The House of Favourite Newspapers

NGUVU YA UVUMILIVU NA MAANA YA MAPENZI!

NI Jumatatu nyingine njema, Mungu ametupa tuweze kujidaidai hapa duniani. Ni vyema kumshukuru na kuendelea kumsifu yeye siku zote za maisha yetu hapa duniani. Tunaishi kwa sababu ya mapenzi Yake, tutaondoka pia kwa mapenzi Yake.

 

Baada ya utangulizi huo, moja kwa moja niende kwenye mada yangu ya leo. Hakika kila mmoja wetu anajua maana ya neno uvumilivu. Ni neno fupi tu lakini lina maana kubwa sana katika ulimwengu wa wapendanao. Nasema lina maana kubwa kwa sababu ya uhalisia wa mahusiano. Mwanamke anakutana na mwanaume ambaye kila mmoja anakuwa na tabia zake.

 

Mnakutana ili muweze kuishi pamoja kwa miaka yenu yote, angalia jinsi mtihani huu ulivyo mgumu. Mtu ana tabia zake za asili ambazo ameziishi kwa miaka 20 au zaidi kabla ya kukutana na wewe ambazo pengine si nzuri lakini anaanzisha safari na wewe. muelewani na muishi kama mke na mume hili sio jambo dogo hata kidogo.

 

Usipokuwa mvumilivu unaweza kuishi naye miezi sita, mwaka mmoja au miwili baada ya hapo uvulivu utakushishnda na utaamua kuachana naye ukiamini kwamba hawezi kuwa saizi yako. Pengine mtu sahihi si huyo labda atakuja hapo baadaye. Marafiki zangu, kwenye mahusiano lazima tukubali kuwa suala la kubebeana tabia lina umuhimu sana.

 

Hata kama tabia ni mbaya kiasi gani lakini kama kweli moyo wako unamhitaji mhusika, komaa naye. Hakikisha unautendea moyo wako kwa kumbadilisha. Unachotakiwa kujua tu ni kwamba, hakuna binadamu aliyemkamilifu. Kama kweli unaamini unampenda, muoneshe kama unampenda na kweli hakikisha anakuwa wako daima.

 

Kwa hatua zile za awali mkiwa ndio mnaanza mahusiano, hakikisha tu kwamba kweli uliyeanaye unampenda na unaamini anaweza kubadilika. Wekeza nguvu kubwa katika kumtengeneza mtu vile unavyotaka awe.

 

Kuna raha yake kumbadilisha mtu tabia. Siku zote wapendanao huwa wana jukumu la kufundishana, kuelekezana ili kuweza kufikia malengo ya safari yao. KOSA KUBWA Kosa kubwa ambalo huwa tunakosea ni kukata tamaa baada ya kuona mtu unayempenda anashindwa kubadilika kirahisi katika tabia fulani basi unakata tamaa. Komaa kumbadilisha, huyo ni wako utakuja kujivunia baadaye pindi atakapokuwa anakwenda kwenye mstari.

 

 

ANGALIZO

Hakikisha tu huyo mtu unayekomaa naye kuhusu tabia fulani basi anakubali kosa na analijutia. Kuna wengine ni wabishi, wanajua kabisa wanakosea lakini kamwe hawakiri kwamba wanakosea. Watu wa aina hiyo kidogo ni ngumu hata kuwabadilisha.

 

Anayebadilika huwa siku zote anakiri kosa. Anajua kweli anakosea na wewe kama mwenza wake huna budi kumsaidia namna bora za kuweza kuepukana na tabia ambayo mara nyingi huwa kama kilema. Si rahisi sana kumbadilisha mtu tabia lakini inawezakana, kwa nini ushindwe wakati unampenda? Penzi la kweli linajengwa na historia, halishuki tu kwa bahati mbaya.

 

Linasukwa na watu wanaojuana vizuri kwa muda mrefu ambao wamekubali kujitoa kusaidiana ili waweze kufurahia safari yao ambayo wanaitamani kwenda. Nikuache na msemo huu kutoka kwa mwandishi mashuhuri wa Marekani, Elbert Hubbard: “A friend is someone who knows all about you and still loves you.” Tafsiri isiyo rasmi; “rafiki ni yule ambaye anakujua udhaifu wako na bado anakupenda tu.”

Instagram & Facebook:

Erick Evarist

Twitter: ENangale.

Comments are closed.