The House of Favourite Newspapers

NDOA YA LULU USIPIME!

DAR ES SALAAM: Iyena Iyena… Iyena Iyena…Iyena Iyena…Kwa heri tutaonana! Ndivyo zitakavyokuwa cherekochereko siku ya ndoa ya malkia wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ itakayofungwa mwezi ujao wa Desemba, mwaka huu ambapo maandalizi yake usipime, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.

 

Wikiendi iliyopita furaha ilitawala nyumbani kwa mama wa staa huyo, Lucresia Karugila ‘Mama Lulu’ maeneo ya Mbweni jijini Dar, wakati mrembo huyo akitolewa mahari na mumewe mtarajiwa ambaye ni mmiliki wa Radio EFM, Francis Siza ‘DJ Majizo’.

 

MAANDALIZI USIPIME

Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa mtu wa ndani wa familia ya Lulu zilieleza kwamba kutolewa huko kwa mahari ni sehemu ya maandalizi baab’kubwa ya ndoa hiyo. Chanzo hicho kililithibitishia gazeti hili kwa uhakika kuwa ndoa ya Lulu itafungwa kabla ya siku 40 zilizobaki kumalizika kwa mwaka huu wa 2018.

 

Maandalizi hayo yanakuja ikiwa ni siku chache tangu Lulu amalize adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia na mahakama ya kumuua bila kukusudia Steven Kanumba. Chanzo hicho kilitiririka kwamba, maandalizi ya shughuli hiyo kabambe yanaendelea kwa kasi ili kukamilisha mambo ambayo yamesalia.

UKUMBI WA MLIMANI CITY WATAJWA

“Kuna vitu vidogovidogo tu vya makubaliano ya mwishomwisho juu ya ukumbi gani wenye viwango vya hali ya juu utumike, lakini ule wa Mlimani City (Dar) unapigiwa chapuo na wengi. “Kinachoonekana wengi wameuchagua Ukumbi wa Mlimani City kutokana na aina ya watu walioalikwa.,“Mialiko itatolewa kwa watu maalum wenye vyeo na majina makubwa hapa nchini na nje ya nchi.

 

VIONGOZI WA SERIKALI

“Lulu amepanga harusi yake ihudhuriwe na viongozi wengi wa Serikali, wabunge, mabosi wa taasisi na kampuni kisha mastaa wenzake wa filamu na muziki, ndugu, jamaa na marafiki. “Si unajua Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Harusi ya Lulu na Majizo ni Paul Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar)? Basi ujue siyo shughuli ya kitoto!

 

MAGARI YA KIFAHARI

“So unaambiwa kila kitu kinakwenda sawia kuanzia usafiri maana harusi ya Lulu itafunga barabara Jiji la Dar kwa muda kutokana na misururu ya magari ya kifahari. “Kama hiyo haitoshi, kama nilivyosema mambo ya ukumbini, unaambiwa watu watakula na kunywa hadi wasaze.

 

FUNGATE ULAYA

“Baada ya shughuli ya ukumbini, ngoja nikung’ate sikio kuwa honeymoon (fungate) itakuwa Paris (nchini Ufaransa) barani Ulaya.

VIPI KUHUSU MICHANGO?

“Mpaka sasa hivi taarifa zilizopo ni kwamba hakuna mtu atakayechangishwa badala yake atapokea tu mwaliko,” kilidai chanzo hicho na kuongeza:

 

“Kuhusu gauni la harusi siyo la nchi hii kwani Lulu alishaweka oda nje ya nchi muda mrefu kwa njia ya mtandao. Kwa hiyo kwenye eneo la mavazi na bling’ibling’i Lulu ndiye mwenyewe. “Kwa kifupi tu, chukua harusi zote kubwa zilizowahi kufanyika hapa Bongo, hakuna itakayofikia ya Lulu.

 

“Lulu amepanga kuweka rekodi ya kipekee itakayodumu kwa muda mrefu hadi atakapojitokeza mtu mwingine wa kumfunika, lakini kwa zilizopita, hakuna ya kuifunika ya Lulu.”

MASTAA WASUBIRI MWALIKO TU

Kufuatia taarifa za kutotoa mchango na kusubiria tu mwaliko, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya mastaa ambao walisema wanazo taarifa hizo, lakini bado hawajapewa kadi za mwaliko hivyo wanasubiria. “Ni kweli tumesikia hakuna michango, tunachosubiri tu ni mwaliko,” alisema mmoja wa mastaa wakubwa wa filamu za Kibongo aliyeomba hifadhi ya jina.

 

MAMA LULU SASA

Ili kupata udambwidambwi kamili wa ishu hiyo, gazeti hili lilimtafuta Lulu na lilipomkosa liliwasiliana na mama yake ambaye baada ya kuulizwa ukweli juu ya maandalizi hayo alikuwa na haya ya kusema kwa kifupi kisha akakata simu: “Niko bize (huenda yupo bize na maandalizi hayo).”

 

MSIMAMIZI MAKONDA

Kwa upande wake Makonda ambaye ndiye msimamizi wa ndoa hiyo alitoa taarifa kuhusiana na wawili hao kukutana siku hiyo ya Jumapili iliyopita. “Mrembo Elizabeth Michael ‘Lulu’ anadaiwa ametolewa mahari na mpenzi wake wa muda mrefu, Majizo ikiwa ni maandalizi ya ndoa yao mwisho wa mwaka huu,” aliandika Makonda kwenye ukurasa wake wa Instagram.

 

TUMEFIKAJE HAPA?

Taarifa za Lulu kufunga ndoa na Majizo zilianza kuzagaa tangu mwaka jana. Hata hivyo, haikufanyika. Sababu kubwa ikitajwa ni kesi iliyokuwa ikimkabili staa huyo wa filamu. Pia mipango ya Lulu kutaka kufunga ndoa ilianza tangu mwaka 2012, lakini Mungu hakupenda, ikayeyuka.

 

Mwaka huo kulikuwa na taarifa za Lulu kuvishwa pete ya uchumba na Kanumba. Hata baada ya kifo cha Kanumba, habari za Lulu kutaka kuolewa hazijawahi kukoma kwani mwaka 2013 alidaiwa kupata mchumba wa kuziba pengo la Kanumba, lakini kwa bahati mbaya, mwanaume huyo alifariki dunia.

 

Ulipoingia mwaka 2015 zilianza kusikika tena habari za Lulu kupata mchumba. Katika mitandao ya kijamii umbeya ulisema mfanyabiashara huyo anataka kufunga ndoa na Lulu. Mwaka 2016, ikagundulika kuwa mfanyabiashara huyo ni Majizo aliyetoka kuachana na mwanamitindo Hamisa Mobetto na uhusiano wao ulianza tangu mwaka 2015.

Stori: SIFAEL PAUL NA IMELDA MTEMA, RISASI MCHANGANYIKO

HIVI NDO’ VITU KONKI ANAVYOVIPENDA MAGUFULI!

Comments are closed.