The House of Favourite Newspapers

Ndoa Isikufanye Uwe Na Papara

0

NDOA ni jambo la heri kwa kila mwanadamu hasa anapokuwa amefikia wakati wa kuolewa au kuoa, kwani kwa tamaduni za kiafrika ukifikisha umri flani hujaolewa au kuoa inaonekana kama ni mkosi vile na watu hukunyooshea vidole, kitendo ambacho huwaumiza watu wengi hasa wanawake. Ni wanaume wachache ambao hukaa na kuliwaza jambo hilo la ndoa kama ilivyo kwa mwanamke kwani mara nyingi yeye ndiye husemwa vibaya.

 

Maana ya mada yangu ya leo hapa ni kuwapa faraja wale wote ambao hawajaolewa kwani kuolewa ni mipango ya Mungu na kila mmoja amempangia siku yake ya ndoa hata akiwa mzee, kwani tumeshashuhudia wengi wakiolewa wakiwa na umri mkubwa kabisa.

 

Awali ya yote hayo niliyoanza nayo, ni kukueleza wewe unayeweza kudanganyika kwa sababu tu umetajiwa neno nitakuoa, nakusihi sana usiwe na papara ya kuingia kwenye maisha ya ndoa wakati hujamjua kiundani mwanaume anayetaka kukuoa, kwa maana ya tabia zake, makuzi yake, kazi yake na mambo mengine mengi ambayo ukishaingia kwa papara unaweza kujikuta unajuta na kuishia kwenye kuivunja ndoa yako hapo sasa ndiyo utanyooshewa sana vidole.

 

Wapo akina baba ambao si waoaji lakini ili wampate mwanamke gia yao ya kuingilia ni kumweleza jinsi anavyotaka kumuoa na mwanamke kama ana kiu ya kuolewa, anaingia mazima, lakini mwisho hujikuta akiishia kuumia. Hao ni wa gia ya kumpatia mwanamke, lakini wapo ambao humlaghai mwanamke kwa kumtajia ndoa na kumuingiza kwenye ndoa yenyewe lakini akishaingia anakutana na mambo ambayo yanakuwa ni mwiba mkali kwake. Kuwa mpole hata kama unao uhitaji wa ndoa kiasi gani ni lazima ujipange kwa kila kitu, ndoa si lelemama kama unaamua kuingia ujue kuna mbivu na mbichi na ujue utazikabili vipi.

 

Kuna mkasa wa dada mmoja ambaye ndiyo amenifanya niandike makala haya yeye anasema alikaa bila ya kupata mwanaume wa kumuoa mpaka alipotimiza umri wa miaka 45, siku moja akakutana na mwanaume akamtongoza na kumweleza jinsi alivyomvutia na nia yake ya kutaka kumuoa.

 

Dada kusikia ndoa alichanganyikiwa kwani ndicho kitu alichokuwa akikisubiria kwa hamu, walikaa kama wiki tatu hivi hatua
zote za ndoa zikaanza wakafunga ndoa na kuwa mume na mke.

 

Dada huyo anasimulia aliyokutana nayo ndani ya ndoa, kwani ndoa ilimshinda kwa miezi sita tu, alikutana na visa vya mwanaume kutoka na kila aina ya wanawake huku akiwaleta nyumbani lakini hiyo haikutosha mwanaume huyo hakuwa na kazi ya maana zaidi ya ujambazi ambapo alikuwa akipata pesa kwa muda na zikikata pesa hizo nyumba inakuwa haikaliki.

 

Sasa kwa haya machache wapenzi wasomaji wa makala hii naamini mmepata somo kubwa ambalo litawafanya msiwe na papara kisa mmetamkiwa ndoa, tulia na uchunguze taratibu je, unapoingia panafaa au ndiyo unajimaliza kabisa. Ni bora ufanye kazi kwa bidii uwe na amani kuliko kukimbilia ndoa ambayo inakuingiza matatani. Kwa haya machache tukutane wiki ijayo kwa makala nyingine kali.

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leave A Reply