The House of Favourite Newspapers

Ni Kweli Kuna Dawa Za Kuongeza Nguvu Za Kiume?-2

0

WIKI iliyopita tulieleza mambo mengi kuhusiana na tatizo la nguvu la kiume, tunaona jinsi madaktari na wataalamu wa lishe walivyojadili, leo tutaeleza kwa urefu chanzo cha mtu kukumbwa na maradhi hayo.

 

Endelea: Ni vyema tukajua mambo yanayosababisha mtu kupatwa na upungufu wa nguvu za kiume. Mambo yanayosababisha mwanaume akose nguvu za kiume wakati wa tendo la ndoa yapo mengi sana. Yafuatayo ni baadhi ya mambo hayo; UZEE. Kwa kijana ambaye kila siku anakuwa kiumri, hata uwezo wake wa kushiriki tendo la ndoa ndivyo hubadilika kutoka kwenye ujana, utu uzima na uzee.

Hivyo mtu anapofikia umri wa uzee, uwezo au nguvu zake za kushiriki tendo la ndoa hupungua, hivyo hatakuwa na uwezo kama wa awali. Mtu kama huyo anahitaji kuonwa na daktari kwani pia kuna uwezekano akawa na magonjwa yanayoshambulia mfumo wa damu pamoja na mishipa ya damu.

Damu ndiyo nishati inayowezesha mwanamme kuwa na nguvu za kiume wakati wa tendo la ndoa, na ili mwanamme aweze kuwa imara na mwenye nguvu, pamoja na kumudu na kustahimili tendo la ndoa wakati wowote, basi ni lazima awe na mfumo imara wa damu utakaoruhusu kutiririka kwa damu kwenda katika sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwamo sehemu ya siri.

 

Kwanza ili mfumo uweze kuwa imara ni lazima mhusika awe na damu ya kutosha, na pili awe na mishipa ya damu yenye afya. Kwa mujibu wa Dk. Leopord Mwinuka ambaye wiki iliyopita alieleza mengi katika sehemu ya kwanza ya makala haya, katika mwili wa mwanadamu, kuna mishipa inayotumika kusafirisha damu kutoka katika sehemu moja ya mwili kwenda katika sehemu nyingine ya mwili ikiwemo uume. “Mishipa hiyo ni kama vile vena (veins), atery (ateri) na capillary ( kapilari ). Mishipa hii ya damu inapaswa kuwa imara na yenye afya njema wakati wote,” anasema Dk. Mwinuka.

 

Lakini pia anasema; mishipa hii ikipatwa na hitilifu, basi itazuia kusafirishwa kwa damu katika sehemu mbalimbali za mwili wa mwanadamu na hatimaye kufanya suala la kuwa na nguvu za kiume kwa mhusika kuwa ugumu kwa sababu ya kushindwa kupeleka damu kwenye mishipa ya sehemu nyeti za kiume zinazofanikisha tendo la ndoa. Magonjwa kwenye mishipa ya damu huzuia kutirika kwa damu kwenye ogani muhimu kama vile moyo, ubongo, sehemu nyeti na figo. Dk. Mwinuka ambaye amekuwa akielimisha jamii kwa njia ya makala katika vyombo vya habari, anasema vipo viashiria vingi vya magonjwa kwenye mishipa ya damu.

 

Ukiwa una matatizo yafuatayo ya kiafya, ni ishara kwamba, una magonjwa kwenye mishipa yako ya damu. “Kolestrol ambayo inaitwa lehemu kwenye damu ikiwa nyinyi itazuia kutiririka kwa damu kwani
ikizidi kwenye damu, husababisha kuziba mishipa ya ateri ambayo kazi yake ni kupeleka damu kwenye uume, matokeo yake ni mhusika kukosa nguvu za kiume kwa sababu damu haitaingia inavyotakiwa kwenye mishipa ya uume. Hivyo basi, pamoja na dawa ya nguvu za kiume, yakupasa kutibu kolestrol,” anasema. Naye Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai anasema, unaweza kuondoa kolestrol kwenye damu kwa kutumia mimea mbalimbali kama vile mdalasini, uwatu, matikiti, mbegu za maboga na kadhalika. Anasema, matumizi ya mimea hiyo si hatarishi kwa sababu inaweza kutumika kama vyakula vya binadamu.

 

Tatizo lingine linaloweza kusababisha ukosefu wa nguvu za kiume ni mtu kuwa na ugonjwa wa shinikizo kubwa la damu (High blood pressure), kwani husababisha mishipa ya ateri ambayo hutiririsha damu iingiayo sehemu nyeti ya kiume kuziba na kushindwa kutanuka kwa kiwango inachotakiwa kutanuka. Pia huifanya mishipa laini ya sehemu hiyo kushindwa ku-relax na hivyo kushindwa kuizuia mishipa ya vena kunyonya damu kutoka kwenye mishipa ya uume na kuipeleka kwenye maeneo mengine ya mwilini. Matokeo yake kunakuwa hakuna kiasi cha kutosha cha damu iingiayo sehemu nyeti hivyo, kumfanya mhusika kuwa na tatizo la nguvu za kiume.

 

Pamoja na kutumia dawa ya nguvu za kiume, mgonjwa atapaswa pia kutumia dawa kujitibu tatizo la shinikizo kuu la damu. Ugonjwa wa kisukari Ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume. Kisukari huathiri mishipa ya damu pamoja na usambazaji wa damu kwenye ogani muhimu mwilini ambazo ni moyo, ubongo, figo na uume. Kiukweli, mwanamme mwenye kisukari yupo katika hatari kubwa ya kupatwa na tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume, tena katika kiwango kikubwa sana.

 

Mgonjwa unashauriwa pamoja na kutumia dawa ya nguvu za kiume, tumia dawa mbalimbali za hospitali au za asili kwa ajili ya kuweka sawa sukari yako mwilini. Zipo dawa mbalimbali zinazosaidia kuweka sawa kiwango cha sukari mwilini. Mtaalamu Mandai anasema, dawa za asili kama mdalasini, unga wa uwatu, mbegu za uwatu, manjano, majani ya manjano, mbegu za katani, na kadhalika husaidia kupunguza ongezeko la sukari kwenye damu. Dawa zote hizo huchanganywa kwenye maji ya moto kwa kiasi kinachotofautiana ndani ya glasi moja na kunywewa na mgonjwa.

 

MAGONJWA YA FIGO

Tatizo la ugonjwa wa figo huathiri vitu vingi ambavyo ni muhimu sana katika kumfanya mwanamme awe na uwezo wa kufanya tendo la ndoa. Tatizo la figo, huathiri homoni, huathiri kutiririka kwa damu kwenda kwenye mishipa ya uume, uathiri mfumo wa mishipa ya neva pamoja na nishati ya mwili mzima. Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply