The House of Favourite Newspapers

Nelly Mwangosi Aelezea Anavyonufaika na Mjengo wa Global

0
Baadhi yab samani zilizomo kwenye nyumba aliyoshinda Nelly Mwangosi.

 

WAKATI siku za kuchezeshwa kwa droo kubwa ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili zikikaribia, mshindi wa bahati nasibu ya kwanza, Nelly Mwangosi ambaye ni mkazi wa Iringa, ameibuka na kuzungumza mambo mbalimbali yanayohusiana na nyumba yake hiyo iliyopo Salasala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Iringa anakoishi, Nelly ambaye ni mjasiriamali, mama wa watoto wawili, alisema kuwa, baada ya kukabidhiwa nyumba hiyo mwaka jana, alimuweka mlinzi ambaye alikuwa akimlipa kila mwezi kwa kuwa familia yake bado haijaamua kuishi jijini Dar.

 

  Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers Ltd, Eric Shigongo akimkabidhi mshindi wa nyumba, Nelly Mwangosi mkataba wa makabidhiano ya nyumba hiyo. Kushoto ni mume wa Mwangosi, Karolo Stephen Magani na katikati ni kijana wao, Emmanuel Karolo.

 

 

“Tulipokabidhiwa, tukamuweka mlinzi wakati tunaangalia taratibu zingine, baadaye tukaona hatuwezi kwenda kuishi kwa sasa, kwa hiyo tukatafuta mpangaji, tunashukuru, tumempeta ambaye kodi anayonilipa, sasa inatumika kuwasomesha wanangu wawili.

“Mmoja mkubwa anasoma shule moja kule njombe, yupo kidato cha pili sasa na huyu mwingine ni bado mdogo, yeye yupo chekechea hapa Iringa. Kwa kweli bajeti yao kwa ajili ya ada imeisha kabisa kwangu, shughuli ninazofanya mimi na mume wangu tunatumia kwa ajili ya mambo mengine.

 

“Mpangaji wetu ni mtu mwenye familia yake na ninashukuru anaiangalia nyumba vizuri, mara ya mwisho nilikwenda Desemba mwaka jana na nikaikuta nyumba ipo vizuri kabisa.

 

Shigongo akimkabidhi mshindi wa nyumba, Nelly Mwangosi ufunguo wa nyumba hiyo.

“Kwa kweli ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuibuka mshindi wa mwaka jana, lakini pia ninaishukuru sana Global Publishers kwa kukubali kurudisha kidogo kwa wasomaji wake. Niwasihi wasomaji wenzangu kuomba Mungu na kutokata tamaa kwa sababu hata mimi wakati ninashiriki mwaka jana, sikutegemea kabisa kama nitashinda.

 

“Wito wangu kwao, wajitahidi kukata kuponi na kuzituma, huwezi kujua nani atapata safari hii, cha msingi ni kuomba Mungu tu,” alisema mshindi huyo.

Juni 30, mwaka jana, Nelly Mwangosi alitangazwa kuwa mshindi wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba awamu ya kwanza iliyoendeshwa na kampuni ya uchapaji Magazeti ya Global Publishers katika droo kubwa iliyofanyika kwenye kwenye Viwanja vya Mbagala-Zakheem jijini Dar.

Ofisa Masoko wa Global Publishers, Yohana Mkanda, alisema jana kuwa, huu ni wakati muafaka wa wasomaji wote waliokata kuponi zao kuziwasilisha kwa mawakala wao nchi nzima.

 

Nelly Mwangosi akifanya mahojiano na Mtangazaji wa Global TV Online, Kelvin Shyao.

 

“Nyumba siyo kitu kidogo, kila mtu angetamani kumiliki nyumba jijini Dar, sasa hii ni fursa adimu ambayo haikulazimu kuwa na mamilioni ya kujenga au kununua, ni kiasi cha kwenda kwa muuza magazeti yeyote, popote alipo Tanzania na kujipatia mojawapo ya magazeti yetu ili ujiweke katika nafasi nzuri ya kuwa mmoja wa wamiliki wa nyumba bora nchini,” alisema Mkanda.

Nyumba hiyo ambayo kama ile ya kwanza imejengwa Dar, itakuwa ni ya kisasa ikiwa na samani zote ndani yake, kiasi cha kumfanya mshindi kuingia na begi lake tu la nguo ili kuanza maisha.

Bahati Nasibu hii ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili imedhaminiwa na Kampuni ya Premier Bet.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply