The House of Favourite Newspapers

NMB Yazindua Kampeni ya ‘NMB Mastaboda- Miliki Chombo’

0
Katika picha ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (mbele) Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna,(katikati ndani ya Bajaj) na Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, (kushoto anayeshuhudia tukio).

BENKI ya NMB imezindua Kampeni ya NMB MastaBoda ‘Miliki Chombo,’ inayotoa mikopo ya pikipiki za miguu miwili na mitatu kwa watoa huduma wa Sekta ya Usafirishaji ‘Bodaboda na Bajaj’, ambako imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 5 za kufanikisha mikopo hiyo kwa mwaka wa kwanza.

 

Uzinduzi wa NMB MastaBoda Loan umefanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ambaye awali Oktoba 2019, aliiomba NMB kufikiria namna ya kuwawezesha vijana wanaohudumu katika Sekta hiyo kote nchini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna akizungumza jambo.

Akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema benki yake ililipa uzito ombi la Waziri Mhagama na kwa nia ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuipatia suluhu changamoto ya ajira, ikaona ianzishe mikopo hiyo kwa maslahi mapana ya ustawi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 

“Tumetenga kiasi cha Sh. Bilioni 5 kwa ajili ya NMB MastaBoda Loan katika mwaka huu wa kwanza na kukiwa na mwitikio mzuri miongoni mwa wakopaji, basi hatutosita kuongeza kiasi hicho ili kuwafikia walio wengi kote nchini. Wakopaji watakuwa na ‘QR Code’ za kupokelea malipo yao na kuingizwa moja kwa moja katika akaunti zao za NMB.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akionesha msisitizo wa jambo.

“Kwa utaratibu huo, kundi hili litarasimisha  mapato yao na kusaidia kukuza biashara zao na uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla. Hapa tunao vijana zaidi ya 350 waliohudhuria, ambao wana akaunti na wanakopesheka kwa mujibu wa vigezo, hasa baada ya awali kuwaunganisha kupitia Kampeni ya NMB MastaBoda uliyoizindua mwaka 2019,” alisema Zaipuna.

 

Bi. Ruth aliongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kuna waendesha bodaboda zaidi ya milioni mbili kote nchini, ambao kabla ya NMB MastaBoda walikuwa wameajiriwa, wakiwa nje ya mifumo rasmi ya kibenki na hivyo kukosa fursa nyingi za kiuchumi na kifedha, lakini sasa NMB imejikita katika kuwawezesha kujiajiri na kuwarasimisha kwenye Sekta ya Usafirishaji kwa njia ya pikipiki.

Kwa upande wake, Waziri Mhagama aliipongeza NMB sio tu kwa kulifanyia kazi haraka ombi lake la kuanzisha mikopo ya pikipiki, bali pia kwa namna inavyoendesha huduma zake kwa uzalendo mkubwa kwa Taifa, ikipambana sambamba na Serikali katika vita ya kutokomeza tatizo la ajira miongoni mwa makundi mbalimbali ya kijamii nchini.

 

“NMB chini ya uongozi wa Mkurugenzi, Ruth Zaipuna, imeonesha uzalendo wa kiwango cha juu kwa kuzivalia njuga changamoto za ajira kwa vijana. Serikali tunawapongeza na kuwaunga mkono, huku tukiamini Sh. Bilioni. 5 zilizotengwa zitachangamkiwa na vijana, kisha kiwango hicho kitapanda hata kufikia Sh. Bilioni 20. Naziomba benki nyingine ziige utamaduni huu wa NMB kwa kuyaangalia makundi mengine.

Uzinduzi rasmi ukifanyika.

“Wito wangu kwa NMB ni kuharakisha kuwafikia vijana wengine walio nje ya Dar es Salaam ili kuwapa fursa hii ya mikopo. Vijana nanyi tumieni vema mikopo hii na kuichagiza NMB kutanua huduma na kuanza kufikiria kuwakopesha magari. Fikeni matawini, kopeni, rejesheni kwa wakati, lakini pia wafichueni madereva wasio waaminifu wanaoichafua Sekta ya Usafirishaji kwa njia ya pikipiki,” alisisitiza Waziri Mhagama.

 

Akaongeza kwa kuahidi kuwa Serikali itaendelea kupambana kuzitafutia ufumbuzi changamoto za ajira, ikiwemo kuhakikisha Sekta ya Usafirishaji kwa pikipiki inabaki kuwa rasmi, kwani kwa kuirasmisha kutasaidia pesa za bodaboda hao zinatunzwa katika mifumo ya kibenki na kusaidia kwenye mzunguko wa ukuaji wa uchumi wa Taifa na watu wake.

 

Naye Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema ili mtu aweze kuwa na sifa za kukopa pikipiki anatakiwa kuwa mtumiaji wa MastaBoda QR, awe mteja wa NMB kwa takribani miezi mitatu, awe na kitambulisho cha Taifa (NIDA), awe mwanachama wa kikundi kilichosajiliwa cha Wamiliki na Waendesha Bodaboda kinachotambulika na NMB na awe pia na leseni ya udereva.

 

“NMB MastaBoda Loan ni namna sahihi na bora ya kuboresha uwajibikaji wa madereva bodaboda, ambao mchango wao kwenye uchumi wa Taifa kwa Sasa unatambulika. Leo ni zamu ya Dar es Salaam, lakini baadaye tutazindua huduma hii kwenye mikoa ya Mwanza, Arusha, Ruvuma, Dodoma, Morogoro, Mtwara na Mbeya na baada ya hapo tutasambaza huduma hii kote nchini.

 

“Hapa katika uzinduzi tuna bodaboda zaidi ya 350, lakini ieleweke kuwa tayari NMB imeshawajengea uwezo zaidi ya bodaboda 5,000 na tunategemea kuwafikia zaidi ya madereva 75,000 kote nchini kuwaelimisha kuhusu mikopo hii na namna ya kutumia Mastercard QR kufanikisha malipo kwa simu za mkononi,” alisisitiza Mponzi wakati wa uzinduzi huo.

 

NMB MastaBoda Loan inampa mkopaji muda wa miezi 12 hadi 24 kulipa pikipiki anayopaswa kukopa kwa kutoa asilimia 20 ya malipo ya awali, ambako chombo husika (pikipiki ya miguu miwili au mitatu), kitakatiwa bima kubwa, pamoja na kufungwa kifaa cha usalama na kuifuatilia (tracking system), yote hayo yakifanywa katika mkopo wenye marejesho nafuu na wezeshi.

Leave A Reply