumla ikawa kama 400.”

 

VIPI KUHUSU NDOA?

“Unajua baada ya watu wengi kuniambia kuhusu ndoa kila wakati nikajifunza maana halisi ya ndoa kwanza kabla sijaingia ndani maana ninajua hakuna mtu anayefahamu jinsi gani nampenda Nahreel kuliko hata hiyo ndoa.”

Na Imelda Mtema

WAZIRI MKUU azungumzia hali ya usalama nchini/ajali

Comments are closed.