The House of Favourite Newspapers

NJEMBA AIBUKA SIKU YA MSIBA WAKE

SHINYANGA: Luhaga Madango (28) ambaye ni mkazi wa Kata ya Kambarage, Manispaa ya Shinyanga, amejikuta akiwekewa msiba nyumbani kwao huku akiwa hai mara baada ya kufananishwa na marehemu aliyefahamika kwa jina moja la Utumbo, ambaye aliuawa usiku wa kuamkia Septemba 19 mwa huu mjini hapa, kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

 

Kama ilivyo ada kwa gazeti la Uwazi, tukio la mauaji hayo lilifuatiliwa kwa kina na mwandishi wetu na kubainika kuwa lilitokea katika choo cha Shule ya Msingi Jomu, Manispaa ya Shinyanga.

Marehemu huyo aligunduliwa na wapita njia majira ya saa moja asubuhi, na kisha kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa huo wa Jomu, ambapo nao wakalitaarifu Jeshi la Polisi ambao walifika eneo la tukio na kisha kuondoka na marehemu.

 

Aidha, wakati wananchi walipokuwa wakijaribu kuutambua mwili huo wa marehemu, baadhi yao wakasema wanamfahamu kuwa ni Luhaga Mandago, ndipo walipofuatwa ndugu zake, walipofika eneo la tukio waliondoka na mwili wake wakiwa na Jeshi la Polisi hadi hospitali ya mkoa, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kisha kuuhifadhi mochwari kwa maandalizi ya mazishi.

 

Wakati taarifa hizo zikizagaa mitaani kuwa Mandago amefariki na msiba kuwekwa nyumbani kwao, ndipo jirani yake mmoja, Yusuf Ahmed akakutana naye na kumweleza juu ya tukio hilo na kumwambia awahi nyumbani ili ndugu na jamaa wakifika wamkute kuwa ni mzima hajafa, bali amefananishwa na marehemu.

 

“Baada ya kukutana naye Madango nikamwambia ndugu yangu sasa hivi wewe ni marehemu, umefananishwa na mtu ambaye ameuawa Shule ya Msingi Jomu, hivyo wahi nyumbani kwenu utakuta umewekewa msiba, ili wanazengo wakuone kuwa ni mzima hujafa,”alisema Ahmed. Gazeti hili lilifanikiwa kuonana na Madango na mahojiano yalikuwa hivi:

 

Mwandishi: Pole kwa yaliyokukuta, tueleze umejisikiaje kudhaniwa umefariki dunia?

Madango: Nimesikitishwa sana na tukio hilo, nilipopewa taarifa za msiba wangu nilikwenda nyumbani haraka na kukuta wanazengo wamekusanyika, huku ndugu zangu wakiwa wanalia kwa uchungu.

Mwandishi: Walipokuona mambo yalikuwaje?

Madango: Waliponiona hawakuamini macho yao kama ni mimi, walidhani mimi ni mzimu.

Mwandishi: Kwani hadi sasa hawaamini kwamba wewe siyo mzimu?

 

Madango: Kwanza niseme tukio hilo ni baya sana kwangu kwani hata sasa wanazengo hawaamini kama ni mimi, walikuwa wanaishi nami kwa mashaka kwa kunishangaa wakihofia kuwa huenda mimi ni mzimu. Sasa hivi siishi kwa amani kabisa, kwani wanazengo hawaamini kama mimi ni mzima wanadhani kuwa ni mzimu.

Mwandishi: Huwaeleweshi kuwa wewe hujafa?

 

Madango: Najaribu kuwa elewesha kuwa sijafa lakini bado wanamashaka, hivyo nawaomba kupitia vyombo vya habari waniamini kuwa mimi ni mzima, nilifananishwa tu na huyo marehemu ambaye hata simfahamu.

Kuna ndugu zangu wanaishi Kahama, walipigia simu na kunililia.

Mwandishi: Ulifanya nini kuondoa tatizo hilo kwao?

 

Madango: Kilichofanyika ni baadhi yao huko Kahama ilibidi wanitumie nauli niende wakanione.

Mwandishi: Baada ya kurejea kutoka Kahama sasa unafanya kazi gani?

Madango: Naendelea na shughuli zangu za welding kama kawaida.

 

Naye Dada wa Madango, Mary Luhaga alidai baada ya kumuona Madango walikwenda Polisi kutengua taarifa za msiba na kuwaambia kuwa mtu aliyeuawa siyo ndugu yao. Nao baadhi ya wanazengo wa Kata hiyo akiwamo Jafari Kumalija, alisema walipigwa na butwaa mara baada ya kumuona mtu aliyekuwa ni marehemu kutokea kwenye msiba akiwa hai, hivyo kwa haraka haraka hawakuweza kuamini na wenye mioyo miepesi walitimua mbio wakidai ni mzimu lakini kadiri siku zinavyokwenda, wanaanza kuamini kuwa Mandago ni mzima.

 

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simoni Haule, alithibitisha kutokea kwa tukio.“Hata hivyo Jeshi la Polisi halijafunga jalada la tukio hilo, bado linafanya uchunguzi juu ya mauaji hayo, ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya rufani ya mkoa,” alisema.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI

Comments are closed.