Ndevu za Prince Harry Zashutumiwa Kwenye Hafla Ya Kijeshi

Prince Harry akishiriki Jumapili ya Kumbukumbu.

 

PRINCE Harry ambaye ni mtoto wa Prince Charles na mjukuu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza, yuko katika misukosuko kwa kuvunja sheria za kijeshi kwa kufanya jukumu la kijeshi akiwa na ndevu na akiwa amevaa kijeshi.

 

Harry  (33) ambaye jina lake halisi ni Henry, alikuwa mmoja wa maofisa walioshiriki katika Jumapili ya Kumbukumbu kwa watu wa Uingereza waliokufa sehemu mbalimbali duniani na ambao makaburi yao hayafahamiki yalipo.

 

Mwaka 2015, akiwa na umri wa miaka 31, Harry aliondoka jeshini baada ya kupewa cheo cha Cornet, lakini alikuwa bado mshiriki katika kikosi cha farasi cha Malkia ambapo maofisa wenzake wamesema “ametuangusha”.

 

Hata hivyo, msemaji wa taratibu za tamaduni za kijeshi amesema, Prince Harry halazimiki kufuata sheria za kijeshi zilizopo.

 

Licha ya kuacha kulitumikia jeshi, msemaji katika kikosi anachotumikia sasa Harry, alisisitiza kwamba hakufurahi kumwona Harry akiwa hakunyoa ndevu kwenye tukio hilo.
Akisisitiza msimamo wa wenzake alisema: “Prince Harry anatuangusha.  Hapana nafasi ya kufuga ndevu katika kikosi cha farasi cha Malkia.  Alilazimika kuzinyoa kwa ajili ya ushiriki wake katika siku hii muhimu.”

 

Sheria za jeshi la Uingereza zinakataza kufuga ndevu, isipokuwa tu katika mazingira machache, kama askari kukumbwa na magonjwa ya ngozi akinyoa ndevu zake, au mazingira ya kidini kama vile Masingasinga ambao huwa hawanyoi ndevu na nywele.

 

NA WALUSANGA NDAKI/GPL

Toa comment