The House of Favourite Newspapers

NBC Yaungana na Jubilee Kutumia Mtandao wa Mawakala wa Bima NBC Kuuza Bidhaa za Bima

0
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, akizungumza na mawakala waliojitokeza kwenye uzinduzi wa mafunzo ya bima kwa mawakala, yanayotolewa na Benki ya NBC pamoja na Jubilee Alience Insurance kupitia Chuo cha Bima na Hifadhi ya Taifa(ACSID). Jumatatu 21 Novemba,2022, Posta-Dar-es-Salaam.

 

DAR ES SALAAM – Novemba 22, 2022. Ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha utoaji wa huduma za bima nchini, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeshirikiana na Jubilee Allianz kutoa mafunzo kwa mawakala wa Benki hiyo (NBC Wakala) na kuwapatia vitendea kazi na maarifa ya huduma za bima katika lengo la kukuza mauzo.

 

Mapema wiki hii, Benki kwa ushirikiano na washirika wa bima ya Jubilee Alliance General Insurance, ilianza mafunzo ya wiki tano  kwa Wakala wa Benki hiyo ili kuwaelimisha na kuwapa taarifa za bidhaa.

Picha ya pamoja kwenye hafla hiyo.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, alisema benki hiyo inaunga mkono ajenda ya Serikali ya huduma za kifedha jumuishi kwa kuweka huduma za kibenki na bima karibu na wateja kupitia mtandao wa NBC Wakala. “Tanzania ina kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma za bima katika Afrika Mashariki, chini ya asilimia 1. Kwa mtandao mpana zaidi wa NBC Wakala zaidi ya elfu nane kote nchini, tuna uhakika wa kuwafikia watu wengi na kuwapa huduma hizi muhimu za bima. Tunatoa huduma mbalimbali za bima kwa magari, mali, na ustawi kupitia bima ya maisha na afya,” alisema Sabi.

 

Sabi pia alieleza kuwa mawakala hao sasa watatumia mfumo maalum uliotengenezwa na benki na washirika wake ili kurahisisha utoaji wa huduma za bima. “Mauzo yetu ya bima kupitia mawakala yatafanywa kupitia mfumo maalum uliotengenezwa na benki na washirika ili kufanya huduma hiyo iwe ya kipekee, na ya kirafiki na jumuishi,” alibainisha.

 

Kwa upande wake, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk. Baghayo Saqware, aliipongeza Benki ya NBC na Jubilee Allianz kwa kutekeleza wito wa Serikali wa kupanua wigo wa huduma na bidhaa za bima nchini. Dk Saqware alikumbusha kuwa Mei 2022, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, ilitoa mwongozo unaoelekeza makampuni na watoa huduma za bima kusajili maafisa mauzo wa bidhaa za bima nchini.

 

“Nimefurahi kuona kwamba Benki ya NBC imekuwa ya kwanza kuitikia azma hii, na kwa kushuhudia mafunzo haya, hakuna shaka kwamba kutakuwa na upatikanaji mzuri wa huduma ya bima nchini kote. Ninaipongeza NBC na Jubilee Allianz kwa kuongoza katika mpango huu, na ninatumai kuwa taasisi nyingi zaidi pia zitashiriki. Baada ya muda mfupi, Watanzania wengi watakuwa na upatikanaji rahisi wa huduma za bima,” alisema Dk. Saqware.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Jubilee Allianz, Bw. Dipankar Acharya, alisema, “Hii ni fursa ya kusisimua kwa mawakala na umma kupata bima ya afya kwa urahisi. Nimefurahishwa na ushiriki na maswali yanayoulizwa. Hii inaonyesha tumejipanga katika kutoa huduma bora za bima kote Tanzania.”

 

Mawakala watafanya mafunzo na uhamasishaji wa kujiunga na bima zaidi kwa kufuata michakato inayoratibiwa na TIRA na mamlaka nyinginezo ili kuhakikisha kuwa huduma za haraka, zinazopatikana kwa urahisi na zinazofaa zinatolewa.

Leave A Reply