The House of Favourite Newspapers

Niyonzima: Kocha kayaelewa mambo yetu na Chama

Haruna Niyonzima

KIUNGO mnyumbulifu wa Simba raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima amesema kinachomfanya kocha wao Mbelgiji Patrick Aussems awapange kwa pamoja yeye na Clatous Chama ni staili yao ya kucheza ambayo kwa namna fulani inafanana, hivyo amegundua fursa ya vipaji vyao na kuviunganisha kwa haraka.

 

Simba, leo itashuka dimbani kupambana na timu ya Bandari ya Kenya kwenye mchezo wa nusu fainali wa michuano ya SportPesa Super Cup 2019, utakaofanyika ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Niyonzima alisema kuwa, tangu arejee kutoka katika majeraha ya muda mrefu amekuwa hapati nafasi vizuri kutokana na kocha kutomjua uwezo wake lakini kwa sasa tangu alipoona uwezo wake amekuwa akimtumia kiasi kwamba hata kuwachezesha na Chama kuna kitu alichokigundua anatamani kuwatumia kwa pamoja.

 

“Ukiangalia kipaji na namna ya uchezaji wangu na Chama hatupishani sana, kama kocha leo hii ameamua kututumia kwa michezo miwili basi kuna jambo ambalo analikusudia kwetu, nadhani mashabiki waendelee kutupa subiri tu kwani tukipata muungano tutaonyesha maajabu mkubwa,” alisema.

Comments are closed.