The House of Favourite Newspapers

NBC Yakabidhi Trekta kwa Chama cha Ushirika Mtwara

0
Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Abdallah Mohamed Malela (wa pili kushoto)akijaribu ubora wa trekta lililotolewa na Benki ya NBC kwa mshindi wa droo ya sita ya kampeni ya ‘Vuna Zaidi na NBC Shambani’ambae ni Chama kikuu Cha Ushirika wa wakulima Mtwara-Masasi ( MAMCU) wakati wa hafla fupi ya kukabidhi ya zawadi hizo iliyofanyika katikati ya wiki mkoani Mtwara. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw Dastan Kyobya (wa sita kushoto), Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Bw Waziri Barnabas, viongozi waandamizi wa benki hiyo, wakulima na viongozi wa MAMCU.

Mtwara: Disemba 15, 2021: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC)imekabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo baiskeli, pikipiki, guta na trekta kwa washindi wa droo ya sita ya kampeni ya ‘Vuna Zaidi na NBC Shambani’kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi, huku serikali ikibainisha kuwa zawadi hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuchochoea kasi ya uzalishaji wa mazao ya korosho na mazao mengine katika mikoa hiyo.

Wanachama Chama kikuu Cha Ushirika wa wakulima Mtwara-Masasi ( MAMCU) pamoja na uongozi wa chama hicho wakifurahia baada ya kukabidhiwa trekta lililotolewa na Benki ya NBC baada ya chama hicho kuibuka mshindi wa droo ya sita ya kampeni ya ‘Vuna Zaidi na NBC wakati wa hafla fupi ya kukabidhi ya zawadi hizo iliyofanyika katikati ya wiki mkoani Mtwara.

Akizungumza katikati ya wiki mkoani Mtwara wakati wa hafla fupi ya kukabidhi ya zawadi hizo kwa washindi mbambali wa droo hiyo ikiwemo zawadi kubwa ya trekta kwa Chama kikuu Cha Ushirika wa wakulima Mtwara-Masasi ( MAMCU), Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Abdallah Mohamed Malela alisema zawadi hizo zimekuja wakati muafaka kwa kuwa mkoa huo upo kwenye utekelezaji wa mkakati wake wa kuongeza uzalishaji wa zao la korosho kutoka tani 280,000 zinazozalishwa sasa hadi kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

“Zaidi pongezi nizielekeze kwa MAMCU kwa kuwa wanapokea zawadi hii ya trekta ikiwa ni hivi karibuni tu kama mkoa tuliweka azimio la msingi kwamba kuanzia msimu ujao wa kilimo kila chama kikuu cha ushirika lazima kiwe na shamba darasa lenye ukubwa wa ekari 1500 ili kufikia malengo ya uzalishaji wa mazao ya korosho na mazao mengine ya kimkakati. Kupitia zawadi hii ni wazi NBC imewashika mkono naomba na nyinyi pia muishike mkono,’ alisema.

Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Abdallah Mohamed Malela (katikati) akikabidhi zawadi mbalimbali kwa wakati wa hafla fupi ya kukabidhi ya zawadi hizo iliyofanyika katikati ya wiki mkoani Mtwara. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw Dastan Kyobya, Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Bw Waziri Barnabas, viongozi waandamizi wa benki hiyo, wakulima na viongozi wa MAMCU

Zaidi Bw Malela aliwasisitiza wakulima mkoani humo kuhakikisha wanahifadhi fedha zao benki sambamba na kuongeza nidhamu ya matumizi ya fedha zao hata pale wanapozihifadhi kwenye taasisi za kifedha na wazitumie kwenye mahitaji ya msingi ikiwemo kuwekeza zaidi kwenye zana za kilimo cha kisasa ili kuboresha hali za maisha yao na familia zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw Dastan Kyobya aliahidi kutoa eneo la ekari 1500 kwa MAMCU ili liweze kutumika katika kufanikisha shughuli za kilimo cha ushirika huo, ikiwa ni ishara pia ya kuunga mkono nia njema ya benki ya NBC katika kuwasaidia wakulima hao.

“Kwa kuwa NBC tayari wameanza kwa kuwazawadia zana za kilimo ikiwemo trekta na sisi serikali ya mkoa tunawapatia eneo la kutosha ekari 1500 ili muweze kufanikia azimo la kulima ekari 1500 katika msimu ujao wa kilimo…hongereni sana’’ alisema Bw Kyobya huku akiiomba benki hiyo kuendelea kufungua matawi mkoani humo sambamba na kuangalia uwezekano wa kutumia wakulima wenye sifa kufungua huduma za uwakala wa huduma za kibenki katika maeneo ambayo benki hiyo haina matawi yake.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Bw Waziri Barnabas alisema tangu kuanza kwa kampeni hiyo tayari jumla ya washindi 139 wamejipatia zawadi mbalimbali ikiwemo baiskeli, pikipiki, pampu za kupulizia dawa mikorosho, guta (Toyo) pamoja na zawadi za nyingine ikiwemo kanga, mabegi ya shule na madaftari vikiwa na thamani ya takribani sh mil 200.

Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Bw Waziri Barnabas akizungumza kwenye hafla hiyo.

Nae Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo wa Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa alisema kupitia droo hiyo benki ilitoa zawadi za aina mbalimbali zipatazo 26 ikiwemo trekta 1, pikipiki 7, baiskeli 9, pampu za kupulizia dawa mikorosho 8, guta (Toyo)1, pamoja na zawadi za nyingine ikiwemo kanga, mabegi ya shule na madaftari kwa wakulima mmoja mmoja, AMCOS na vyama vikuu ushirika katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

“Naendelea kuwahamasisha wakulima waendelee kupitishia fedha zao kupitia benki akaunti ya NBC Shambani ili wawe kwenye nafasi kujishindia zawadi lukuki katika droo zinazofuata,’’ alisema Bw Urassa

Kwa upande wao washindi wa droo hiyo waliishukuru benki ya NBC kwa kuandaa kwa kampeni hiyo kwa kuwa imekuwa na msaada mkubwa kwao.

Meneja wa benki ya NBC Tawi la Mtwara Bi Editha Mwakatobe akizungumza kwenye hafla hiyo.

“Zawadi hii ya trekta imekujwa wakati muafaka sana kwa kuwa kwasasa tumeshaanza utekelekezaji wa azimio la kulima ekari 1500 kwa ajili ya kilimo cha korosho na mazao mengine. Tunawashukuru sana NBC kwa kuwa trekta hili litakuwa msaada mkubwa sana kufanikisha hilo. Katika kurejesha shukrani zetu kwao tunaahidi kuendelea kupitisha fedha zetu kupitia akaunti za NBC Shambani ili tuweze kuwania zawadi zaidi,’’ alisema Bi Biadia Matipa ambae ni Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU.

Leave A Reply