The House of Favourite Newspapers

Nini bongo fleva?… sasa ni singeli time

0

Man Fongo 'Mzee wa hauna' (2)Man Fongo.

BONIPHACE NGUMIJE

MIAKA ya nyuma mitaani kwetu ulikuwa huwaambii kitu watu hasa vijana wachakarikaji a.k.a Masela kuhusu Muziki wa Mnanda.

Nakumbuka long time kitambo ilikuwa muziki huo ukifungwa kitaani, lazima vijana wengi kutoka maeneo mbalimbali watafurika na staili yao ya kuucheza utafurahi na roho yako.

Licha ya kwamba vitendo vingi vya kihalifu vilikuwa vikifanyika kama vile wizi, ukabaji na ngono za kiholela, bado burudani ilikuwa bomba, si ajabu ukamkuta mtu akicheza peku, ndala kaweka mfukoni. Burudani zaidi ni kwamba hakuna staili maalum ya kucheza, utakavyojisikia ni poa tu.

msagasumu akiimba wimbo wa shemeji unanitegaMsaga Sumu

Enzi zile wakati muziki huo unatamba yapo makundi ambayo yalifanya freshi ndani na nje ya Bongo. Makundi hayo ni kama vile Jaguar Music na Seven Surviver alikopatikana mmoja wa wanamuziki wenye heshima ya pekee mtaani katika Muziki wa Mnanda, Juma Mpogo.

Taratibu muziki huo ukapoteza nguvu ya kusikilizwa baada ya Mchiriku kuingia kati na kina Dogo Mfaume kuchukua nafasi. Utakumbuka wimbo kama Kazi ya Dukani wa Dogo Mfaume ulivyofanya poa sana. Lakini mbali na huyo, nani asiyemkumbuka Omari Omari? Kama humkumbuki yeye utakuwa unaukumbuka wimbo wake wa Kupata Majaliwa.

sholo mwambaSholo Mwamba

Singeli Time

Kama walivyosema wahenga kila zama na nyakati zake, Mchiriku nao ukaenda unamezwa na nyakati, kwa namna nyingine tunaweza kusema uliboreshwa ikaibuka aina nyingine ya muziki mtaani ambayo ni gumzo kwa sasa inayoitwa Singeli ambapo mmoja wa waasisi ni Msaga Sumu.

Msanii huyu alianza kama mchezo ambapo moja ya ngoma zake za mwanzoni kabisa ni Mama wa Kambo.

Utakubaliana nami kuwa wakati Msaga Sumu anaibuka na kuimba Singeli watu wengi walikuwa hawamuelewi lakini taratibu baadhi ya vijana wakaanza kuelewa alichokuwa anakifanya.

Baadaye akaanza kupokea upinzani kutoka kwa ‘kichaa’ aliyezaliwa Mitaa ya Magomeni Kagera au Vinyasi kama wenyewe vijana wa mtaani ‘wahuni’ wanavyoita, Khalid Kapara ‘Babu’.

Upinzani huo ni kama ulichochea chachu ya wasanii kufumuka maana kufumba na kufumbua akaibuka kichaa mwingine wa Mburahati ambaye ‘wanaye’ wote wanapatikana Magomeni Kagera, Dogo Niga au Simela ambaye ngoma zake za Mjomba, Uzee Mwisho Chalinze, Twista na Usiniite Super Staa zikaanza kubamba.

Kumuelezea Dogo Niga pekee inaweza kunichukua hata kurasa zote za hili gazeti maana huyu mshikaji ni kichaa kwelikweli.

Kabla hajaanza kupotea na kumezwa na wasanii wengine walioibuka ambao ni kina Sholo Mwamba mzee wa Sembe Tembele, Mczo, Dulla Six Bullet, Virus ‘Mdudu Mmoja’ na Man Fongo mzee wa Hainaga Ushemeji, yalikuwa yanaandaliwa mapambano ya Singeli katika Ukumbi wa Manyara, Manzese halafu kila mmoja wao anaenda na wanaye.

Wakati Dogo Niga anatamba, hawa kina Man Fongo walikuwa wanamalizwa mapema tu pale anaposhika maiki, lakini wakati Muziki wa Singeli ukiwa unapamba moto yeye anaonekana kuanza kupotea!

Huko ndiko umetoka Muziki wa Singeli na kuonesha kuwa sasa ndiyo wakati wake. Fuatilia kwenye matamasha yanayoandaliwa kwa sasa, yawe ya Taarab au Bongo Fleva. Ni ukweli kuwa hawakosekani wazee wa Kisingeli.

Mbali na hiyo, wasanii wa Bongo Fleva Profesa Jay, Mensen Selekta, Chemical na Juma Nature wameingia katika anga za Singeli kwa kutoa ngoma au kushiriki kwenye ngoma za wakali hao wa Kisingeli.

Ni Singeli time, hakuna ubishi, ukifuatilia kuna wasanii wa Singeli kama Msaga Sumu, Man Fongo na Sholo Mwamba wanakunja mtonyo kupitia shoo zao kuliko baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva.

Leave A Reply