The House of Favourite Newspapers

NETI HAIGEUZWI PAZIA

WASWAHILI wanakwambia mtoto wa mjini halali njaa ila anachelewa kula na ukisubiri urithi wa viatu utatembea peku mjini upo nyonyo? Ndo’ nishaingia tena mjini Anti Naa wa kujiachia, najua kuna wengine mkiingia tu kona hii mnakuwa na vijiroho vya kwa nini, mshindwe!  

 

Shoga hakuna raha kama kubebwa na aliyekubeba usimtekenye na ndiyo maana tajiri anuniwi shoga yangu, uongo? Maana nashangaa tangu lini kungwi akaogopa haja ndogo?

Tuachane na udambwidambwi tuingie kwenye kile kilichonifanya nije hapa, ujue shoga kuna maisha mengine ukiona wanavyoishi unakereka, linakufika hapa kwenye koo hata feni ikupulize vipi unabaki na hasira! Ifike mahali basi tusikaushane uzazi!

 

Shoga wenzako wanalilia kupata mtoto wewe unaona hafai tena akiwa na miaka miwili au mitatu tu, shuuuuutuuuuu! Nasema haya namaanisha ati! Juzi kwa macho yangu nimeshuhudia dada mmoja akitoa mijitusi ya nguoni kwa mtoto mdogo, mtoto ambaye ndiyo kwanza anajifunza kuongea, nikauliza ni wake wa kumzaa nikaambiwa ndiyo, loooo!

 

Ndiyo maana kila siku siachi kulalamikia kwamba sisi wanawake tunasababisha wakati mwingine tuonekane wote akili zetu sawa! Hivi kweli mtoto wa kumzaa, uliyemuweka tumboni kwa miezi tisa na pengine ukajifungua kwa uchungu kwa oparesheni baada ya miaka miwili mitatu unasahau na kumtolea matusi! Haya basi akiyakariri kesho na keshokutwa akayaropoka mbele ya wakwe zako hiyo aibu utaificha wapi?

 

Sasa basi, baada ya yule dada kutoa mitusi mbele ya mtoto, nikataka kumfuata kwa bahati iliyoje bajaj ikatokea na kuondoka naye huku yule mtoto akilia mwenyewe! Baada ya kumuulizia nikaambiwa eti amepinda tangu zamani na huyo mtoto alimpata baada ya kuhangaika na wanaume wa dunia, nikachoka!

Shoga wanakwambia bora uwashwe na kichwa utajikuna lakini siyo ulimi, huyo bidada sasa amekuwa kero na mwenye nyumba yake hivi ninavyoongea ameshampa notisi aondoke maana anabadili wanaume kama njugu na mbaya zaidi amekuwa kero kwa makelele yake ya mahaba yanayomharibu mtoto kisaikolojia!

 

Najaribu kufikiria wanawake sisi tunaopitia maisha ya kucheza vibaya na watoto kama haya, kuna wengine huko miaka kumi wanatafuta mtoto na wapo ndani ya ndoa, mwingine amejaliwa kila kitu ndani lakini amani inapotea kwa sababu hana mtoto nakushangaa wewe unayemharibu mtoto, haya kesho na keshokutwa unataka kumjengea maisha gani?

 

Aje kuwa jambazi au mvuta bangi? Badilikeni basi wanawake wenzangu, neti na uzuri wake lakini hata siku moja huwezi kuikuta inageuzwa pazia iwe la mlango au dirishani! Kwa leo niishie hapa, tukutane tena wiki ijayo! Ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu!

Comments are closed.