The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na mganga kwa tamaa ya cheo kazini-41

ILIPOISHIA:
Nilipofika mbele ya meza yake alisimama kabla hajasema neno, nilimuomba afumbe macho naye alifanya hivyo.
Kwa vile nilikuwa nimeshaufungua mkufu nilimvisha na kumfunga kisha nimweleza afumbue macho. Safia hakuamini alipouona mkufu wa thamani shingoni mwake. Alinikumbatia kwa furaha.
SASA ENDELEA…

“Waaaooo! Asante mpenzi wangu, Mungu akuzidishie uende salama, urudi salama pia akutangulie kwa kila jambo lako,” Safia alisema akiwa amenikumbatia kwa nguvu.
“Amen ndugu yangu, kizawadi changu ni hicho kidogo Mungu akijalia nikirudi salama nitakuletea kikubwa.”

“Kingine majaliwa lakini leo umenifanyia bonge la sapraizi, nashukuru sana shoga yangu Mungu akulipe mara mia.”

“Amen, basi shoga kuna mambo nataka niwahi nyumbani ili nijiandae kwa safari, muda wa kuwa nje na nyumbani ni mrefu kidogo.”
“Sawa dada, lakini usiache kuniaga kabla ya kuondoka.”
“Wewe tena? Lazima nikuage.”

Niliagana na Safia huku akili yangu yote ikiwa kwa babu Sionjwi kwenda kumchukua na kumpa zawadi yake. Nilipitia mjini kununua vitu kwa ajili ya familia yake. Kwa vile sikuwa na kitu chochote cha kunirudisha nyumbani kwa wakati ule nilikwenda kijijini kumchukua babu ili aje anipe raha kwa siku mbili nikiondoka niondoke nikiwa mwepesiii.

Kwa vile ilikuwa mapema, sikutembea mwendo wa kasi, nilikwenda kawaida na kutumia saa nne na nusu badala ya saa tatu nilizokuwa nikitumia njiani. Moyoni kila dakika moyo wangu ulichanua kwa furaha, nilijiuliza nitamtazamaje babu Sionjwi kwa muujiza alionifanyia.

Nikiwa nakaribia kwa babu na nyumba yake kuiona kwa mbali nilijiuliza nitamchukuaje babu ili aje mjini kulala nami kwa siku mbili. Kama nilivyokuwa nimepanga kulala naye nyumba ya wageni, nilikuwa nimeshachagua ambayo ipo nje kidogo ya mji.

Wazo la wasiwasi wa kushindwa kutoka sikulipa nafasi kwa kuamini babu tiba zake zote hakuzifanyia nyumbani, kuna muda alikuwa anatoka hata mwezi na kuwa nje ya nyumbani kwake hilo lilinipa faraja.

Gari lilisogea hadi kwenye uzio wa nyumba ya babu Sionjwi, nje kulikuwa na wakeze na watoto wakati ule babu alikuwa na watoto sita na kijacho wa shoga yangu Rose angekuwa wa saba. Walipoliona gari langu niliwaona sura zao zikitawaliwa na tabasamu kwa kujua mkombozi wao nimefika.

Nilisogeza gari sehemu ninayoliegesha kila nilipokwenda pale huku wenyeji wangu wakisogea kunipokea. Nilimuona shoga yangu Rose akijilazimisha kunyanyuka huku tumbo likitangulia mbele. Pamoja na kulakiwa na wake wa babu lakini shauku yangu kubwa ilikuwa kumuona babu, kiumbe mwenye maajabu chini ya jua anayeweza kugeuza nyeusi kuwa nyeupe.

Baada ya kuegesha gari na kulizima, nilifungua mlango ili nitoke, kwa mbali nilimuona babu Sionjwi akirejea na kapu la dawa. Bila kujitambua kuna watu wamekuja kunipokea nilifungua mlango na kutimua mbio kwenda kumlaki babu kwa kumkumbatia kwa vile nilikwenda mbio na nguvu tulijikuta wote tukienda chini.

“Waaaooo babuuu!”
“Mjukuu utaniua bure mwenyewe nimejiishia.”
“Babu unatisha.”

“Kwa nini mjukuu?” aliniuliza huku akinyanyuka nilipomuangushia nami nilinyanyuka na kuliokota kapu la dawa lililokuwa limeanguka pembeni.
“Nimeipata… nimeipata nafasi babu, mwisho wa wiki ninaondoka.”

“Hongera, mi mbona nilijua kila kitu mapema, sema wasiwasi wako tu.”
“Dah! Sasa itakuwaje?” ilibidi nimuulize kabla hatujafika kwa wakeze.
“Kuhusu nini?”

“Safari ya mjini maana nina muda wa siku mbili tu kabla ya kuondoka.”
“Wewe tu.”
“Kwa hiyo babu tunaondoka?”
“Kila nilichokuahidi ndicho kitakachokuwa.”

“Waaaooo.”
Itaendelea Risasi Jumamosi.

Comments are closed.