The House of Favourite Newspapers

NI RAHISI KUWA NA MCHUMBA NA USIFANYE NAYE MAPENZI ?

NAMSHUKURU Mungu kwa mara nyingine tena kwa kunijalia fursa hii adhimu ya kuzungumza nanyi wapenzi wasomaji wa safu hii. Hakika Mungu ni mwema na tuendelee kumuabudu kwa kufanya yale aliyotuagiza na kuachana kabisa na yale yanayomchukiza.  Mpenzi msomaji wangu, leo nitazungumzia dhana ya wachumba kufanya mapenzi ikiwa ni hatua ya ‘kujuana vizuri’ kabla ya kuingia kwenye ndoa, pia nitagusia wanawake walio na tabia ya kubadili wanaume kila kukicha kwa nia ya kuchagua wachumba na hatimaye kujikuta wakiingizwa kwenye kundi la wahuni, malaya bila kutarajia.

Hapa siwazungumzii tu wale viruka-njia ambao kazi yao ni kubadili wanaume kwa staili ya kuwachuna bali nawagusa hata wale wake za watu ambao hujikuta kwa kutokuwa makini wanaolewa leo kisha baada ya siku chache wameachika kisha wanaolewa tena na tena.

Lakini niseme tu kwamba, kwa wewe ambaye umekuwa na msururu wa wanaume wengi mpaka leo hii uko na mtu sahihi, huna tatizo na hatuwezi kukuita mhuni au malaya kwani wataalam wa masuala ya mahusiano wanasema kuwa, safari ya kupata mwenza sahihi wa maisha ndiyo inayowaponza wengi na kujikuta wameingia katika kashfa ya kuwa na uhusiano na wapenzi kibao ndani ya muda mfupi. Wanasema msichana au mvulana anayeingia katika uwanja wa mapenzi kwa kuwa na hisia za kufanya ngono, hukosa umakini wa nani anafaa kuwa mpenzi wake kutokana na kukosa elimu ya uhusiano.

Kwa mantiki hiyo, bila upembuzi wa kina, mtu asiye na elimu ya jinsi ya kumpata mpenzi wa kweli hujikuta ameangukia kwa mtu asiyemfaa, ambapo baadaye huamua kuachana naye na kwenda kwa mwingine kujaribu bahati tena, huko kote anakopita anakuwa ameshafanya mapenzi. Zinatajwa zawadi, hitaji la kusaidiwa kimaisha, mvuto wa kimahaba na mazoea kuwa vichocheo vinavyowaingiza wengi kwenye wapenzi wasiowafaa.

Ukweli ni kwamba mtu aliyenaswa kwa ulimbukeni huo, huwa hakatwi kiu ya penzi na mtu asiye chaguo sahihi la maisha yake. Hivyo hufikia uamuzi wa kujiingiza katika uhusiano mpya mara nyingi na kujikuta akiambulia watu walewale wasio sahihi. Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Zawadi aliwahi kuniomba ushauri, akasema amechoka kuchezewa, maana kila mwanaume anayempata anakuwa si chaguo lake. Lakini kibaya zaidi huachia ngazi au hutemwa huku akiwa tayari ameshafanya mapenzi na wanaume hao.

Nia ya swali lake ilikuwa ni kuniomba njia za kumtambua mwanaume mkweli bila kufanya naye mapenzi. Aliuliza hivyo huku akiwa na hoja kuwa wanaume wengi hawako tayari kuwa na uhusiano na msichana bila kufanya naye mapenzi na wakati huohuo huficha tabia zao chafu wakilenga kumnasa wamtakaye.

Binafsi nafahamu kuwa kuna watu wengi ambao hujiingiza katika mapenzi kwa kutekwa na hadaa za mwili na kujikuta wanacheza mchezo wa pata potea. Labda nikuambie tu kwamba, unapompata yule ambaye moyo wako umemzimikia, jipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza. Keti chini na uanze kujumlisha alama za vigezo ulivyojiwekea na jinsi mtu huyo alivyopata au kukosa.

Ukiona uliyemchagua amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo ulivyoweka, tambua huyo anakufaa. Kuhusu alama chache alizokosa unaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati mko ndani ya uhusiano. Lakini pia unatakiwa kuwa makini sana pale ambapo utakayempata ataonesha kuharakisha suala la kufanya mapenzi na wewe. Kwa mfano, msichana unapokutana na mwanaume ambaye anaonesha kulazimisha penzi, huyo atakuwa amekutamani na ukimpa nafasi kwenye moyo wako, atakuja kukuliza.

Pia ikumbukwe kwamba, tendo la ndoa ni kwa ajili ya wanandoa, kwa hiyo hutakiwi kufanya hivyo kwenye hatua ya uchumba. Kikubwa hapa ni kujali maisha yako na kuhakikisha unaepuka kuwa na historia ya kuwa na wapenzi kibao ambao wameshaujua mwili wako kabla ya kuingia kwenye maisha ya ndoa.

Pia epuka sana kuwa na watu zaidi ya mmoja eti kwa lengo la kuwachunguza ili mmoja wao akionekana kuwa na muelekeo, umpe nafasi. Hii ni hatari sana kwani kama watajuana unaweza kujikuta unachafuka kwa kuitwa malaya kumbe huenda ulikuwa na nia njema ya kuwachunguza bila kufanya nao mapenzi.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

Comments are closed.