The House of Favourite Newspapers

NMB yakabidhi gawio la Shilingi Bilioni 10 kwa serikali

Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango DR Philip Mpango akipokea mfano wa hundi ya Shilingi Bilioni 10.17 kutoka kwa Mkurungenzi wa Benki ya Nmb – Ineke Bussemaker (kulia)  ikiwa ni gawio la Serikali, katikakati anayeshuhudia ni  Msajili wa Hazina Nchini  Athuman Mbutuka, makabidhiano hayo yalifanyika Wizara ya Fedha Jijini Dodoma.

Dodoma. Benki ya NMB jana ilikabidhi gawio la Shilingi Bilioni 10.17 kwa serikali kutokana na faida iliyopatikana mwaka 2017.

 

Pesa hizo ni sehemu ya jumla ya Shilingi Bilioni 32 ambazo ziliidhinishwa na mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa Benki ya NMB uliofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.

 

Katika mkutano huo, wanahisa waliidhinisha kutolewa kwa gawio la jumla ya Shilingi Bilioni 32 baada ya NMB kupata faida ya baada ya kodi ya Shilingi Bilioni 93.3 kwa mwaka 2017.

 

Akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya Shilingi Bilioni 10.17 kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker alisema benki yake imejikita katika kuhakikisha kuwa Watanzania wengi zaidi – hususani wakulima – wanapata huduma zakibenki popote pale walipo.

 

Alisema mbali na gawio la Shilingi Bilioni 10.17, NMB pia ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa nchini, ikiwa imelipa jumla ya Shilingi Bilioni 127 kama kodi mbali mbali za serikali kwa mwaka 2017 pekee.

 

“Pamoja na hayo, tunatenga asimilia moja ya faida yetu na kuipeleka katika kuboresha huduma zakijamii ambapo mwaka jana pekee tulinunua na kusambaza jumla ya madawati 6,000,” alisema Bi. Bussemaker.

 

Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 17 tu ya Watanzania watu wazima ambao humiliki akaunti katika benki za biashara.

 

Kutokana na hali hiyo, NMB imeongeza juhudi za kuhamasisha wakulima wafungue akaunti ambapo kwa mwaka jana pekee, jumla ya akaunti 300,000 zilifunguliwa na kuiwezesha benki kuongeza idadi ya wateja kufikia jumla ya milioni 2.7.

 

Akizungumza kabla ya kukabidhiwa mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.17, Dk Mpango aliishukuru NMB kwa kuendelea kupata faida licha ya kukiri kuwa mwaka jana (2017) ulikuwa na changamoto nyingi kwa sekta ya fedha.

 

“Mwaka 2017 haukuwa mzuri kwa sekta ya fedha ila ninayo furaha kujua kwamba NMB iliweza kupata faida na leo wanatoa gawio kwa Watanzania maskini…Hii inadhihilisha ukweli kwamba NMB inao uongozi na usimamizi madhubuti katika utoaji wa huduma zake,” alisema Dk Mpango.

 

Aliuhakikishia uongozi wa NMB kuwa gawio hilo litatumika kwa malengo yaliyokusudiwa huku akitoa rai kwa kampuni nyingine zote ambazo kuna hisa za serikali kuiga mfano wa NMB na kuanza kutoa gawio.

 

Benki ya NMB ina jumla ya matawi 220 nchini. Kupitia NMB Wakala, huduma zake pia hupatikana katika vituo 6,000 nchini kote huku ikiwa na lengo la kufikisha idadi ya mawakala 10,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Comments are closed.